Katika kuhakikisha Watanzania wengi wanatumia huduma za bima na kufikia lengo la asilimia 50 ifikapo mwaka 2029/30, Benki ya NMB imezindua msimu wa tano wa kampeni ya UmeBima. Kampeni hiyo itakayokuwa na kauli mbiu isemayo: ‘Ni Kubofya tu’, inaakisi mapinduzi ya kidijitali yanayoletwa na benki kwenye sekta ya bima nchini.
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika Jumanne Aprili 29, 2025 jijini Dar es Salaam, umekwenda sambamba na utambulisho wa maboresho ya kimkakati ya huduma za bima kupitia ushirikiano baina ya NMB na Shirika la Bima la Taifa (NIC). Katika ushirikiano huo, kuanzia sasa mifumo ya taasisi hizo kongwe na kubwa katika sekta ya fedha na bima nchini, itasomana.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Idara ya Bima wa Benki ya NMB, Martin Masawe, amesema kampeni hiyo inalenga kutambulisha kwa umma juu ya mapinduzi ya kidijitali kwenye utoaji wa huduma hiyo, ambapo sasa wanaweza kununua bima za vyombo vyao vya moto kwa urahisi kupitia simu zao za mkononi.

“Huu ni msimu wa tano wa UmeBima, lakini kampeni hii ilianza mwaka 2021 tulipoiita UmeBima, ikaja UmeBima ‘Sio Ngumu Kihivyo,’ kisha ikafuata UmeBima ‘Teleza na Bima’ katika msimu tatu, msimu wa nne tukaiita UmeBima ‘Haachwi Mtu’ na sasa ni kidijitali zaidi ‘Ni Kubofya tu’.
“Huduma hii imelenga kurahisisha mfumo wa upatikaniji wa huduma za bima kwa kumuondolea mteja usumbufu wa kusafiri kufuata huduma hii kwenye matawi.
Masawe ametumia nafasi hiyo kutambulisha maboresho ya huduma za bima kupitia ushirikiano wao na NIC, ambao ulianzishwa rasmi mwaka 2020 huku NMB kama Wakala wa Bima za Mali wa NIC, ulilenga kuleta mapinduzi makubwa katika upatikanaji wa huduma za bima kwa Watanzania wote.
“Katika jitihada za kuboresha zaidi huduma hii muhimu, sasa wateja wanaweza kupata namba za malipo (control number) papo hapo, hii ni baada ya mifumo yetu na ya NIC kusomana na kuondoa utaratibu wa kumsubirisha mteja kwa muda mrefu.
Naye Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa NIC, Karimu Meshack, amesema shirika hilo lina furaha kubwa kufanikisha mchakato sio tu wa maboresho ya kimkakati, bali kuwezesha kusomana kwa mifumo ya NIC na NMB, akiamini itachochea ukuaji wao kibiashara katika zama za teknolojia.
“Ulikuwa mchakato wa muda mrefu uliolenga kuendana na dunia ya sasa ambayo ni ya kidijitali, ambayo ili ufanye vema biashara na kuwafikia wengi, unapaswa kufanya uwekezaji katika teknolojia, hasa katika nchi kama yetu ambayo elimu ya bima ipo chini, lakini pia hata watumiaji wa bima ni wachache.
“Na hasa katika hii sera ya Rais Samia Suluhu Hassan ya bima kwa wote, inakulazimisha kuhakikisha mitandao ya kidijitali inakuwa sehemu ya mchakato.
“Baada ya maboresho, tumeungana na NMB katika Kampeni ya UmeBima ‘Ni Kubofya tu,’ na sisi tukiwa na NIC Kiganjani na Chatbot wetu. Kwa hiyo huko kote utakakopita utakutana na NMB na NIC katika kuhakikisha bima kwa wote inafika kwa kila Mtanzania,” amebainisha Meshack.