Bao pekee la ushindi alilofunga Ousmane Dembele limevunja mwiko wa PSG kutopata matokeo ya ushindi mbele ya Arsenal.
Bao la dakika ya nne alilofunga mshambuliaji wa PSG, Ousmane Dembele limetosha kuipa ushindi timu yake hapo jana dhidi ya Arsenal katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye uwanja wa Emirates.
Dembele amekuwa na wakati mzuri msimu huu akiwa amehusika kutengeneza mabao 27 kwenye Ligi One ya Ufaransa akifunga 21 na kutoa kupiga pasi za mwisho sita wakati kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya amehusika katika mabao 11 akifunga nane na kupiga pasi za mwisho tatu.
Nyota huyu wa Ufaransa jana amethibitisha makali yake baada ya kuingizia mpira wavuni kwenye uwanja wa Emirates na kuitanguliza PSG mguu mmoja kwenye fainali ya mashindano hayo.
Arsenal ina mtihani wa kupindua matokeo ya bao moja katika mchezo wa marejeano utakaofanyika Mei 7 mwaka huu ambapo itatakiwa kupata ushindi wa kuanzia mabao 2-0 au 3-1 ili kusonga katika hatua ya fainali.
Huu ni ushindi wa kwanza kwa PSG kwani katika michezo mitano iliyopita Arsenal imeshinda mechi mbili na kupata sare tatu. Mara ya mwisho timu hizi kukutana ilikuwa Oktoba Mosi mwaka jana ambao Arsenal ilipata ushindi wa mabao 2-0 kwenye uwanja wa Emirates.
Katika mchezo wa jana PSG ilimiliki mpira kwa asilimia kubwa kuliko Arsenal huku wakikosa baadhi ya nafasi za wazi walizotengeneza. Kama asingekuwa golikipa wa PSG, Gianluigi Donnarumma kuokoa michomo ya Gabriel Martinel na Leandro Trossade huebda washika mitutu wa London wangebadilisha matokeo.
Arsenal imesalia katika mashindano ya UEFA msimu huu baada ya kushindwa na Liverpool katika kuwania mbio za ubingwa wa EPL ambao imetoka kuutangaza Jumapili Aprili 27 baada ya kuifunga Tottenham mabao 5-1 na kufikisha jumla ya pointi 82 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine huku Arsenal ikisalia katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 67.

PSG imetwaa ubingwa wa Ligue One ya Ufaransa ambapo mpaka sasa inashika usukani kwenye Ligi hiyo ikiwa na pointi 78 dhidi ya Marseille inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 58.
Timu zote mbili zinahitaji kuvunja mwiko wa kutochukua ubingwa wa UEFA kwani Arsenal imeshacheza fainali mara moja mwaka 2006 ikipoteza mabao 2-1 dhidi ya Barcelona wakati PSG yenyewe ilifika fainali mwaka 2020 ikipoteza bao 1-0 dhidi ya Bayern Munich.
Ligi ya Mabingwa Ulaya itaendelea tena leo ambapo utachezwa mchezo mwingine wa nusu fainali utakaozikutanisha Barcelona ambayo itakuwa nyumbani kuikabili Inter Milan kwenye uwanja wa Olympic Luis, Cataluña.