Madrid, Hispania. Shirikisho la mpira wa miguu Hispania (RFEF) limempa adhabu beki wa Real Madrid, Antonio Rudiger ya kutocheza mechi sita za Ligi Kuu Hispania maarufu kama La Liga.
Adhabu hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na ripoti ya mwamuzi wa mchezo wa fainali ya Kombe la Mfalme (Copa del rey) uliowakutanisha Real Madrid na Barcelona Jumamosi, Aprili 26 kwenye uwanja wa La Cartuja, Sevilla ambapo Barcelona ilitwaa taji hilo kwa kuichapa Madrid mabao 3-2.
Refa wa mchezo huo Ricardo De Burgos katika ripoti yake amesema kwamba Rudiger (32) alipewa kadi nyekundu kwa sababu ya kurusha kitu uwanjani kutokea katika eneo la benchi la ufundi ambacho kilimkosa refa huyo.

Katika mchezo huo Rudiger alionekana akirusha uwanjani kipande cha barafu alichokuwa ameshika mkononi ambacho kilimkosa refa huyo baada ya benchi la ufundi la Madrid kusimama likidai beki wa Barcelona, Eric Garcia amemchezea vibaya Kylian Mbappe.
Michezo sita aliyofungiwa Rudiger itahesabiwa katika mechi za Ligi Kuu Hispania, La Liga ambapo atakosekana katika michezo mitano iliobaki kwenye Ligi Kuu pamoja na mchezo wa kwanza wa msimu ujao.
Katika michezo mitano iliyobakia upo wa El Clasico ambao utawakutanisha tena na mahasimu wao Barcelona, Mei 11 mwaka huu.
Hata hivyo, kabla ya kupewa adhabu hiyo na Shirikisho la Soka Hispania (RFEF), Real Madrid ilithibitisha kuwa beki huyo raia wa Ujerumani atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki sita hadi nane kutokana na majeraha ya goti.

Rudiger anatarajiwa kurejea uwanjani katika mashindano ya Kombe la Dunia la klabu yatakayoanza kutimua vumbi Juni 15 mwaka huu huko Marekani ambapo Real Madrid imepangwa kundi H na timu za Al Hilal (Saudi Arabia), CF Pachuca (Mexico), pamoja na Salzburg ya Australia.
Mbali na Rudiger, Shirikisho la Soka Hispania (RFEF) limemfutia kadi nyekundu Jude Bellingham huku Lucas Vazquez akipewa adhabu ya kukosa michezo miwili ya Kombe la Mfalme (Copa del rey) msimu ujao kutoka na kadi nyekundu ya moja kwa moja aliyoonyeshwa kwenye fainali hiyo.