
Tangu Donald Trump arejee katika Ikulu ya White House, mashambulizi yameongezeka dhidi ya Afrika Kusini, ambayo imekuwa mojawapo ya shabaha kuu za rais huyo wa Marekani. Miongoni mwa shutuma zake kuu: nchi hiyo inawatendea vibaya raia wake kutoka jamii ya walio wachache, walioalikwa kuja na kuishi Marekani kama wakimbizi.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Na mwanahabari wetu mjini Johannesburg, Claire Bargelès
Donald Trump anaungwa mkono na Elon Musk, mzaliwa wa Pretoria, ambaye hawezi kuzindua kampuni yake ya Starlink nchini Afrika Kusini. Siku hizi 100 za kwanza za Donald Trump tangu achukuwe madaraka kama rais hazijakuwa rahisi kwa Pretoria.
Mvutano kati ya Afrika Kusini na Marekani ulifikia kilele mwezi uliopita wakati balozi wa Afrika Kusini mjini Washington alipoamriwa kuondoka nchini humo baada ya kuzitaja sera za rais wa Marekani kuwa za “ubabe.” Lakini ugomvi unarudi nyuma zaidi. Tayari wakati wa muhula wake wa kwanza, Donald Trump alishutumu kile alichokiita “kunyang’anywa ardhi kutoka kwa wakulima wazungu,” kutokana na nadharia za mauaji ya kimbari ya wazungu ambayo pia yanashirikiwa na Elon Musk. Donald Trump na Elon Mus, wote wawili wanaikosoa Afrika Kusini kwa sera zake za ugawaji upya wa ardhi, ingawa Pretoria inakanusha unyakuzi wowote kiholela.
Mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Afrika Kusini
Wiki mbili baada ya kuapishwa kwake, rais wa Marekani alianza tena mashambulizi yake kwenye mada hii kwenye mtandao wake wa kijamii, kisha akatangaza kwamba amekata misaada yote kwa Afrika Kusini. Kufuatia hili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alikataa kusafiri kwenda Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa maandalizi wa G20. Nchi hiyo ilipigwa na ushuru wa 30% wakati wa wimbi la ushuru mpya wa forodha, tangu kusimamishwa.
Ikumbukwe pia kwamba Pretoria ni mmoja wa washika viwango wa kadhia ya Palestina, haswa kutokana na malalamiko yake dhidi ya Israeli mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ), hali ambayo haiufurahishi utawala wa Trump, mtetezi wa dhati wa Waziri Mkuu wa sasa wa Israeli, Benjamin Netanyahu. Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa hivi karibuni alizungumza kwa simu na mwenzake wa Marekani, na kwa mujibu wa ofisi ya rais wa Afrika Kusini, wawili hao wanatarajiwa kukutana ana kwa ana hivi karibuni.