
Aliposhika madaraka, Rais Samia Suluhu Hassan alionyesha siyo tu nia kwa maneno, bali pia kwa matendo kwa kuchukua hatua mbalimbali zilizolenga kuliponyesha Taifa.
Rais Samia alikutana na makundi mbalimbali ya kijamii, wakiwemo viongozi wa dini, kisiasa na kimila kujadiliana juu ya mustakabali wa Taifa.
Alizuia ukusanyaji wa kodi kimabavu kupitia vikosi kazi, kesi za kisiasa zilifutwa na marufuku haramu ya shughuli za kisiasa kuondolewa.
Hatua hizo za Rais Samia ambaye ni mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo zililenga kuliondoa Taifa kutoka kwenye fukuto siyo tu la kisiasa, bali pia hofu iliyotanda karibia katika maeneo yote wakati wa uongozi wa miaka saba ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Katika miaka hiyo ya giza, nikiazima maneno ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Dk Anthony Diallo wakati wa mahojiano yake na kituo kimoja cha runinga, hakuna Mtanzania aliyekuwa na uhakika wa kesho endapo tu maoni na mawazo atakayotoa yanaweza kukinzana na mamlaka.
Wanasiasa, wafanyabiasha, wasanii na hata wananchi wa kawaida wote walionja joto la jiwe.
Viongozi na makada wa vyama vya shindani (wengi wanaviita vyama vya upinzani) hawakuwa na uhakika wa uhuru wao pindi wanapofanya shughuli au kutoa kauli na maneno ya kisiasa.
Baadhi yao walijikuta mikononi mwa Jeshi la Polisi na kusota mahabusu kwa kipindi kirefu, kufunguliwa kesi mahakamani na kunyimwa dhamana, hata kwa mashauri yenye dhamana lilikuwa jambo la kawaida katika kipindi fulani.
Kwa kifupi, Taifa lilikuwa katika kipindi cha giza kiasi cha utii wa Katiba na utawala wa sheria kuwekwa kando, huku baadhi ya viongozi, watendaji na watumishi katika ofisi za umma, vikiwemo vyombo vya dola wakifanya watakalo bila hofu.
Ni katika kipindi hicho, Jeshi la Polisi lilizuia isivyo halali mikutano ya kisiasa na kuingilia hata vikao vya ndani vya vyama vya upinzani.
Wafanyabiasha nao hawakubaki salama, kwa kuwa ni miongoni mwa walioonja joto la jiwe kutoka kwa vikosi kazi vya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambavyo siyo tu vilikusanya kodi kwa vitisho, bali pia vilitoa makadirio ya juu yasiyolipika.
Wapo baadhi ya wafanyabiashara walijikuta biashara na akaunti zao za benki zikifungwa, huku kukiwa na madai ya fedha kukwapuliwa katika akaunti zilizofungwa.
Wapo watu walilazimika kukiri makosa mahakamani baada ya kuingia makubaliano na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka (DPP) kwa kulipa faini na fidia kukwepe kusota mahabusu kwa muda mrefu.
Japo wapo wanaoweza kubisha, lakini kuna dalili zimeanza kuonekana katika siku za karibuni kuwa baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali, hasa vyombo vya ulinzi na usalama, likiwemo Jeshi la Polisi wanataka kulirejesha Taifa katika fikra za kipindi kile cha giza.
Matukio ya viongozi wa vyama vya siasa, hasa Chama cha Demokasia na Maendeleo (Chadema) kutiwa mbaroni na Jeshi la Polisi na baadhi yao kushtakiwa kwa makosa yanayotokana na maneno na hoja zao za kisiasa ni mfano hai.
Dalili hizo zilianza kuonekana Agosti, 2024 baada ya viongozi wakuu wa Chadema, akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe kutiwa mbaroni jijini Mbeya walipokwenda kuhudhuria kongamano la maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa chama hicho, (Bavicha). Matukio ya matumizi ya nguvu ya Jeshi la Polisi dhidi ya wananchi na wafuasi wa Chadema waliofika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza kesi dhidi ya Mwenyekiti wao Tundu Lissu pia yanaturejesha enzi zile za giza.
Dalili za baadhi ya viongozi na watendaji serikalini na vyombo vyake kutamani kila mtu kusifia na kupongeza bila kutoa hoja au maoni kinzani pia zinatukumbusha na kuturejesha kwenye enzi za giza ambazo kwa hakika hatustahili kurejea.
Vitendo vya kuminya haki na wajibu, ikiwemo uhuru wa maoni, uhuru wa kukutana, kujiunga katika makundi, ulinzi wa umma na Taifa siyo tu ni kinyume cha sheria, bali pia vinakiuka Ibara ya 12 hadi 28 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Ni rai yangu kuwa viongozi ndani ya Jeshi la Polisi na taasisi nyingine za Serikali wajitahidi kujiepusha na matendo yanayohujumu nia njema ya Rais Samia ya kuliponya Taifa kutoka enzi ya giza.
Lakini pia hata vyama vya upinzani navyo vijifunze namna njema ya kuwasilisha hoja zao pale wanapobaini mambo hayajaenda sawa. Kupimana ubavu na vyombo vya dola haina afya.
Nasisitiza mazungumzo ndiyo njia sahihi ya kumaliza sintofahamu baina yao.
Peter Saramba ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa; anapatikana kupitia [email protected] au 0766434354.