Wito wa amani budi uambatane na haki

Kila anapozungumza iwe na wananchi sehemu mbalimbali, mikutano, semina, misikitini au akiwa na mabalozi wa nchi za nje, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi hutoa tamko la kuhakikisha uchaguzi ujao utakuwa wa amani, huru na wa haki.

Hii ni kauli inayotoa matumaini mema wakati huu ambapo joto la uchaguzi linapanda, huku kukiwa na mashaka ya kurudiwa yaliyodaiwa kuharibu chaguzi za vyama vingi zilizopita, ambazo ziligubikwa na vurugu na mizengwe.

Hata uchaguzi wa 2020 ulielezwa na baadhi ya watazamaji wa ndani na nje kukosa sifa za kuwa uchaguzi ulio huru na wa haki.

Kada maarufu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ambaye alijijengea sifa ya kuhimiza utawala bora, alikiri kabla ya kustaafu wadhifa wa Katibu Mkuu wa chama hicho kuwa uchaguzi uliopita, Zanzibar na Bara, ulikosa sifa za kuwa wa huru na wa haki.

Uchaguzi wa 2020 ulikumbwa na matukio mengi, ikiwa ni pamoja na watu kupotea, kujeruhiwa na hata kuuawa.

Majimbo ambayo daima yalikuwa ngome za upinzani, kama Mji Mkongwe na Pemba, ACT-Wazalendo yalichukuliwa kirahisi na CCM kana kwamba ghafla maeneo hayo yaligeuka kuwa ngome za chama hicho.

Kwa sasa, mbio za kuelekea uchaguzi mkuu ujao zimeanza, huku kelele za kudai kuwa mazingira ya kuelekea uchaguzi huo si sawa zikisikika.

Ni CCM pekee inayoweza kubandika mabango na karatasi za kampeni barabarani na kwenye nyumba na maduka ya watu bila ridhaa yao, huku vyama vingine vikisubiri kampeni kuanza rasmi.

Kelele za kutaka Katiba iheshimiwe kwa kuhakikisha uchaguzi wa Rais unafanyika siku moja badala ya sheria inayoruhusu uchaguzi wa siku mbili zimekuwa zikigonga mwamba.

ACT – Wazalendo wanadai kuwa siku ya pili imewekwa kimakusudi kuruhusu mizengwe ya watu kupiga kura mara mbili katika vituo vya siri, ambavyo vinakosa uwazi wa kinachofanyika.

Hili linapaswa kuangaliwa kwa umakini, kwa sababu iwapo Tanzania Bara na nchi jirani zinaweza kufanya uchaguzi wa siku moja, ni kwa nini Zanzibar yenye majimbo madogo ya ukubwa wa chini ya nusu kilomita, ihitaji siku mbili?

Wapinzani walidai kuwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa mwaka 2020, alikuwa kinara wa kasoro zilizokithiri, lakini amepewa tena jukumu la kusimamia uchaguzi ujao.

Hili linaongeza mashaka, hata kama kuna ahadi za kuwa uchaguzi utakuwa wa uadilifu. Methali ya Kiswahili yasema, “Aliyezowea vya kunyonga, vya kuchinja haviwezi.”

Kulikuwa na shida gani ya kumbadilisha mtu huyo ili kuondoa mashaka? Au tunataka kuambiwa kuwa mtu huyo ana ujuzi wa kipekee ambao haupatikani kwa mtu Manzibari mwingine.

Katika chaguzi zilizopita, wagombea wa upinzani, wakiwamo mawaziri wa zamani na wawakilishi, walizuiliwa kugombea kwa madai ya dosari katika fomu zao, lakini hili halikuwahi kuwakumba wagombea wa CCM.

Wasiwasi uliopo sasa ni kwamba huenda mizengwe kama hiyo ikajirudia, kwa sababu waliohusika na ukiukwaji wa haki za uchaguzi hawakuwahi kuwajibishwa kisheria, kana kwamba mwenendo huo ni halali.

Masheha walikataa kuwaandikisha vijana waliowaoa mabinti zao na hata watoto wao kwa madai kwamba hawawatambui, lakini walikuwa tayari kuwasaidia katika shida zao za kila siku.

Watu waligunduliwa kuwa wameandikishwa kupiga kura mara mbili au tatu katika vituo tofauti, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yao.

Kwa sasa, yapo madai kuwa vitambulisho vya Mzanzibari vinatolewa kwa wageni kama njugu, huku wazaliwa wa Zanzibar wakinyimwa haki hiyo.  Hili linatia mashaka na linaweza kusababisha vurugu iwapo watu hao watazuiliwa kupiga kura.

Wito wangu kwa Serikali, madai hayo yafuatiliwe kwa kina na yasipuuzwe, kwani mchelea mwana kulia hujikuta akilia mwenyewe. Kila uchaguzi unapofanyika, hujitokeza makundi ya watu wanaoitwa “Janjaweed” na “Mazombi” wanaopiga watu ovyo barabarani na nyumbani, na hata kuua bila kukamatwa. Je, safari hii tutaepuka hali hiyo?

Katika chaguzi zilizopita, wagombea na wapigakura walipigwa, wengine kuuawa na madai ya ubakaji kusikika, lakini hakuna hata kesi moja iliyofunguliwa.

Mpaka leo hakuna anayeweza kusema nini kilichompata kada maarufu wa CCM, Khamis Musa, aliyekuwa Kamishna wa Bajeti na aliyekuwa akihusishwa na nia ya kugombea urais wa Zanzibar.

Tunapozungumzia umuhimu wa amani na uchaguzi usiwe chanzo cha umwagaji damu, lazima kuhakikisha mazingira ya uchaguzi yanakuwa mazuri, hakuna uonevu na uchaguzi uonekane kuwa huru na wa haki kwa vitendo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *