Robert Matano safari imewadia Fountain Gate?

INAELEZWA kwamba Kocha wa Fountain Gate, Robert Matano anaweza kutoendelea na timu hiyo kwa msimu ujao kutokana na kushindwa kuipa matokeo yaliyotarajiwa.

Matano ambaye ameiongoza Fountain Gate kwenye mechi 11 za Ligi Kuu Bara, tangu Januari 10, mwaka huu alipochukua nafasi ya Mohammed Muya, amefanikiwa kushinda mbili za ugenini Ligi Kuu Bara ilipozichapa KMC 2-1 kisha Tanzania Prisons 1-0.

Katika mechi tatu ameambulia sare na vipigo sita, akivuna pointi tisa. Kwa ujumla timu hiyo ina pointi 29 ikiwa nafasi ya 12 kwenye msimamo ikicheza mechi 27.

“Bado hatujafikia uamuzi wa mwisho, lakini wakati wowote tutafanya jambo ambalo tutalitangaza kuhusu mustakabali wa kocha,” alisema bosi mmoja wa juu ndani ya Fountain Gate.

Awali, akizungumza na Mwanaspoti, Mkurugenzi Mtendaji wa Fountain Gate, Tabitha Kidawawa alisema kocha huyo ameshaondoka kwa sababu ya matatizo ya kiafya.

“Alikuwa na changamoto ya kiafya, ndio maana tukaona ni vyema apate muda mzuri wa kupumzika na kujiuguza.

“Ligi inakwenda mwishoni kwa hiyo watamalizia makocha wengine, ili yeye akapumzike na kupata muda mzuri wa kujitibu,” alisema kiongozi huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *