Waandikishaji watakiwa kushirikisha mawakala wa vyama vya siasa

Njombe. Waandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura katika Jimbo la Njombe Mjini wametakiwa kushirikiana kikamilifu na Mawakala wa Vyama vya Siasa kwa kuwapokea kwenye vituo vyao, kwani mawakala hao wanatambulika kisheria na wana haki ya kuwepo katika maeneo ya uandikishaji.

Kauli hiyo imetolewa leo, Aprili 29, 2025 na Ofisa Mwandikishaji wa Jimbo la Njombe Mjini, Samson Meda, wakati wa mafunzo kwa waandikishaji wasaidizi na waendesha vifaa vya kielektroniki vya biometria (BVR), kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura  awamu ya pili, yaliyofanyika katika Halmashauri ya Mji wa Njombe.

Amesema kuwa miongoni mwa wadau wakuu wa mchakato wa uchaguzi ni vyama vya siasa na hivyo, ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaoboresha taarifa zao katika vituo husika wanazingatia maeneo sahihi ya usajili, ni lazima kwa mujibu wa sheria  vyama hivyo viwe na mawakala waliothibitishwa kisheria kutekeleza majukumu yao ndani ya ardhi ya Tanzania.

“Kwa hiyo, mawakala hao wana haki ya kuwepo kwenye vituo, ingawa hawana mamlaka ya kuingilia moja kwa moja mchakato wa uboreshaji. Wao ni waangalizi (observers) wanaoshuhudia na kuhakikisha kuwa anayeboresha taarifa zake ni yule anayestahili kufanya hivyo,” amesema Meda.

Meda amesema waandikishaji hao wa daftari la kudumu la wapiga kura wamekula viapo vya aina mbili cha kwanza kujitoa katika chama cha siasa ili kuleta usawa na kingine kiapo cha kutunza siri.

Amesema katika utekelezaji wa majukumu ya uandikishaji wapiga kura kwenye daftari la kudumu yapo mambo mengi ambayo watekelezaji wanatakiwa kuwa watunza siri kuhusu taarifa mbalimbali za wananchi.

Meda amesema kuwa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili litaanza rasmi Mei 1, 2025, na kumalizika Mei 7, 2025, ambapo jumla ya vituo 45 vitahusika katika uandikishaji ndani ya Jimbo la Njombe Mjini.

Mwandishi Msaidizi katika zoezi hilo, Happiness Mwaituka amesema kuwa wana matumaini ya kutekeleza jukumu hilo kwa weledi wa hali ya juu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha siri zote za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi zinahifadhiwa kwa uaminifu mkubwa.

“Changamoto tuliyokutana nayo awamu ya kwanza watu wengi walikuwa hawana elimu ya kutosha, lakini wengine walikuwa wanachanganya zoezi hili na lile la vitambulisho vya Nida,” amesema Mwaituka.

Naye Christian Nyengela amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuwaandikisha wapigakura ambao hawakupata nafasi ya kujiandikisha katika zoezi lililopita na hata wale ambao waliiandikisha, lakini taarifa zao zimekosewa.

“Tunaamini mafunzo hayo yatatusaidia sisi kuwaongeza wapiga kura ili wapate haki yao ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba,” amesema Nyengela.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *