Askofu Nkwande ataja kiini ongezeko la uhalifu, maadili mabovu kwa vijana

Mbeya. Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza, Renatus Nkwande amesema ukosefu wa ajira kwa vijana ni moja ya sababu za kuongezeka kwa matukio ya uhalifu na mmomonyoko wa maadili nchini.

Amesema vijana wengi wanakabiliwa na maumivu ya maisha na mahangaiko ya kila siku, hivyo kuwa rahisi kuwasukuma kujiingiza katika vitendo viovu ili kupata namna ya kujikimu.

Nkwande amesema hayo leo Jumanne Aprili 29, 2025 mkoani Mbeya, wakati wa Misa ya Jubilei Kuu ya Miaka 25 ya Ukristo na uzinduzi wa miundombinu mipya ya majengo na vyumba vya madarasa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki (CUoM). Majengo hayo yana uwezo wa kuchukua watu 5,000.

Amesema kutokana na tatizo hilo, umefika wakati  mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania kuungana kutembea umbali mrefu wakibeba msalaba kama ishara ya kufanya Hija ya kuwaombea.

“Kuna kauli inasemwa vijana wajiajiri watapata wapi ujasiri wa kujiajiri wakati wapo ambao, watoto wao wanapewa ajira, huku wengine wakipata mahangaiko na kujikuta wamekata tamaa hivyo kujiingiza kwenye uhalifu na mmonyoko wa maadili ,” amesema.

Amesema kwa miaka ya nyuma wao walikuwa wakiajiriwa na wao kujiajiri, jambo ambalo kwa sasa ni ngumu na badala yake vijana wameishia kupata maumivu na kukata tamaa wakijiona hawana umuhimu wa kuwepo.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza ,Renatus Nkwande akishika jiwe la msingi kama kuashiria uzinduzi wa miundombinu kumbi za mihadhara na vyumba vya madarasa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mbeya (CUoM). Picha na Hawa Mathias

“Vijana mnapaswa kukimbilia kwenye nguvu ya msalaba kwani ndio suluhisho la kuleta tumaini la kuwaondoa kwenye fikra za njia za mkato, lakini nasi tutaendelea kuwaombea kwa kubeba msalaba na kufanya Hija,” amesema.

Askofu Nkwande amesema wataendelea kubeba msalaba wa kuyombea makundi ya vijana nchini  ili kupata suluhisho la kudumu na kuwarejesha kwenye tumaini.

Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Ronald Haule, amesema maadhimisho ya Jubilei hiyo yamehudhuriwa na maaskofu kutoka majimbo mbalimbali nchini, pamoja na mapadri, watawa, wanachuo na waumini wa Kanisa Katoliki.

Ameeleza kuwa ujenzi wa miundombinu mipya ya chuo hicho umehusisha kumbi nane zenye uwezo wa kuchukua zaidi ya watu 5,000 wakiwemo wanafunzi, walimu na watumishi, pamoja na chumba cha Tehama kwa ajili ya kukuza ubora wa mafunzo na matumizi ya teknolojia chuoni hapo.

Ameeleza kuwa miundombinu hiyo imehusisha vyumba sita vya mihadhara, ambapo viwili kati yake vimetengwa mahususi kwa ajili ya walimu na wanafunzi, vyote vikiwa na uwezo wa kuchukua hadi watu 400 kwa wakati mmoja.

Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa CUoM, Dk Mutahyoba Baisi amesema mradi wa ujenzi huo umekamilika ndani ya kipindi cha miezi 10, na mara utakapokamilika utafungwa mitambo ya kisasa ya mifumo ya Tehama ili kuwawezesha walimu kuachana na matumizi ya chaki na kutumia mbinu za kisasa kufundishia.

“Chuo chetu kinakwenda kuboresha matumizi ya teknolojia za kisasa katika ufundishaji maono yetu ni kuboresha zaidi ili kupanua uwezo wa kuongeza programu nyingine,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *