
Watu tisa wameuawa katika mapigano ya kidini katika kitongoji cha Druze cha Jaramana karibu na Damascus, shirika lisilo la kiserikali limesema siku ya Jumanne, huku mamlaka zikiapa kuwashtaki waliohusika katika mapigano hayo.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Ghasia hizo zinakuja mwezi mmoja baada ya mauaji ya watu kutoka jamii ya walio wachache ya Alawite, ambapo anatoka rais aliyeondolewa madarakani Bashar Al Assad, ambaye alipinduliwa na muungano wa Kiislamu ulionyakua madaraka mwezi Desemba.
Kulingana na Shirika la Haki za Kibinadamu la Syria (SOHR), “vikosi vya usalama vilianzisha mashambulizi” dhidi ya Jaramana baada ya ujumbe wa sauti unaohusishwa na mtu mmoja kutoka kabla la Druze kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii na kuonekana kuwa ni kufuru dhidi ya Uislamu.
AFP haikuweza kuthibitisha uhalisi wa ujumbe huu.
Shirika la SOHR lenye makao yake nchini Uingereza, ambalo lina mtandao mkubwa wa vyanzo nchini Syria, limesema wapiganaji sita wa eneo hilo kutoka Jaramana na “washambuliaji” watatu waliuawa.
Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Ndani ilisema makabiliano hayo yalitokea kati ya “makundi yenye silaha” kabla ya vikosi vya usalama kuingilia kati, na kupeleka “kuwalinda wakaazi.”
Wizara iliahidi “kuwafuatilia” watu wenye silaha waliohusika katika mapigano haya, ambayo yalisababisha “vifo na majeruhi,” idadi yao ambayo haikutajwa.
– “Tunaogopa” –
Wakaazi kadhaa wa Jaramana waliowasiliana kwa simu na shirika la habari la AFP wamesema walisikia milio mingi ya risasi usiku.
“Hatujui kinachoendelea, tunaogopa Jaramana itakuwa ukumbi wa vita,” amesema Riham Waqaf, mfanyakazi wa shirika moja lisilo la kiserikali aliyejificha nyumbani na mumewe na watoto.
“Tulitakiwa kumpeleka mama yangu hospitali kwa matibabu, lakini hatukuweza kutoka,” mwanamke huyo wa miaka 33 ameongeza.
Wapiganaji wa eneo hilo walisambaa mitaani na kwenye lango la kuingilia mjini, wakiwataka wakaazi kusalia majumbani, mmoja wa watu wenye silaha, Jamal, ambaye hakutaja jina lake la mwisho, ameliambia shirika la habari la AFP.
Tangu muungano wa Kiislamu unaoongozwa na Ahmad al-Sharaa, ambaye alitangazwa kuwa rais wa mpito, kuchukua madaraka, jumuiya ya kimataifa imekuwa ikiongeza wito wake wa kuwalinda walio wachache.