Mlipuko mbaya nchini Iran: Moto unaendelea katika bandari kubwa zaidi ya nchi

Wazima moto wameendelea kujaribu siku ya Jumatatu, Aprili 28, kuzima moto mkubwa ambao umeteketeza bandari kubwa zaidi ya Iran kwa siku ya tatu mfululizo. Mlipuko wa Jumamosi ulisababisha vifo vya watu 40 na wengine zaidi ya 1,000 kujeruhiwa.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Moshi mnene mweusi unaendelea kupanda juu ya makontena yaliyorundikwa kwenye bandari ya Shahid Rajai, kulingana na picha za televisheni ya taifa ya Iran zilizorushwa hewani moja kwa moja siku ya Jumatatu asubuhi. Baada ya moto kudhibitiwa, “tutaingia katika hatua ya kusafisha eneo la tukio na kutathmini uharibifu,” serikali imesema.

Mlipuko huo, uliosikika umbali wa kilomita kadhaa, ulitokea Jumamosi mwendo wa saa sita mchana saa za Iran (4:30 saa za Ufaransa) kwenye kivuko kwenye bandari ya Shahid Rajai, ambapo 85% ya bidhaa za Iran hupitia. Bandari hii ya kimkakati iko karibu na mji mkubwa wa pwani wa Bandar Abbas, kusini mwa nchi, kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz, ambapo sehemu ya tano ya uzalishaji wa mafuta duniani hupitia, kilomita elfu kusini mwa Tehran.

Ali Khamenei anataka uchunguzi ufanyike

Chanzo cha mlipuko huo hakijabainika mara moja, lakini mamlaka ya forodha katika bandari hiyo imesema huenda ulitokana na moto uliozuka katika vifaa hatari na kituo cha kuhifadhi kemikali. 

Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameagiza uchunguzi ufanyike kuhusu tukio hilo ili kubaini iwapo mkasa huo ulisababishwa na “uzembe” au “makusudi.” Rais Massoud Pezeshkian alitembelea hospitali katika mji wa karibu wa Bandar Abbas siku ya Jumapili kuwatembelea majeruhi. Wizara ya Afya imetoa wito kwa wakazi takriban 650,000 kukaa nyumbani “hadi ilani zaidi.” Ombi la kuchangia damu limezinduliwa kwa waliojeruhiwa.

Kauli za uwongo

Kulingana na ripoti zingine za vyombo vya habari, bidhaa hatari sana zilihifadhiwa katika sehemu hii ya bandari na kauli za uwongo kuhusu asili ya bidhaa hizi, zikitangaza kuwa sio hatari. Kwa mujibu wa kanuni za bandari, vifaa hatari lazima vihifadhiwe katika eneo maalum la bandari. Bado hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu kampuni iliyoagiza bidhaa hizi.

Lakini msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Iran amekanusha ripoti katika baadhi ya vyombo vya habari vya kigeni kwamba milipuko hiyo ilisababishwa na kemikali zilizoagizwa kutoka nje zinazotumiwa kutengeneza mafuta ya makombora ya balistiki, kwa mujibu wa mwandishi wetu mjini Tehran, Siavosh Ghazi.

Kwa ombi la Iran, Urusi ilituma ndege tatu za kurusha maji ambazo zilifika Bandar Abbas kusaidia waokoaji wa Iran kuzima moto huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *