Beki wa kati wa Real Madrid, Antonio Rudiger huenda akakumbana na adhabu kali kutokana na kitendo cha utovu wa nidhamu alichoonyesha jana Aprili 26, 2025 kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Mfalme dhidi ya Barcelona.
Katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa Barcelona kuibuka bingwa baada ya kupata ushindi wa mabao 3-2 ilishuhudiwa refa wa mchezo huo Ricardo De Burgos Bengoetxea akionyesha kadi tatu nyekundu kwa wachezaji wa Real Madrid ambao ni Rudiger, Lucas Vazquez na Jude Bellingham.
Rudiger ambaye alikuwa benchi baada ya kufanyiwa mabadiliko akimpisha Endrick alionekana kutoridhika na maamuzi ya mwamuzi baada ya beki wa Barcelona, Eric Garcia kuonekana kumchezea vibaya Mbappé wakati mwamuzi akionyesha kwamba haikuwa faulo.

Kitendo hicho kilipelekea benchi la ufundi la Madrid kuamka wakimlaumu refa huku Rudiger akionekana kumrushia mwamuzi huyo kipande cha barafu alichokuwa ameshika mkononi na kusababisha kuonyeshwa kadi nyekundu.
Kwa mujibu wa jarida la AS Sport la Hispania, huenda Rudger akakabiliwa na adhabu kali ikiwemo kufungiwa kucheza michezo kuanzia minne hadi 12 ikiwa ni kwa mujibu wa sheria zinazomlinda mwamuzi dhidi ya vitendo visivyo vya kiungwana.

Hata hivyo, mchezaji huyo ameomba radhi kupitia mitandao ya kijamii kwa kile alichokifanya katika mchezo wa jana:
“Hakika sina sababu yoyote ya kunifanya nisiombe msamaha kwa tabia yangu usiku uliopita. Samahani sana kwa hilo. Tulicheza mchezo mzuri sana kuanzia kipindi cha pili.
Baada ya dakika 111 sikuweza tena kusaidia timu yangu na kabla ya filimbi ya mwisho nilifanya kosa. Samahani tena kwa mwamuzi na kwa kila mtu niliyemkwaza usiku uliopita,”ameandika Rudiger.

Mbali na Rudiger wachezaji wengine ni Lucas Vazquez na Jude Bellingham ambao pia walionyeshwa kadi nyekundu wakidaiwa kumtupia maneno yasiyo ya kiungwana refa wa mchezo huku Bellingham akionyeshwa kadi baada ya mchezo kumalizika.

Madrid imepoteza mchezo wa tatu mfululizo dhidi ya Barcelona msimu huu. Licha ya kuwa na mastaa wengi wamejikuta katika wakati mgumu kwani hadi sasa timu hiyo imeondolewa kwenye mashindano yote iliyokuwa ikishiriki.
Madrid imesalia kwenye Ligi Kuu Hispania ‘La liga’ inakoshika nafasi ya pili ikiwa nyuma kwa pointi nne dhidi ya Barcelona inayoongoza Ligi hiyo ikiwa napointi 76.