Dar es Salaam. Katika kukabiliana na changamoto ya vijana kujitenga na masuala ya siasa na uongozi, umezinduliwa mpango wa kukuza uongozi kwa vijana kwa lengo la kulea kizazi kipya cha viongozi wenye mabadiliko kuanzia ngazi ya jamii.
Lengo kuu la mpango huo uliozinduliwa jana, Aprili 25, 2025, ni kukabiliana na changamoto zinazozidi kuongezeka kama vile ushabiki wa kisiasa usio na tija, uwajibikaji duni, na kupungua kwa ubunifu katika uongozi wa taasisi za umma na binafsi.
Mpango huu unaojulikana kama ‘Tanzania NextGen Leaders Fellowship’ (TNLF) unatekelezwa na Taasisi ya Uongozi wa Afrika kwa Maendeleo Yenye Mchango (African Leadership Initiative for Impact – ALII), kwa kushirikiana na HakiElimu.
Kundi la kwanza litahusisha vijana 350 wa Kitanzania wenye umri kati ya miaka 17 hadi 19, ambao watapata mafunzo ya kina ya uongozi na ushauri kuanzia Septemba.
Mkurugenzi Mtendaji wa ALII, Joseph Malekela amesema programu hiyo imetengenezwa mahususi kuwawezesha vijana walioko katika hatua za mwisho za elimu ya sekondari kwa kuwapa ujuzi wa vitendo katika uongozi, fikra pevu na maamuzi yenye maadili.

Amesema lengo kuu la programu hiyo ni kuwaandaa vijana hao kwa nafasi za uongozi zenye uwajibikaji, kitaifa na kimataifa, kama sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kubadilisha taswira ya uongozi nchini Tanzania.
“Tunapoteza vipaji vingi vya vijana kwa mfumo unaotukuza kufuata mkumbo na kujipendekeza. Ushirika huu ni njia mbadala, tunajenga viongozi waadilifu na wenye fikra huru kuanzia ngazi ya jamii,” amesema Malekela.
Ameeleza kuwa programu hiyo inalenga kuwafundisha vijana kundi jipya la viongozi watakaoendelea kufuatiliwa katika safari yao ya elimu ya juu na maisha ya kitaaluma hadi wawe watu wa kuigwa katika jamii zao.
“Hatufundishi halafu tunawaacha. Tutakuwa tukiwafuatilia. Tunataka kuwaona wakichukua nafasi zenye maana katika jamii kutoka vituo vya ubunifu hadi meza za kutunga sera,” ameongeza Malekela.
Mafunzo hayo yatakayofanyika kuanzia Septemba 13 hadi 26, mwaka huu jijini Dar es Salaam, yataendeshwa kwa awamu, ili kuwapa washiriki nafasi ya kushiriki shughuli nyingine kama JKT au maandalizi ya chuo.
Kila mkoa kati ya mikoa 34 ya Tanzania utawakilishwa na hadi wanafunzi 10 kutoka shule tofauti, ambapo kila shule itaruhusiwa kumpendekeza mwanafunzi mmoja.
Ili kustahiki, mwanafunzi lazima awe Mtanzania mwenye umri wa miaka 17 hadi 19 (aliyezaliwa kati ya mwaka 2006 hadi 2008), awe amemaliza kidato cha sita mwaka huu, anatambulika kama kiongozi bora wa wanafunzi katika shule yake, na awe na uwezo mzuri wa kuwasiliana kwa Kiswahili na Kiingereza.
“Hatuangalii tu ufaulu darasani. Tunachunguza maadili yao, jinsi wanavyoongoza wenzao, kutatua matatizo, na uwezo wao wa kuwasilisha mawazo, hivyo walimu wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uteuzi kwa kuwa wana nafasi kubwa ya kugundua viongozi wenye uwezo wakiwa bado wachanga kabla hawajaingia kwenye mifumo inayoweza kupotosha maadili yao.”
Mchambuzi wa sera na Meneja wa Mpango kutoka HakiElimu, Makumba Mwemezi amesema programu hiyo ni majibu ya moja kwa moja kwa hali inayozorota ya uongozi nchini.
Ameeleza kuwa mara nyingi vijana wanakumbwa na utegemezi wa kisiasa na hawapati nafasi ya kujifunza mifano ya uongozi wa uhuru na wenye maadili.
“Kila mwaka ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu (CAG) zinaonyesha mapungufu makubwa ya kiuongozi. Wakati huohuo, vijana wanajikuta wameingia kwenye mifumo hiyo.
“Ushirika huu ni suluhisho la muda mrefu. Tunapanda mbegu za uadilifu, maono na uwajibikaji kwa viongozi wa kesho kabla hawajapotea,” amesema Mwemezi.
Ameongeza kuwa programu hiyo pia inalenga kupunguza pengo la kijinsia, hasa katika upatikanaji wa nafasi za uongozi.
Kwa upande wake, Ofisa wa Uhusiano na Uchechemuzi wa HakiElimu, Benedicta Mrema amesema TNLF itawawezesha wasichana kwa ujuzi wa uongozi, ushauri na mitandao ya kijamii ili waweze kupata nafasi katika ajira rasmi na uongozi.
“Hatubadilishi tu tofauti za kijinsia, tunafafanua upya namna uongozi unavyopaswa kuwa hapa Tanzania. Wasichana watafundishwa sambamba na wavulana, kwa usawa wa fursa za kuongozwa, masoko ya ajira na nafasi za kuleta mabadiliko,” amesema Benedicta.