Papa Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, amezikwa katika Kanisa la Santa Maria Maggiore Basilica jijini Roma nchini Italia, baada ya maelfu ya waombolezaji wakiwemo marais mbalimbali akiwemo Donald Trump wa Marekani na Emmanuel Macron wa Ufaransa kuhudhuria ibada ya mazishi katika viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Mazishi ya Papa Francis, aliyefariki dunia Aprili 21 akiwa na umri wa miaka 88, imehudhuriwa na maelfu ya waombolezaji, wanaokadiriwa kuwa laki nne, katika ibada iliyoongozwa na Kadinali Giovanni Battista Re, ambaye katika mahubiri yake, alimwelezea Papa Francis kama kiongozi aliyekuwa na moyo wa upendo, kwa kila mmoja.
Baada ya kukamilika kwa ibada hiyo, mwili wa Papa Francis uliowekwa kwenye jeneza la mbao, ulisafirishwa kwenda kuzikwa katika Kanisa la Santa Maria Maggiore Basilica jijini Roma alikochagua kuzikwa, kinyume na Vatican ambako Mapapa huzikwa.

Maelfu ya watu walijitokeza kushuhudia masafara uliobeba mwili wake, huku wakimpungia.
Mazishi ya Papa Francis, aliyeongoza kwa miaka 12, kunafungua ukurasa mpya kwa Makadinali wa Kanisa Katoliki, wanaotarajiwa kumchagua kiongozi wao mpya mwezi Mei, kuwaongoza waumini wa Kanisa Katoliki wapatao Bilioni 1.4 kote duniani.