Hatuwezi kumaliza Malaria bila kuwa na msukumo thabiti

Msukumo unahitajika kwani tuna kila sababu ya kuhakikisha tunatokomeza malaria

Uimara wa uongozi haup­imwi katika nyakati njema, bali katika nyakati ambazo unatakiwa kukabiliana na changamoto zinazoweza kufifisha mafanikio yaliy­opatikana kutokana na kazi kubwa iliyofanyika. Mojawapo ya changamoto kubwa inayoikabili bara la Afrika ni afya na ustawi wa watu wake. Na ni dhahiri kuwa, malaria ni moja ya kiini cha changamoto hizo.

Inaelezwa kuwa, malaria bado inasababisha vifo vya zaidi ya watu laki tano bara­ni Afrika kila mwaka, huku wengi kati ya hao wakiwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Rais wa Jamhuri ya Botswana, Wakili Duma Gideon Boko akizungumza wakati akikabidhiwa uenyekiti wa ALMA katika mkutano wa AU uliofanyika Februari, 2025.

Zaidi ya asilimia 95 ya vifo hivyo hutokea kutokana na jamii kukosa mbinu za kujikinga na ugonjwa huo, kupima afya mara kwa mara na kukosekana kwa mati­babu sahihi. Hii inasababi­sha ugumu katika kufikia lengo la Umoja wa Afrika la kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030, huku visa vya malaria vikiongezeka.

Changamoto hii inasa­babishwa pia na kupunguz­wa kwa ufadhili kutoka kwa wafadhili wakubwa, ikiwa ni pamoja na kupunguzwa kwa hivi karibuni kwa mis­aada ya kigeni ya Marekani ambayo kihistoria imekuwa msaidizi mkuu wa kutoko­meza malaria kupitia Mpan­go wa Rais wa Malaria (PMI) na Mfuko wa Dunia (Global Fund). Kusitishwa kwa ufadhili wa Shirika la Mis­aada la Marekani (USAID) kumerudisha nyuma juhudi za kupambana na malaria zilizosababishwa na kupun­gua kwa bidhaa muhimu za malaria katika nchi nyingi hasa za Afrika.

Wataalamu wanakadiria kuwa, kama fedha za misaa­da zitaendelea kukosekana, Afrika itashuhudia visa mil­ioni 112 na vifo 280,000 zaidi vya malaria kuanzia mwaka 2027 hadi 2029. Aidha, ufad­hili mdogo wa Global Fund utasababisha visa kufikia milioni 137 na vifo 337,000 vya malaria na hivyo kurudi­sha nyuma mafanikio yaliy­opatikana katika miongo iliyopita. Kwa mwenendo huu, hatutapoteza tu ngu­vu ya mapambano dhidi ya malaria bali pia tutarudisha nyuma maendeleo yaliyo­fikiwa katika karne iliyopita.

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Mrisho Kikwete akikata utepe kuzindua ofisi za ALMA jijini Dar es Salaam mwaka 2009.

Na huo ndiyo ukweli kuhu­su malaria, bila marekebi­sho ya haraka, changamoto hii itaongezeka na hivyo kuhatarisha vifo vya watoto zaidi na vikwazo kwa afya, uchumi na utulivu wa kikan­da. Hatutakiwi kulichukulia hili kama jambo la kawaida bali ikiwa tuna nia ya dhati ya kulinda kizazi kijacho, mapambano dhidi ya malar­ia lazima yaendelee bila kuathiriwa na kitu chochote. Tanzania na Botswana zimeonyesha jinsi uongozi unavyopaswa kuwa katika juhudi za kudhibiti malaria.

Tanzania imejikita katika kupanua juhudi hizi katika ngazi ya jamii, kuunganisha huduma za malaria katika huduma za afya ya msingi na kuhakikisha upatikanaji wa matibabu kwa wakati. Botswana, ambayo sasa inakaribia kutokomeza ugonjwa huo, ina mifumo dhabiti ya ufuatiliaji, mwi­tikio wa haraka wa mlipuko na udhibiti wa vimelea vya malaria unaolenga katika maeneo yenye hatari kubwa. Nchi zote mbili zinaendelea kuonyesha kwamba kuto­kana na uwepo wa uongozi thabiti na mikakati imara, maendeleo yanawezekana.

Changamoto zilizopo kati­ka kukabiliana na malaria Afrika

Katika bara zima la Afrika, mapambano dhidi ya malar­ia yanakumbana na changa­moto kadhaa zinazotishia kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana kwa miaka mingi.

Mabadiliko ya tabianchi yanaongeza hatari ya malar­ia. Mabadiliko ya hali ya hewa na matukio mengine kama hayo yanasababisha kueneza maambukizi katika maeneo mengine na kure­fusha misimu ya malaria. Wakati huohuo, upungufu wa fedha unatishia maende­leo ya mapambano haya. Afrika inahitaji nyongeza ya Dola bilioni 5.2 kila mwaka kutekeleza kikamilifu mika­kati ya kitaifa ya kupambana na malaria.

Watoa huduma za afya wa kijamii wakionyesha matumizi ya vyandarua vilivyowekwa dawa nchini Nigeria. Picha na US PMI

Licha ya kutengwa kwa bajeti na misaada kutoka kwa washirika wa maende­leo, upungufu wa fedha bado unaongezeka. Kupun­guzwa kwa misaada ya kimaendeleo kunakwami­sha programu za malaria, kuchelewesha miradi na kusababisha uhaba wa dawa na vifaa kinga na tiba.

Pia tunakabiliwa na chan­gamoto ya ukinzani wa kibaolojia. Viuatilifu vinash­indwa tena kuwaathiri mbu na vimelea vya malaria vinaonyesha dalili za kusta­himili dawa. Ukinzani huu wa kibaologia unadhoofisha ufanisi wa dawa na kinga hivyo kuwepo kwa uhitaji wa haraka wa jitihajada mpya.

Migogoro ya kibinadamu inayoendelea ni changamo­to nyingine katika utoaji wa huduma za malaria. Katika mazingira haya magumu, mwendelezo wa huduma unakuwa mgumu na hatari ya milipuko ya malaria ina­ongezeka zaidi.

Kuendelea kupambana na changamoto bila kuchoka

Licha ya kupitia chan­gamoto hizi, maende­leo katika kupambana na malaria yanawezekana. Nchi zinaendelea kuongeza zana za udhibiti wa malaria ikiwa ni pamoja na vyanda­rua vyenye dawa na kunyu­nyizia dawa ukoko ndani ya nyumba. Vyandarua hivi pia vinasaidia kupambana na ukinzani wa viuatilifu katika maeneo yenye maam­bukizi makubwa na hivyo kusababisha kupungua kwa malaria.

Tumeshuhudia kwamba dawa za kuzuia malaria na chanjo vinaleta matumaini mapya. Matumizi ya dawa za kemikali za kuzuia malar­ia yanaendelea kuongezeka jambo linalosaidia kuwalin­da watoto dhidi ya maam­bukizi.

Mtoa huduma za afya wa kijamii kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara akimfanyia vipimo vya malaria mwananchi. Picha na Abbie Trayler-Smith – Malaria No More UK

 

Uchunguzi wa mapema na matibabu yanaende­lea kuokoa maisha. Watoa huduma za afya wa kijamii mara nyingi ndiyo wameku­wa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma. Hivyo kuongeza nguvu kazi hii na kuboresha minyororo ya usambazaji wa bidhaa tiba bado ni muhimu. Juhudi za kuwalinda wale ambao wanakabiliwa na hatari zai­di kama vile wakinamama wajawazito zinaimarika huku utumiaji wa dawa kinga wakati wa ujauzito (IPTp) husaidia kuwalinda mama na mtoto.

Juhudi hizi zinafanya kazi, lakini ni lazima ziboreshwe na kuungwa mkono na vion­gozi, ushirikishwaji wa jamii na uwekezaji thabiti.

Msukumo mkubwa unahita­jika ili kutokomeza malaria

Kutokomeza malaria hakutafanikiwa pasi na kuwepo juhudi za ziada. Ina­hitaji msukumo thabiti kati­ka nyanja zote ili kuhakiki­sha matokeo yanapatikana kwa haraka na kwa viwango.

Lazima tuhakikishe upa­tikanaji endelevu wa kinga, utambuzi na matibabu. Vyandarua vilivyowekwa dawa, vipimo vya haraka na dawa bora huokoa mai­sha. Ni lazima kuwepo kwa mifumo bora ya utendaji kazi, kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wake na kuhakik­isha uwajibikaji katika ngazi zote.

Maendeleo yanatege­mea uratibu sahihi pamoja na maamuzi yanayoto­kana na data. Nchi zinat­akiwa kutumia data sahihi katika utekelezaji wa afua za malaria. Hii inahitaji uwekezaji katika mifumo ya taarifa na uongozi wenye maono.

Mbinu moja haitafanya kazi. Ndiyo maana ush­irikiano wa kimataifa kati­ka utekelezaji wa afua za malaria ni muhimu sana. Wilaya zenye maambukizi tofauti ya malaria zinahitaji masuluhisho tofauti, na ni lazima tubadilike ipasavyo.

Mtoa huduma za afya wa kijamii kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara akimfanyia vipimo vya malaria mwananchi. Picha na Abbie Trayler-Smith – Malaria No More UK

 

Uhamasishaji wa rasili­mali za ndani ni msingi wa maendeleo endelevu. Mafanikio ya muda mrefu yanategemea nchi kuweka kipaumbele kwa ugonjwa wa malaria ndani ya bajeti zake na mikakati ya ufadhili pamoja na kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi.

Tunahitaji juhudi za jamii nzima. Serikali haiwezi kufanya hivyo peke yake. Mafanikio yanategemea kushirikisha kila sekta, iwe ya afya, fedha, elimu, kilimo, mazingira, na kila sehemu ya jamii, wakiwemo wabunge, jumuiya za kiraia, vijana, sekta binafsi na viongozi wa imani. Kila mtu ana jukumu lake. Kutokomeza malaria kunaanza na sisi sote!

Hakuna mkakati utakao­fanikiwa bila kuwa na watu wanaofanya kazi kwa bidii. Watoa huduma za afya wa kijamii, ambao mara nyingi ndiyo sehemu ya kwanza ya utoaji wa huduma, ni lazima wapatiwe mafunzo, wawezeshwe ili wawe na vifaa bora na waungwe mko­no ili kuendeleza kazi yao ya kuokoa maisha.

Ni lazima tujumuishe malaria katika utoaji wa huduma za afya kwa map­ana zaidi, kuingiza malaria katika huduma za wajawa­zito, programu za afya shu­leni na huduma za afya za jamii ili kufanya afua ziweze kupatikana kwa ufanisi zaidi. Zana pekee haziwezi kumaliza malaria isipokuwa zikiungwa mkono na dhami­ra ya kisiasa na uwajibikaji.

Jukwaa la Afrika la uongozi na uwajibikaji

Muungano wa Viongozi wa Afrika Dhidi ya Malaria (The African Leaders Malar­ia Alliance, ALMA) uliundwa ili kukidhi mahitaji haya. ALMA ilianzishwa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete ikiwa na maono ya kuwaleta pamoja wakuu wa nchi na Serikali ili kugeuza dhamira za kisiasa kuwa hatua ende­levu, kupambana na malaria kuwa kipaumbele chao na kuunganisha bara zima kati­ka malengo ya pamoja.

Mtoa huduma za afya wa kijamii kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara akifanyia vipimo vya malaria maabara. Picha na Abbie Trayler-Smith – Malaria No More UK

Tanzania ni mwenyeji wa makao makuu ya ALMA, kama sehemu ya uongozi na dhamira ya kudumu ya kuendeleza ushirikiano wa afya na kikanda katika bara la Afrika.

Kwa miaka mingi, uon­gozi wa ALMA umekuwa ukizunguka katika nchi zote, ikionyesha wajibu wa Afrika nzima. Leo, kanda ya SADC inaongoza, huku Rais Wakili Duma Gideon Boko wa Botswana akiwa mwe­nyekiti wake.

Jukumu la ALMA katika kuongeza kasi ya kupam­bana na malaria

Kama jukwaa linaloon­gozwa na wakuu wa nchi za Afrika, ALMA huzipa nchi zana zinazohitaji ili kupata matokeo. Zana hizi husaid­ia nchi kufuatilia maende­leo, kutambua vikwazo na kuchukua hatua haraka ili kuleta matokeo. Wizara za Afya hutumia zana hizi katika kufanya maamuzi na kuelekeza matumizi ya rasil­imali kwa ufanisi zaidi. Zana hizi pia huwapa wananchi sautikwa kutoa maoni kuhu­su huduma za afya ili kui­marisha uwajibikaji kuanzia ngazi za chini.

ALMA inakuza mtazamo wa jamii nzima, kuwashirik­isha wabunge, mashirika ya kiraia na vijana katika juhudi za kitaifa. Kampeni ya ‘Zero Malaria Starts with Me’ imesaidia kuongeza ufahamu wa malaria katika jamii. ALMA pia imefadhili mifuko 9 ya kupambana na malaria, ambayo imekusan­ya zaidi ya dola za Marekani milioni 125 na kuzindua Kundi la Vijana katika nchi 16 ili kuwawezesha viongozi vijana.

ALMA inaunga mkono wazalishaji wa ndani, mageuzi ya udhibiti na upatanishi wa kikanda ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje. Maamuzi haya yatasaidiakuimarisha uwezo wa Afrika wa kuk­abiliana na matishio ya afya katika siku zijazo.

Upatikanaji wa ubunifu na uzalishaji wa ndani

Afrika haijapungukiwa na ubunifu. Lakini mara nyingi, kuna pengo kati ya kile kili­chopo sehemu zingine za dunia na kile kinachopa­tikana ndani ya bara la Afrika. Kuziba pengo hilo kunamaanisha kuharakisha ufikiaji wa zana mpya na kuwekeza katika uzalishaji wa ndani katika bara zima.

Mkakati wa ubunifu kati­ka kupambana na malaria una nguvu zaidi kuliko hapo awali. Zana mpya ni pamoja na vyandarua vyenye dawa, huduma bora za vipimo, chanjo na dawa zinazofaa zaidi. Pia kuna masuala ya teknolojia kama vile dawa za kufukiza (spatial repellents), kingamwili za monokloni n.k.

Lakini ubunifu ni muhimu tu ikiwa utawafikia watu wanaouhitaji. Hata hivyo, nchi nyingi zinakabiliwa na changamoto za muda mrefu kama sheria ngumu za usa­jili kwa ajili ya ununuzi na michakato ya upatikanaji wa vyeti vya ithibati vya bidhaa tiba. Vyote hivi huchelewe­sha ufikiaji wa huduma hizo.

Mtaalamu wa afya akipulizia dawa ukoko kwenye nyumba kwa ajili ya kuua mbu waenezao malaria. Picha na Brant Stewart RTI

Chini ya asilimia 2 ya bid­haa za malaria zinatengene­zwa barani Afrika. Kuon­geza uzalishaji wa ndani si hiari tena bali ni muhimu. Tanzania tayari inaonyesha kwamba hili linawezekana. Kupitia uwekezaji wa ndani kama ule wa kiwanda cha A-to-Z, unazalisha vyan­darua vyenye dawa, hivyo basi kupunguza gharama na kujenga uwezo wa nchi na bara la Afrika.

Kinachohitajika kwa sasa ni kasi na ushirikiano mkub­wa ili kuoanisha michakato ya udhibiti. Mwitikio ende­levu wa malaria lazima uwe wa kujitegemea. Afrika laz­ima iondoke kutoka kuwa mlaji mkubwa zaidi duniani hadi kuwa mzalishaji mkub­wa.

Je, tutashinda au tutash­indwa?

Bado tunaweza kushinda pambano hili. Nchini Tanza­nia, maambukizi ya malaria yamepungua kutoka asil­imia 18.1 hadi 8.1 katika kip­indi cha muongo mmoja tu. Botswana inakaribia hali ya kutokuwa na malaria kabi­sa. Haya si mafanikio pekee, bali yanaonyesha kile kina­chowezekana kwa uongozi thabiti, na hatua endelevu.

Kuondoa malaria kutawezeakana tu kupitia kujitoa, uratibu thabiti na upatikanaji wa haraka wa zana mpya. Tunajua kina­chofanya kazi, sasa ni laz­ima tukifanye haraka, kwa ubora na kwa pamoja.

Hitimisho: Dhamira ya Afrika kuelekea msukumo thabiti

Kama Marais wa Tanzania na Botswana, tunasisitiza dhamira yetu ya pamoja ya kukomesha ugonjwa wa malaria, sio tu katika nchi zetu, bali Afrika nzima.

Hii sio safari ambayo Seri­kali zinaweza kutembea peke yake. Inahitaji ushiriki­ano wa pamoja kutoka kila sekta, ikijumuisha viongozi wa imani, vijana, wanasay­ansi, wahudumu wa afya na sekta binafsi. Ukweli ni kwamba Afrika haijawahi kujitosheleza katika juhudi za kupambana na malaria, lakini sasa uwezo tunao, mifumo tunayo na nia tunayo. Tunachohitaji ni msukumo thabiti ili kum­aliza kazi hii.

Msukumo huu huanza kwa kuziba pengo la ufad­hili. Ufadhili wa kimataifa ni muhimu na ni lazima tuwe na msaada wa kifed­ha kutoka Mfuko wa Dunia. Upatikanaji wa rasilimali za ndani ni muhimu ikiju­muisha mifuko ya kitaifa ya kutokomeza malaria. Majukwaa haya yanaweze­sha rasilimali za ndani na kuweka malaria kama kipa­umbele katika ajenda za kisiasa. Malaria lazima pia iunganishwe katika ufadhili wa afya, kuanzia huduma za msingi hadi juhudi za kuk­abiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Lazima pia tuhakikishe kunakuwa na ubunifu. Ni laz­ima nchi ziondoe urasimu, zipunguze gharama na kui­marisha mifumo ya udhibiti ili zana mpya ziwafikie wale wanaozihitaji zaidi.

Tanzania na Botswana ziko tayari kuongoza msu­kumo huo. Tumejitolea kuharakisha michakato, kuhamasisha washirika wetu na kuwa na uon­gozi unaoleta matokeo. Tunawaalika wengine Afri­ka na ulimwenguni, kuun­gana nasi. Hatua inayofuata katika mapambano dhidi ya malaria ni nzuri. Wacha hat­ua hii iwe ya vitendo, umoja na ushindi.

Imeandikwa na:

Rais wa Jamhuri ya Muun­gano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan

Rais wa Jamhuri ya Botswana, Wakili Duma Gideon Boko

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *