Ruto anahoji uhalali wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika hotuba ya Beijing

Rais wa Kenya William Ruto ambaye yuko ziarani Beijing, nchini China, ametilia shaka umuhimu wa muundo wa sasa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kushughulikia changamoto za leo za amani na usalama.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza katika Chuo Kikuu cha Peking mjini Beijing, rais William Ruto amesema uaminifu wa Baraza hilo unazidi kupungua.

“Baraza la Usalama, ambalo limekuwa kinara wa amani na diplomasia, sasa lina mwanachama mmoja wa kudumu anayevamia nchi moja, huku mjumbe mwingine akishiriki katika mzozo kinyume na maazimio ya Baraza,” Ruto amesema.

Amedai kuwa muundo wa sasa wa Baraza hilo ulikubalika tu katika matokeo ya kipekee ya Vita vya Pili vya dunia

“Hakuna hali nyingine, isipokuwa hali ya baada ya vita, ingeweza kufanya muundo wa sasa wa Umoja wa Mataifa na hasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo ni wanachama watano wa kudumu wenye mamlaka ya kibinafsi, muundo unaokubalika wa amani na usalama,” amesema.

Rais Ruto amesema wanachama hao wa kudumu wanapinga mabadiliko, licha ya kupungua kwa umuhimu wa Baraza hilo kimataifa.

“Hata hivyo leo, wanachama wa kudumu wanaishi katika kukataa na kupinga mageuzi, hata kama Baraza la Usalama linazidi kuwa halali na umuhimu wake unatiliwa shaka,” ameongeza.

Matamshi ya rais Ruto yanajiri huku kukiwa na ongezeko la wito wa kimataifa wa kufanyia mageuzi chombo cha juu zaidi cha maamuzi cha Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya amani na usalama.

Mnamo mwezi Agosti 2024, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa mabadiliko ya “muundo uliopitwa na wakati” wa Baraza la Usalama, akisisitiza haja ya Afrika kupata kiti cha kudumu, kutokana na uwakilishi wake mdogo katika maamuzi ya kimataifa.

Wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama ambalo, kwa kawaida hujulikana kama P5, ni China, Ufaransa, Urusi, Uingereza, na Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *