Yanga yapiga hodi CAF, mipango yaanza

KATI ya mashirikisho 54 ya soka Afrika ambayo yanapeleka timu zao kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kila msimu, Tanzania tayari imepata mwakilishi wake mmoja, bado mwingine.

Kwa mujibu wa CAF, mashirikisho yaliyopo kwenye orodha ya 12 bora kwa viwango, yanawakilishwa na klabu mbili kwenye Ligi ya Mabingwa.

Kwa wastani, timu 68 zinatarajiwa kushiriki michuano hiyo, lakini tayari mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga imejihakikishia tiketi moja kwa msimu ujao, baada ya kukusanya pointi 70 katika michezo yake 26 ya Ligi Kuu Bara ambazo haziwezi kuwatoa nafasi mbili za juu kwenye msimamo, hivyo moja kwa moja imefuzu.

Simba yenye pointi 57, ikishinda mechi zake zote nane hazitowaathiri Yanga zaidi ya kuungana nao kwani Azam iliyopo nafasi ya tatu (pointi 54) na Singida Black Stars nafasi ya nne (pointi 53), mechi zao tatu zilizobaki haziwezi kuishusha Yanga.

Kitendo cha Yanga kujihakikishia nafasi hiyo, inaungana na miamba mingine kukata tiketi hiyo mapema ambao ni RS Berkane ya Morocco waliopo kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Timu hiyo ilitangazwa bingwa wa Ligi Kuu Morocco ‘Botola Pro’ msimu huu baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Union Touarga Sport, ikiwa ni ubingwa wake wa kwanza tangu kuanzishwa kwao, ikiwa na pointi 60, kufuatia kucheza michezo 26, ikishinda 18, sare sita na kupoteza miwili.

Timu nyingine iliyofuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao ni Mamelodi Sundowns yenye pointi 58, baada ya kucheza michezo 23, ikishinda 19, sare mmoja na kupoteza mitatu, nyuma yake kuna Orlando Pirates inayoshika nafasi ya pili na pointi 46.

Kitendo cha Afrika Kusini kupeleka timu mbili Ligi ya Mabingwa, kinaonyesha wazi Mamelodi kimahesabu imefuzu michuano hiyo kwani hata kama Sekhukhune iliyopo nafasi ya tatu na pointi 40, ikishinda mechi sita zilizobaki itafikisha 58, sawa na za Mamelodi.

Miamba mingine iliyofuzu ni Al-Hilal Omdurman na Al-Merreikh za Sudan ambazo zinashiriki Ligi ya Mauritania kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyopo nchini kwao, hivyo hata kama zitamaliza mkiani hazitaathiriwa na lolote na zimefuzu pia moja kwa moja. Katika Ligi ya Mauritania, Al Hilal iko nafasi ya tatu na pointi 43, baada ya kucheza michezo 19, ikishinda 13, sare minne na kupoteza miwili, nyuma ya Douane iliyo nafasi ya pili na pointi 44 na vinara wa ligi hiyo, Nouadhibou wenye 47.

Kwa upande wa Al-Merreikh, iko nafasi ya sita katika Ligi ya Mauritania ikiwa na pointi 36, baada ya kucheza michezo 25, ikishinda 10, sare sita na kupoteza tisa, hivyo inaungana moja kwa moja na ndugu zao, Al-Hilal kufuzu Ligi ya Mabingwa.

Katika Ligi ya Zambia, Power Dynamos inahitaji pointi tatu kwenye michezo miwili iliyobakia ili kukata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, kwani itafikisha 67, ambazo hazitafikiwa na Zesco inayoshika ya pili na pointi 60.

Dynamos ina pointi 64 baada ya kucheza michezo 32, ikishinda 19, sare saba na kupoteza sita ikiwa na pointi 64, huku ikibakiwa na miwili ambayo inahitaji kufikisha pointi 67 ambazo hazitafikiwa na Zesco kwani itaishia na pointi zake 66.

Nkana yenye pointi 55 ikiwa nafasi ya tatu baada ya kushinda michezo 15, sare 10 na kupoteza saba, hata ikishinda mechi zake mbili zilizobakia itaishia na 61, hivyo nafasi kubwa iko kwa Power Dynamos au Zesco ya kucheza Ligi ya Mabingwa.

MIKAKATI YAANZA MAPEMA

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amezungumzia ishu ya timu hiyo kukata tiketi mapema ili kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao akisema tayari mipango ya kuboresha kikosi imeanza.

“Sasa hivi kikanuni ukiangalia pointi ambazo Yanga tuko nazo moja kwa moja tumefuzu Ligi ya Mabingwa kwa sababu anayeshika nafasi ya tatu hawezi kutufikia…hii maana yake ni kwamba maandalizi yanakwenda sambamba na msimu unavyomalizika.

“Wachezaji bora wengi lazima uanze kuwatafuta mapema, kama mchezaji yupo huru maana yake mkataba wake unaelekea kumalizika na yule mwenye mkataba mazungumzo na klabu yake yanaanza kipindi hiki.

“Tumeanza kuboresha timu yetu kwa ajili ya msimu ujao, maboresho ya kwanza ni kubakisha nyota tulionao kwa mujibu wa ripoti ya mwalimu, wale ambao watataka kuondoka, tutaangalia kwa maslahi ya klabu nani tumuondoe, lakini malengo makubwa ni kutengeneza timu ya msimu ujao kwa sababu tayari tuna tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa,” alisema Kamwe.

Msimu huu 2024-2025, Yanga ilishiriki Ligi ya Mabingwa na kuishia hatua ya makundi ikimaliza nafasi ya tatu Kundi A nyuma ya vinara Al Hilal na MC Alger. Msimu uliopita 2023-2024 ilifika robo fainali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *