
Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imekutana na wadau wa uchaguzi wilayani Magu, mkoani Mwanza kwa lengo kujiridhisha kuhusu mapendekezo ya ugawaji wa jimbo hilo.
Magu ni miongoni mwa majimbo mengi ambayo wadau wa uchaguzi wilayani humo, wamependekeza ligawanywe ili kurahisisha huduma za kijamii.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na INEC leo Jumatano Aprili 23, 2025 imeeleza Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele ndiye aliyeongoza kikao hicho cha wadau wa uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu.
”Tulipokea maombi ya mapendekezo ya kugawa jimbo la Magu Machi 11, 2025 kutoka kwa Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, hivyo kikao hiki ni kifupi, lengo lake ni kujiridhisha na takwimu na jina la jimbo kama mlivyowasilisha.”
“Hii ni sehemu ya jukumu la tume la kuwashirikisha wadau wake wa uchaguzi,” amesema Jaji Mwambegele katika taarifa hiyo.
Jaji Mwambegele amesema INEC imechagua kutembelea baadhi ya majimbo yaliyoomba kugawanywa ili kujiridhisha iwapo taarifa zilizopo kwenye maombi yaliyowasilishwa ni sahihi kuhusu jimbo husika.
Amesema kwa mujibu wa ibara ya 75(4) na 74(6) (c) za Katiba ya Tanzania ya Mwaka 1977 ikisomwa pamoja na kifungu cha 10(1)(d) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 2024, INEC ina jukumu la kuchunguza na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika majimbo ya uchaguzi.
“Tume inaweza kutekeleza jukumu hilo mara kwa mara au angalau kila baada ya miaka 10. Ibara ya 75(3) na (4) imeainisha vigezo vya ugawaji wa majimbo ambavyo ni idadi ya watu, upatikanaji wa mawasiliano na hali ya kijiografia.
“Vigezo vingine vinavyozingatiwa na Tume katika kugawa majimbo vimeainishwa katika Jedwali la Tatu la Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024,” amesema Jaji Mwambegele.
Amevitaja vigezo hivyo ni pamoja na hali ya kiuchumi, ukubwa wa eneo la jimbo husika, mipaka ya kiutawala, jimbo moja kutokuwa ndani ya wilaya au halmashauri mbili, mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo na mazingira ya muungano.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na viongozi wa mkoa wa Mwanza, wakiwemo wa wilaya ya Magu vyama vya siasa, wawakilishi wa makundi mbalimbali ya wanawake, vijana, wenye ulemavu na wazee wa kimila.
INEC ilitangaza kuanza kwa mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi ambapo ilipokea mapendekezo kuanzia Februari 27 hadi Machi 26, 2025.