
Waasi wa M23 wamesitisha ushiriki wao katika mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya Kongo huko Doha, nchini Qatar. Majadiliano haya, ambayo yalichukua karibu wiki tatu, hayakuzaa matunda, licha ya mikutano michache ya moja kwa moja kati ya wajumbe kutoka pande hizo mbili. Hakuna maendeleo makubwa ambayo yamepatikana, kulingana na vyanzo vilivyo karibu na mazungumzo haya.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Kwa mujibu wa vyanzo vilivyowasiliana na Radio Okapi, wajumbe wa vuguvugu la waasi la M23/AFC, wakiongozwa na naibu mratibu wake Bertrand Bisimwa, waliondoka Doha siku ya Jumanne kurejea Goma, ambako AFC/M23 imekuwa na makao yake makuu kwa wiki kadhaa.
Kwa mujibu wa vyanzo hivi, mazungumzo hayo yalishindikana kutokana na kutoelewana kwa kina, hasa kuhusu rasimu ya taarifa ya pamoja, iliyonuiwa kuweka msingi wa mazungumzo yenye kujenga kati ya pande hizo mbili.
Kulingana na vyanzo vilivyonukuliwa na Radio Okapi, wawakilishi wa serikali ya Kongo walisisitiza kwamba taarifa ya Doha inasema wazi kwamba ilifuata mkutano kati ya Marais Félix Tshisekedi na Paul Kagame. Inasemekana kuwa AFC/M23 walikataa ombi hili, wakisema kwamba mzozo kati ya Kinshasa na Kigali hauwahusu, kwani waasi wana madai yao na sababu zao.
Hoja nyingine ya mzozo: wajumbe wa serikali waliripotiwa kutaka pande zote mbili kujitolea kuhimiza makundi yenye silaha kuweka chini silaha zao, jambo ambalo AFC/M23 inaripotiwa kulipinga, wakiishutumu Kinshasa kwa kushirikiana na wanamgambo kadhaa kutoka makundi hayo.
Zaidi ya hayo, kundi hili la waasi liliripotiwa kutaka askari wa Jeshi la DRC (FARDC) na washirika wao, wapiganaji wa Wazalendo, kuondoka Walikale, mji ambao hivi karibuni ulichukuliwa tena na vikosi vya jeshi la serikali baada ya waasi hao kuondoka. M23 inachukulia kujiondoa huku katika mji wa Walikale na kujipanga upya kama ishara ya nia njema.
Hata hivyo, kikwazo kikuu na hoja ya kutokubaliana itakuwa katika masharti yaliyowekwa na waasi, na kupitishwa kwa upatanishi wa Qatar kabla ya mazungumzo. AFC/M23 inashutumu serikali kwa kuwapuuza, kwa kuona hii kama ushahidi wa imani mbaya.
Kundi hili la waasi sasa linatoa masharti kwa kuanza tena kwa mazungumzo yoyote kwa Kinshasa kuteua “wajumbe wenye uwezo wa kufanya maamuzi ya wazi, na sio tu wataalam wenye mamlaka isiyoeleweka.” Wapatanishi wa Qatar bado hawajatoa maoni yao.