Mashariki mwa DRC: Umoja wa Mataifa unaripoti ongezeko kubwa la unyanyasaji dhidi ya wanawake

Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, bado liko katika mzozo wa vita. Hali hii ina madhara makubwa kwa raia. Kulingana na ripoti ya hivi punde kutoka Ofisi ya Pamoja ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (UNJHRO), hali ya haki za binadamu nchini humo ilizorota mwezi Februari 2025. Ukiukaji wa haki za binadamu umejikita katika maeneo yenye migogoro mashariki mwa nchi.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Na mwandishi wetu mjini Kinshasa, Paulina Zidi

Umoja wa Mataifa umerekodi zaidi ya wahasiriwa 1,200 wa ukiukaji wa haki za binadamu na dhuluma kote DRC mwezi wa Februari. Idadi hii inawakilisha ongezeko la 47% ikilinganishwa na mwezi wa Januari 2025. Kama ilivyokuwa katika vipindi vya awali, ripoti nyingi zaidi zilipokelewa katika mikoa iliyoathiriwa na migogoro: Kivu Kaskazini, Ituri, na Kivu Kusini, ambapo idadi ya ukiukaji iliongezeka kwa 158% katika mwezi mmoja tu.

UNJHRO inatahadharisha haswa juu ya kuongezeka kwa unyanyasaji wa kijinsia: +152%. Wasiwasi sawa kuhusu ukiukaji unaoathiri watoto: + 137% ikilinganishwa na mwezi wa Januari. Tena, ni katika maeneo ya vita ndipo kunapatikana kesi nyingi zaidi.

Hali pia imezorota katika mikoa ambayo haina migogoro. Takriban visa 45 vya vurugu na ukiukwaji wa haki za binadamu vimerekodiwa na Umoja wa Mataifa katika maeneo mengine ya DRC, ongezeko la 28%. Kwa ofisi ya pamoja, data hii inaonyesha “ongezeko la watu kukamatwa kiholela na kuwekwa kizuizini katika mikoa ya Haut-Katanga na Kinshasa katika muktadha wa upanuzi wa waasi wa M23.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *