NIKWAMBIE MAMA: Mdharau mwiba huota tende

Bwana au bibi harusi anayekosa dukuduku siku ya harusi yake, ujue hana mzuka nayo. Ni lazima bibi harusi akaribie kuzimia wakati anasubiri jibu la “ndiyo ninakubali” kutoka kwa mumewe mtarajiwa. Kadhalika mwanamume ni lazima akumbwe na hali hiyo pale bi harusi anapovuta pumzi kabla ya kutoa jibu lake mwanana. Jibu hili ndiyo hatima ya ndoa yao.

Uchaguzi ni zaidi ya ndoa. Ni lazima mgombea apatwe na dukuduku ikiwezekana hata kukosa mapigo ya moyo wakati akisubiri matokeo ya uchaguzi. Vinginevyo atakuwa si mshindani wa kweli, naweza kumfananisha na bibi arusi anayefunga ndoa kwa ajili ya kutoa gundu. Ni kipindi kigumu sana, na ndiyo maana mapito yake ni hekaheka mtindo mmoja.

Wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2025, presha ni kitu cha kawaida sana kwenye vyama na wagombea wao. Ni kawaida kutokea makosa ya kizembe kama vile mtoto anaposahau kalamu siku ya mtihani. Ukimpa adhabu mtoto wa aina hiyo unamvuruga akili na kumtoa kwenye mstari wake wa kufaulu.

Serikali ndiye baba wa vyama vyote vya siasa vilivyoingia kwenye ushindani. Ndiyo yenye mamlaka ya kufagia uwanja na kuondoa vigingi ili mchuano uende sawa kwa wote. Ni kama tunavyoona sheria za soka zinavyofuatwa.

Timu iliyoanzia upande wa Kaskazini mwa uwanja kwenye kipindi cha kwanza, itaenda kumalizia kwenye upande wa Kusini kwenye kipindi cha pili.

Hii ni kuepuka manung’uniko ya timu inayoshindwa, kwamba wao walipangiwa bondeni na wenzao kileleni. Au wasije kusingizia walipangiwa upepo unakoelekea ili wazidiwe nguvu.

Ni lazima anayeshindwa akubali, kama atagoma basi jamii nzima ione uhalali na uharamu wa mgomo wake. Iwapo haki yake inaonekana basi apewe.

Lakini malalamiko ya wakati na baada ya uchaguzi yanaashiria mapungufu ya mchakato mzima. Kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa 2020 kulikuwa na malalamiko mengi kutoka kambi ya upinzani na wananchi wengine. Makosa yalionekana kujirudia hata kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huu.

Tume iliyakiri baadhi na kuahidi kuchukua hatua. Lakini ni kawaida kwa mtu aliyegongwa na nyoka kushtuka pale ujani unapomgusa mguuni.

Watu wamekuwa na wasiwasi wa kuendelea kujirudia kwa makosa hayo kila uchaguzi utakapofanyika. Wahenga walisema “wasiwasi ndiyo akili”, na kupitia wasiwasi lazima malalamiko yajitokeze.

Malalamiko mengi dhidi ya Serikali yanatokana na watendaji wake. Watendaji wanajichukulia maamuzi kwa faida yao, na kwa bahati mbaya wanafanya hivyo wakiwa na kofia za Serikali. Kwa mfano unaiadabishaje Tume inapoonesha mapungufu yaliyo dhahiri. Inawezekana hapa ndipo penye ugumu na panaposababisha Serikali kurushiwa lawama za moja kwa moja.

Serikali inaweza kupata picha ya kinachoendelea mtaani kwa urahisi sana. Wapelelezi wa Urusi, Marekani na Ulaya walisimika sanamu za viongozi wao kwenye bustani za wazi. Raia walipokwenda kujipumzisha pale bustanini na kuzikuta sanamu zile, mijadala juu ya viongozi wao ilianza. Walijikuta wakiongelea mafanikio na mapungufu ya watawala wao.

Wapelelezi walipoona raia wakipandwa na jazba kiasi cha kuipiga mawe sanamu ya mkuu, walipeleka habari kwenye chombo cha juu zaidi (Warusi walikuwa na baraza la Politburo). Chombo hicho ndicho kilichoamua nini la kufanya kwenye wakati kama huo, au kama kuna haja ya kuendelea na kiongozi asiyekubalika na wananchi wake.

Watanzania hawana haja ya kusimikiwa masanamu wala kupelelezana. Malalamiko yao yanawafikia viongozi wa chini kwa urahisi sana. Tatizo viongozi hao hawakuletei kwa kuchelea hatima zao. Wanakudanganya kuwa wanakubalika huku mtaani ili waendelee kusalia kwenye nafasi zao. Na inawalazimu kushinda kibabe ili waendelee kukudanganya kuwa wanakubalika.

Hawa ndio wanaoibebesha Serikali zigo la lawama. Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko juu ya Serikali kufumbia macho figisu za uchaguzi.

Tuhuma hizi zinakuja baada ya kuonekana Tume ikisawazisha kambi moja na kuadhibu kambi nyingine kutokana na makosa yanayofanana. Kwa mfano kujaza fomu upya badala ya ile iliyokosewa, au kufutiwa nafasi baada ya kukosea kujaza fomu.

Kumbe nyuma ya pazia kuna baadhi ya wagombea wanaowatisha wasimamizi kwa kinyago cha Serikali. Wanavaa majoho ya mamlaka kwa mfano wa bondia mmoja kuvaa koti la mwamuzi kwenye pambano lake mwenyewe.

Lakini kwa vile wameiwamba sauti ya chini isifike juu wala macho ya juu yasione chini, hakuna wa kumfunga paka kengele.

Ndicho kilichotokea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mapema mwaka huu. Wafuasi wa chama tawala waliandamana kupinga matokeo ya uchaguzi mitaani mwao baada ya kuletewa wagombea wasio machaguo yao.

Malalamiko yao hayajafanyiwa kazi mpaka wakati wakielekea uchaguzi mkuu. Hili halijapita, ila ni bomu linalosubiri muda wa kulipuka.

Malalamiko yote yafanyiwe kazi kabla kipyenga hakijapulizwa. Ieleweke kuwa makosa mengi ni vivuli vya yale yaliyopita. Hivyo kama yataendelea kupanga foleni, kutakuwa na mnyororo mrefu wa matatizo.

Haya yatazalisha harakati na kaulimbiu nyingi zitakazotazamwa kwa jicho la uhaini; wagombea watakamatwa, na vyama vitasusia uchaguzi.

Hili litaibainisha Serikali kuwa “Mdharau mwiba.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *