Papa Francis wa Kwanza, mwanaharakati mkereketwa aliyefungamana na Rais Samia

Machi 13, 2013 mpaka Aprili 21, 2025, inakuwa miaka 12, mwezi mmoja na siku nane, hizo ni tarakimu za Jorge Mario Bergoglio, kutumikia wadhifa wa Askofu wa Roma na Kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni. Utambulisho rasmi kicheo ni Papa. Alichagua kutumia jina la Francis I, kwa heshima ya Mtakatifu Francis wa Assis.

Machi 11, 1958, Papa Francis akiwa na umri wa miaka 21, alijiunga na shirika la Jamii ya Yesu (Jesuit). Shirika hilo ni jumuiya ya Kanisa Katoliki, iliyoanzishwa Karne ya 16 na Mtakatifu Ignatius wa Loyola, kwa idhini ya Papa Paul III. Msingi wa Jesuit ni utumishi wa kibinadamu, kusaidia jamii, kujenga umoja wa Wakristo wa madhehebu yote na kadhalika.

Papa Francis alijiunga na Jesuit kama shukurani kwa Mungu, baada ya kunusurika kifo kutokana na maradhi ya pumu, ambayo chanzo chake ni majipu matatu kwenye pafu. Alifanyiwa upasuaji na kuondolewa pafu moja. Papa Francis amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88, hivyo aliishi miaka 67 na pafu moja.

Zipo namba moja nyingi kwenye wasifu wa Papa Francis. Ni mwanachama wa kwanza wa Jesuit kuwa Papa. Mzawa wa kwanza wa Amerika kuwa Papa. Mtu wa kwanza kutoka Kusini ya ikweta (Southern Hemisphere) kuwa Papa. Binadamu wa kwanza aliyezaliwa au kukulia nje ya Ulaya kuwa Papa, tangu Karne ya Nane, Kanisa Katoliki lilipoongozwa na Papa Gregory III, raia wa Syria.

Mzaliwa wa Buenos Aires, Argentina, Juni 27, 1992 alisimikwa Uaskofu wa Burgos, Juni 3, 1997, alitawazwa kuwa Askofu Msaidizi wa Buenos Aires, Februari 28, 1998, akawa Askofu Mkuu wa Buenos Aires, mwaka 2001, alisimikwa Ukardinali na Papa John Paul III, Machi 13, 2013 akachaguliwa kuwa Papa baada ya Papa Benedict XVI kujiuzulu. Aprili 21, 2025, akafunga agano la uhai na kuirejea asili; mavumbini.

Papa Francis, miaka yake 12 ya uongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni, inampambanua kuwa kiongozi wa kiimani aliyetoka nje ya sanduku la nyaraka za kimaandiko na kutoa tafsiri yenye wigo mpana kuhusu binadamu, dini, kuabudu na utu wema.

Nukuu zake mbili, zinaweza kutosheleza ujenzi wa hoja. Ya kwanza alisema: “Namwamini Mungu, siyo Mungu wa Katoliki. Hakuna Mungu wa Katoliki. Kuna Mungu, na namwamini Yesu Kristo, mwili wake. Yesu ni mwalimu wangu na mchungaji wangu, lakini Mungu, Baba, Abba, ni nuru ni Muumba.”

Nyingine, Papa Francis alisema: “Si lazima kumwamini Mungu uwe mtu mwema. Kuna namna, utamaduni wa taifa la Mungu umepitwa na wakati. Mtu anaweza kuwa wa kiroho lakini hana dini. Si lazima kwenda kanisani. Kwa watu wengi, asili inaweza kuwa Kanisa. Baadhi ya watu bora katika historia hawakumwamini Mungu, wakati baadhi ya waovu kupindukia walitenda kupitia jina la Mungu.”

Papa mwanaharakati

Miaka yake 12 ya uongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis alijitoa kwa asilimia 100 kama mwanaharakati wa mazingira. Kupitia mafundisho yake na hamasa kwa jamii, aliunganisha mabadiliko ya tabia nchi kuwa suala la kiroho. Siku zote alisisitiza kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya ongezeko la joto ulimwenguni, ufukara na misukosuko ya kijamii.

Eneo la ukereketwa wa mazingira, ndilo linamfanya Papa Francis kufungamana na Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan. Tangu Rais Samia alipoingia madarakani, amekuwa mstari mbele kwenye mapambano ya mazingira.

Rais Samia amekuwa championi wa nishati safi ya kupikia ili kulinda afya za wapishi, wengi wao wakiwa wanawake, vilevile kuepusha uharibifu wa mazingira. Eneo hilo la mazingira kwa sehemu kubwa, linawafanya wawe wazalendo wanaoshabihiana. Mazingira kwao ni vita ya moyoni.

Februari 11, 2024, Papa Francis, baada ya misa takatifu, Kanisa la Mtakatifu Peter (St Peter’s Basilica), alimpokea Rais Samia. Papa Francis, alimwalika Rais Samia, na walifanya mazungumzo ndani ya Jumba la Mitume la Sixtus V (Apostolic Palace), ambalo ndiyo makazi rasmi ya Papa. Siku hiyo, (Februari 11, 2024), ilikuwa maadhimisho ya miaka 95 ya uhuru wa Dola ya Vatican. Februari 11, 1929, aliyekuwa Mfalme wa Italia, Victor Emmanuel III na Papa Pius XI, walisaini Mkataba wa Lateran, ulioitambua Vatican kuwa ni Kiti Kitakatifu (The Holy See). Mkataba huo ulihalalisha Vatican kuwa nchi huru na inayojitegemea, ndani ya Jiji la Roma. Mkuu wa Dola ya Vatican ni Papa.

Mtandao wa Vatican News, uliripoti kuwa mazungumzo ya Papa Francis na Rais Samia, kwa sehemu kubwa yalihusu mazingira, amani ya nchi za Afrika Mashariki, vilevile uhusiano wa kihistoria baina ya Tanzania na Kanisa Katoliki.

Papa mpenda amani

Januari na Februari 2023, Papa Francis, alifanya ziara DRC na Sudan Kusini, nchi ambazo zina machafuko. Tukio lililoteka hisia ni la Papa akiwa Sudan Kusini, kupiga magoti na kubusu miguu ya Rais wa nchi hiyo, Salva Kiir na Makamu wa Rais, Riek Machar, akiwaangukia waache vita na wajenge taifa moja.

Imepita miaka miwili tangu Papa Francis alipofanya ziara DRC na Sudani Kusini. Nchi hizo hali imeendelea kuwa mbaya. Inasikitisha kuwa Papa Francis ameondoka duniani, bila makundi yenye kupigana Sudan Kusini na DRC kuheshimu juhudi zake za upatanisho.

Mtazamo tata kiimani

Papa Francis aliuambia ulimwengu kwamba mapenzi ya jinsi moja siyo uhalifu, ila ni dhambi kwa Mungu. Alitaka dunia iachane na sheria zenye kutafsiri mapenzi ya jinsia moja kama uhalifu, badala yake lishughulikiwe kiroho.

Desemba 18, 2023, Papa Francis, alitoa ruhusa kwa mapadri kuwabariki wapenzi wa jinsia moja kuwa wanandoa kamili. Ruhusa hiyo ilitoka kupitia azimio la Papa, aliloliita “Fiducia Supplicans”, lililofafanua kuwa hayo ni maendeleo halisi, lakini halibatilishi mafundisho na msimamo wa Kanisa Katoliki, kuhusu ndoa.

Mkazo ni kuwa Kanisa Katoliki linasimamia ndoa yenye kukutanisha mwanamume na mwanamke. Wanaume wawili (wapenzi) au wanawake wawili (wapenzi), ni mwiko kwa Kanisa kuwafungisha ndoa. Hata hivyo, Papa Francis aliruhusu wapenzi wa jinsia moja ambao tayari wanaishi pamoja, wabarikiwe.

Januari 29, 2024, gazeti la Italia “La Stampa”, lilichapisha mahojiano ambayo lilifanya na Papa Francis. Kupitia mazungumzo hayo, Papa alisema, anaelewa msimamo wa maaskofu kutoka Afrika kuhusu ndoa za jinsi moja kuwa ni jambo baya. Akasema Afrika kwenye suala la mapenzi ya jinsia moja ni kesi maalumu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *