Dar es Salaam. Wakati Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, likisema halimshikilii Makamu mwenyekiti wa Chadema, John Heche, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Aman Golugwa amesema bado wanamtafuta kiongozi huyo kujua ni kituo kipi cha Polisi anakoshikiliwa.
Heche anadaiwa kukamatwa leo Jumanne Aprili 22, 2025 muda mfupi baada ya kuanza mkutano wa hadhara ambao ni mwendelezo wa kutoa elimu kuhusu kampeni yao ya ‘No reforms, no election’ (Bila mabadiliko, hakuna uchaguzi) katika Mtaa wa Mkunguni na Nyamwezi mkabala na Soko Kuu la Kariakoo.
Mwananchi lilizungumza na Golugwa kutaka kujua kiongozi huyo amepelekwa katika kituo gani cha Polisi kiongozi huyo amesema; “Hadi sasa hatujui kiongozi wetu alipo tumezunguka vituo vyote, Kituo cha Central Polisi na Osterbay bado hatujamuona.”

Kulingana na Golugwa wakati anakamatwa maeneo ya Mkunguni, alipakizwa kwenye gari lakini walipokaribia maeneo ya Polisi Central walimbadilisha na kumpandisha kwenye gari lingine.
“Sasa kuna gari tunaifuatilia kujua ni wapi amepelekwa kuhifadhiwa ili tujue,” amesema
Kufuatia malezo hayo, alipoulizwa Kamanda wa Kanda Maalumu, Jumanne Muliro amesema “Kifupi hatujakamata mtu isipokuwa tulikuwa tunatuliza hekaheka zilizokuwa zinaendelea katika eneo lile na kama si jeshi la Polisi kuwa sehemu ile kuna kitu kibaya kingetokea,”

Kulingana na Muliro amesema Jeshi la Polisi walichokifanya ni kusambaratisha watu waliokuja na kiongozi huyo John Heche ili kurejesha utulivu wa eneo hilo baada ya kubaini jambo la uvunja sheria lingetokea.
“Hatuja mkamata Heche kama una namba yake mpigie kwanza alafu utaniuliza maswali yako,” amesema
Katika maelezo yake, Muliro amesema mikutano ya hadhara imeruhusiwa kufanyika lakini awali waliwapa tahadhari lakini walidharau.
“Lazima ifike mahali tuheshimiane tunapofikia kufanya kazi, ukishauriwa jambo na mamlaka lazima uzingatie kwa faida ya usalama,” amesema.
Endelea kufuatilia Mwananchi.