Masauni aja na hoja sita 4R za Rais Samia

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, ametaja mafanikio sita yaliyopatikana nchini kupitia falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan, yakiwemo vyama vya siasa kufanya shughuli zao kwa uhuru.

Mbali na mafanikio hayo, Masauni amesema falsafa hiyo ni daraja la kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kiongozi huyo ametoa kauli hiyo leo Aprili 22, 2025, alipokuwa akifungua Kongamano la Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema falsafa ya 4R zinazojumuisha maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya Taifa, zimeendelea kujenga umoja wa kitaifa, mapenzi na undugu bila kujali tofauti za kiitikadi.

“Kupitia falsafa hii mambo mengi yamefanyika, tumeimarisha mfumo wa haki jinai, uhuru wa kujieleza, uhuru kwa vyama vya siasa kufanya kazi zao, mazungumzo na ushirikishwaji, mabadiliko ya sheria za uchaguzi na vyama vya siasa na sheria ya Tume ya Uchaguzi.

“Mama Samia ana majina mengi je, tukimuita Mama mageuzi tutakuwa tumekosea?” alihoji Masauni.

Akizungumzia maadhimisho ya Muungano, Masauni amesema falsafa hiyo imeimarisha uhusiano wa pande mbili za muungano.

Amesema misingi ya muungano imejengwa juu ya undugu wa kihistoria kati ya Tanganyika na Zanzibar, jiografia ya mataifa hayo na utashi wa wazee waliouamini umoja, mshikamano, ushirikiano na upendo.

Masauni ameeleza kuwa Aprili 26, 1964, waasisi wa Tanganyika na Zanzibar walikubaliana kuunda nchi huru, ambayo wananchi wenyewe waliiunda.

“Tangu kuasisiwa kwa muungano huu, tumeendelea kupata mafanikio katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Muungano huu umebaki kuwa kielelezo cha umoja, undugu na utaifa wetu kama Watanzania,” amesema Masauni.

Amebainisha kuwa mafanikio ya muungano hayaonekani ndani ya nchi pekee, bali hata kimataifa ambapo Tanzania inatambulika kama nchi moja yenye sera thabiti ya diplomasia ya uchumi.

Amesisitiza Zanzibar na Tanzania Bara si washindani, bali ni sehemu ya nchi moja inayolinda masilahi yake kupitia diplomasia ya uchumi.

“Muungano huu ni wa watu, hivyo unaishi na kutimiza malengo ya wananchi wake,” amesema.

Kuhusu changamoto za Muungano, Masauni amesema haziwezi kuepukika, lakini zimekuwa zikitatuliwa kadri zinavyojitokeza.

“Watu hujiuliza kwa nini Muungano huu umedumu, ilihali mingine huvunjika. Hii ndiyo sababu yake, tumekuwa na utaratibu mzuri wa kushughulikia changamoto,” amesema.

Amebainisha changamoto za Muungano zilikuwa 25, lakini sasa zimebaki tatu tu, ambazo nazo zipo katika hatua mbalimbali za kutatuliwa.

Katika uongozi wa Rais Samia, Masauni amesema hoja 15 kati ya hizo zimeshapatiwa majibu, na alitabiri kuwa zilizobaki zitapatiwa ufumbuzi kabla ya kumalizika kwa awamu ya uongozi wake.

Amesisitiza uwepo wa changamoto haiondoi maana ya muungano, bali jambo la msingi ni kuzitambua na kuzitatua kwa masilahi ya pande zote mbili.

Kuhusu utoaji wa elimu ya muungano, amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imekusudia kuanzisha mkakati wa kudumu wa utoaji elimu ambao hautasubiri tu maadhimisho ya Muungano.

“Baada ya sherehe za Muungano, tutaendelea kutoa elimu kwa umma. Mkakati huu utahusisha njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na makongamano, na kulenga zaidi makundi ya vijana kupitia shughuli wanazopendelea,” amesema.

Mjadala wa muungano

Katika mjadala wa kongamano hilo kuhusu muundo wa Muungano, aliyewahi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harison Mwakyembe amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni wa nchi mbili huru zilizokuwa wanachama wa Umoja wa Mataifa, zilizokubaliana kuungana.

Amesema barani Afrika kulikuwa na majaribio mengi ya muungano, ambapo hayati Mwalimu Julius Nyerere alijaribu kushirikiana na Marais Jomo Kenyatta (Kenya) na Milton Obote (Uganda) kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki, lakini mwitikio haukuwa mkubwa.

“Alipoona mwitikio ni mdogo, Mwalimu alipendekeza tukishaunda shirikisho, Mzee Kenyatta awe Rais wa kwanza. Alikuwa tayari kuchelewesha uhuru wa Tanganyika ili tuanze pamoja kama Shirikisho la Afrika Mashariki,” amesema Dk Mwakyembe.

Ameongeza, baada ya kushindwa kwa juhudi hizo, alimuona mzee Abeid Karume ndiye aliyekuwa tayari kushirikiana naye kuunda Muungano.

Kwa upande wake aliyewahi kuwa Makamu wa Rais Zanzibar, Hamad Rashid Hamad amesema mwaka 1983, baada ya baadhi ya Wazanzibari kulalamika kuwa hayati Mwalimu Nyerere anaing’ang’ania Zanzibar, alimwuliza Mwalimu kuhusu hilo.

“Mwalimu alisema yeye ni muumini wa majumui na aliamini katika umoja. Karume naye alikuwa muumini wa jambo hilo ikiwa na maana kuwa muumini ni tofauti na mfuasi.

Sisi tulikuwa wanamajumui wa Muungano huu. Wanaouliza ni wafuasi na mfuasi anaweza kubadilika wakati wowote,” amesema Hamad.

Kuhusu madai kuwa Muungano unaunufaisha upande mmoja zaidi ya mwingine amesema,” Muungano ulipo si wa vitu bali wa watu na ulijengwa juu ya misingi minne.

“Misingi hiyo ni umoja, utu, usalama na amani pamoja na usimamizi wa rasilimali kwa masilahi ya nchi zote mbili.”

Akidokeza kuhusu kero za Muungano, Hamad ameshauri zilizopatiwa ufumbuzi wananchi wawe wanapewa taarifa na kuelezwa taratibu zilizopo.

“Kuna mambo mengine yanahitaji kanuni, sheria na mengine Katiba, mfano suala la mafuta linahitaji Katiba, suala la fedha za pamoja linahitaji utekelezaji sheria zipo Katiba ipo tayari wakielezwa wananchi wataelewa na kelele zilizopo zitaondoka,” ameeleza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *