
Dodoma. Serikali imetaja mikakati ya kulinda haki za watoto kuwa ni pamoja na adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa atakayempa mimba mwanafunzi, huku wazazi wasiolea na kutunza watoto adhabu yao ni faini isiyozidi Sh5 milioni au kifungo miezi sita au vyote kwa pamoja.
Adhabu hizo zimetajwa bungeni leo Jumanne Aprili 22, 2025 na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum Najma Giga (CCM).
Naibu Waziri amesema lengo ni kukomesha ukatili wa watoto na kuifanya jamii iishi kwenye maisha ya amani na furaha ikiwemo kuwalinda watoto.
Katika swali la msingi Giga alitaka kufahamu serikali ina mkakati gani wa ziada wa kulinda haki za watoto, kwa vile kuna ongezeko kubwa la uvunjifu wa haki za watoto nchini.
Naibu Waziri ametaja mikakati yake ya ziada ya kulinda haki za watoto ikiwemo kutekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto wa 2024-2029 unaolenga kutokomeza ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2029.
Mwanaidi alitaja mikakati mingine ni kuendelea kuelimisha jamii kuhusu Sheria za Ulinzi wa Mtoto kwani ndiyo tiba halisi ya kumaliza migogoro hiyo.
Amesema Serikali itaendelea kuibua kampeni za kuelimisha jamii kuhusu haki za watoto, mfano Kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia (2023-2025).
Naibu Waziri ametaja kampeni nyingine ni kuimarisha kamati za ulinzi wa mtoto kwenye jamii pamoja na madawati ya ulinzi na usalama wa mtoto katika shule za Msingi na Sekondari.