
Dar es Salaam. Mzazi au mlezi ndiye mwalimu wa kwanza wa mtoto. Ni kwa sababu hiyo, hana budi kumfundisha mtoto huyo ujuzi na kumpatia maarifa yatakayomsaidia maishani mwake.
Hatu hiyo itamsaidia mtoto kuepuka ile kauli maarufu isemayo: ‘Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu’ kwakuwa elimu atakayompatia ikiwemo kuishi na watu vizuri kuwa na nidhamu na muda, pesa itamsaidia.
Stadi 20 muhimu kwa watoto
Mwananchi inakutajia mambo muhimu 20 ya mzazi kumsaidia mtoto wake katika makuzi yake.
Mambo hayo ni uwezo wa kutatua matatizo, ujuzi wa mawasiliano, akili ya kihisia, usimamizi wa muda, uwezo wa kusuluhisha migogoro na kufikiri kwa kina.
Mengine ni ni uelewa wa masuala ya fedha, kuwa na nidhamu binafsi, uwajibikaji, elimu ya upishi na usafi na kufanya kazi kwa ushirikiano.
Pia kuna uwezo wa kuweka malengo,kufanya uamuzi, ujuzi wa kazi za mikono, heshima na wema kwa wengine, kuwa na huruma, mazoezi na afya ya mwili, utoaji wa huduma ya kwanza na mwisho, uwezo wa kuendana na mabadiliko na uvumilivu.
Kwa kuwapa watoto aina hizi za stadi, kutawafanya kuhisi kuwa na uwezo zaidi katika kazi zao za kila siku na wana uwezekano mkubwa wa kujiendesha zaidi na kujisikia kuwa na udhibiti zaidi wa maisha yao.
Akizungumza na Mwananchi, mwanasaikolojia Prisca Sao anasema kumfundisha mtoto stadi hizi, kunamsaidia kwa kiasi kikubwa katika maisha yake ikiwamo kumuongezea hali ya kujiamini.
Anasema shule ya kwanza ya mtoto inaanzia nyumbani pale anapokuwa anajifunza kwa kuona na kuiga anapokuwa mdogo na anapoendelea anajifunza kwa kusikia na kwa mifano.
Anasema ujuzi wa maisha anapofundishwa na mzazi au mlezi wake, unamsaidia kuendana na mazingira yaliyopo na dunia inavyotaka.
“Inamsaidia kujitegemea mfano kupika au kutunza hela kwanzia mdogo itamsaidia kujitegemea hadi pale atakapokuwa mkubwa. Mtoto anakuwa anaweza kujijali yeye mwenyewe na kuwajibika kwa uamuzi atakaochukua. Pia inamtengeneza kujiamini yeye mwenyewe bila ya wengine,” anasema.
Anasema wazazi wanapaswa kufundisha haya ili watu wabaya wasimfundishe vitu vibaya kama vile urafiki wa kimapenzi.
“Mzazi usipoweza kumfundisha mtoto wako kuhusu aina gani ya rafiki anapaswa kuwa naye baadaye akisubiri afundishwe na ulimwengu anaweza kukutana na watu wabaya, ” anasema na kuongeza:
‘Mzazi lazima atoe taarifa sahihi ili dunia isije kumpa taarifa zisizo sahihi. Wazazi wanapaswa kusisitiza tabia njema na mwenendo kwa watoto wao.”
Kwa upande wake, mwanasaikolojia Modester Kimonga anasema katika maisha ya mtoto, ujuzi wa namna hiyo utamsaidia kukua nao tangu akiwa mdogo hadi atakapokuwa mtu mzima na ataweza kuishi nao.
“Akikosa stadi hizo atashindwa kujiendesha mwenyewe, kwasababu maisha kwa ujumla yanahitaji kujumuiks na wenzake,” anasema.
Wasemacho wazazi
Mzazi Rashid Maulid, anasema anajuta kutomfundisha mwanawe stadi ndogondogo za maisha, jambo analosema kwa sasa anamsumbua kwakuwa hakumuandaa tangu akiwa mdogo.
Anasema hakumzoesha kufanya mambo yake kwa kujitegemea, heshima kwa ndugu zake na uwezo wa kuishi mazingira magumu mambo ambayo kwa sasa yanampatia shida.
“Tulihama mjini kwa sasa tunaishi maeneo ya vijijini inampa shida kijana wangu wa miaka 15, ndugu zake hajazoeana nao, kazi za vijijini kama kupasua kuni kuchota maji kwenye kisima inamsumbua,” anasema.
Maulid anasema amejifunza hilo na sasa ikitokea kupata mtoto mwingine, atamfundisha kila kitu ili awe na ujuzi katika ukuaji wake.
Naye Rosemary John anasema mtoto wake wa kiume, ana miaka tisa lakini anajua kupika kudeki na kuosha vyombo na kazi zote za ndani.
“Nimefanya hivi kwakuwa sitaki awe tegemezi katika maisha yake. Najua haya yote yatamsaidia katika maisha yake popote pale atakapoenda, sipendi mtoto wangu awe tegemezi,” anaeleza.
Mkazi wa Dar es Salaam, Aman Michael anasema watu wengi sasa hivi wanakosa ujuzi kama wa kuwa na nidhamu ya fedha kwasababu hawakufundishwa tangu walivyokuwa watoto.
‘’Hali ni tofauti kwa wale waliofunzwa udhibiti wa pesa, unakuta wanajielewa waishi vipi na mazingira gani. Mfano kama una hela umetembea nayo ukiona shati na hukuwa umepanga, lakini ukanunua, hiyo ni ishara umekosea nidhamu ya pesa,” anasema.
Anasema huo ni mfano mdogo wa kujua mtu asiyejielewa katika nidhamu ya fedha.