
Dar es Salaam. Ripoti ya ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, imebainisha kuwa jumla ya Sh1.25 bilioni za kugharimia elimu bila malipo, hazikufika kwa mamlaka husika.
Katika ripoti hiyo iliyokabidhiwa kwa Bunge wiki iliyopita, jumla ya mamlaka 15 za serikali za mitaa hazikufikishiwa fedha kamili, hatua ambayo ripoti imetaja kuwa ina athari katika utoaji wa elimu bila malipo.
“Nimebaini kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, haikutoa Sh1.25 bilioni za ruzuku ya elimu bila malipo kwa mamlaka 15 za serikali za mitaa, ikilinganishwa na mahitaji ya Sh 11.83 bilioni kwa mujibu wa
waraka wa ruzuku. Hii imeathiri upatikanaji wa vifaa vya kufundishia, ukarabati wa miundombinu na hivyo kudhoofisha mazingira ya elimu, ” inasema sehemu ya ripoti ikimnukuu CAG Charles Kichere.
Hii si mara ya kwanza kwa ofisi ya CAG kuonyesha namna Serikali inavyosuasua kugharimia sera ya elimu inayotajwa kuwa mkombozi kwa watoto wengi wa familia masikini.
Katika ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2018/19, CAG alibainisha namna Sh2.9 bilioni zilivyoshindwa kufika katika halmashauri 42, akisema utoaji wa elimu bora unahitaji mazingira wezeshi.
‘’Sera ya Serikali ya kuboresha elimu nchini inaweza isitekelezwe kama ilivyopangwa. Ninaishauri Serikali kutoa fedha kulingana na bajeti iliyopitishwa ili kutengeneza mazingira mazuri ya elimu kwa walimu na wanafunzi hivyo kuongeza ufanisi katika elimu na hatimaye kufanikisha malengo yaliyowekwA,’’ alisema Kichere.
Elimu bila malipo sera
Mpango huu ulioanza mwaka 2016 ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambapo Serikali iliamua kugharimia elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Katika ugharimiaji huo, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya Sh6,000 na Sh20,000 kwa wanafunzi wa msingi na sekondari mtawalia.
Wanachosema wadau wa elimu
Mdau wa elimu Ochola Wayoga anasema fedha za kugharamia elimu zinapopelekwa zikiwa ndogo au kucheleweshwa, zinaathiri upatikanaji wa elimu bora na hivyo malengo yaliyowekwa katika sekta hiyo kutofanikiwa.
“Kama fedha haziendi yapo malengo tutashindwa kufikia ikiwemo Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) lengo la nne la ubora wa elimu. Hapa tulipo elimu bora bado haitolewi hivyo kama bajeti itakuwa finyu morali ya walimu itashuka na ari ya wanafunzi kujifunza itashuka,”anasema.
Anasema japo walimu hawatalalamika kwa kutopewa fedha hizo ambazo wakati mwingine zinapaswa kutumika kununua chaki, kulipia huduma mbalimbali shuleni hapo, athari zitaonekana kupitia matokeo ya wanafunzi shuleni.
Ochola anasema sera mpya ya elimu imeanza kutekelezwa na ina mambo mengi ya msingi ikiwemo walimu kupewa mafunzo kuendana na sera hiyo, hivyo kama bajeti itatolewa kwa kusuasua uwezekano wa kutekelezwa kwa ufanisi unaweza kuwa mdogo.
“Kama halmashauri fulani inapata fedha zote na nyingine haipati tunatengeneza madaraja kwenye elimu, Serikali haiwezi kuona kama kuna shida lakini ni tatizo kwani hatuhitaji kuwa na madaraja kwenye elimu,”anaongeza.
Mdau huyo anashauriSerikali kuweka macho katika bajeti ya elimu ili fedha zinazohitajika zitolewe zote, ili kusaidia upatikanaji wa elimu bora kwa wanafunzi.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dodoma (Udom), Christian Bwaya anasema ubora wa elimu unategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa fedha, zinazowezesha kupatikana na vifaa na rasilimali nyingine za kutekeleza mipango iliyowekwa.
“Nafikiri ndio maana uamuzi wa Serikali kutoa ruzuku kwa ajili ya elimu ulikuwa sahihi, kwa maana ya kumhakikishia mtoto haki ya kupata elimu bila kumbebesha mzazi mzigo mzito,’’ anasema na kuongeza:
Taarifa kuwa bilioni 1.25 hazikutolewa zinasikitisha na kwa hakika zinatia doa nia njema ya Serikali kutoa elimu bila malipo. Tukumbuke wazazi wameshajihakikishia kuwa jukumu la malipo linabebwa na Serikali. Katika mzingira haya ni wazi kuna pengo kubwa katika bajeti za mamlaka hizi za serikali za mitaa.’’
Bwaya anasema huenda malipo ya wazabuni hayajafanywa na ni wazi hilo litaathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia na huduma nyingine muhimu kwa ajili ya wanafunzi.
Anasema hakuna kinachoweza kufanyika shuleni kama mwenye fedha hajatoa na inafahamika ni vigumu shule kuwa na vyanzo vingine nje na ruzuku ya Serikali.
“Tunaikumbusha Serikali kuhakikisha ruzuku inapatikana kwa wakati ili kuziwezesha shule kutekeleza mipango yake kama ilivyopangwa,”anasema.
Naye mchambuzi wa masuala ya kijamii, Dk Faraja Kristomus anasema kinachoonekana ni tatizo hata kabla ya CAG kulifichua likishakuwepo kwa miaka kadhaa sasa.
Anasema walimu wakuu wengi wamekuwa wakieleza kuwa pesa za ruzuku zinazofika shuleni kwao ni kiasi kidogo.
“Nakumbuka niliwahi kuchapisha makala kuhusu malalamiko ya walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari kuhusu pesa za ruzuku kutotosha,”anasema.
Mathalani, anasema wanafunzi wa bweni walikuwa wakitengewa Sh 1,700 kwa siku pesa ambayo walimu walikuwa wanadai haifiki yote.
‘’Kiasi fulani kilikuwa kinakatwa na halmashauri. Kiasi hiki mbali na kuchelewa kufika shuleni, bado kimekuwa kidogo sana, kisichokidhi mahitaji ya uendeshaji wa shule. Hali hii inazifanya shule za sekondari za serikali za bweni na za kutwa kuonekana zinatoa elimu duni ukilinganisha na shule binafsi ambazo bajeti ya mahitaji ya mwanafunzi kwa siku ni makubwa zaidi, ‘’ anaeleza.
Anasema jambo linaloumiza zaidi ni kuwa mbali na pesa kuwa kidogo, baadhi ya halmashauri zimekuwa zikinyimwa pesa hizo na hivyo kuleta ukosefu wa usawa kwenye mgawo na hivyo kuathiri huduma za elimu shuleni.
“Mazingira haya ya ukosefu wa pesa za ruzuku yamekuwa yakizilazimu kamati na bodi za shule kuwaomba wazazi wachangie gharama za kuendesha shule hizo. Wakati huohuo uamuzi huo umekuwa ukipingwa na wanasiasa kwa sababu za kisiasa bila ya kuzingatia hali halisi ilivyo shuleni, “anasema.