
Dodoma. Hotuba za bajeti za Wizara ya Utumishi na Utawala bora, Mipango na uwekezaji, Muungano na Mazingira zinangojewa kutokana na kuhusisha maeneo nyeti ikiwamo ajira, uwekezaji pamoja na kilio cha kupanda kwa madaraja na malipo ya wastaafu.
Kabla ya hizo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa atakuwa anahitimisha bajeti yake kesho Jumatatu ya Sh11.7 trilioni.
Katika kikao kinachofuata kwenye Bunge hilo la 12, Mawaziri watatu watawasilisha na kujibu hoja za wabunge katika hotuba za bajeti zao kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Mawaziri wanaosubiriwa ni Mohamed Mchengerwa (Tamisemi) ambaye bajeti yake imeshajadiliwa na wabunge na sasa anasubiri kutoa hitimisho, George Simbachawene (Utumishi na Utawala Bora), Profesa Kitila Mkumbo (Mipango na Uwekezaji) na Hamad Yusufu Masauni (Muungano na Mazingira) ambao wao watasoma hotuba zao wiki hii.
Baadhi ya hoja ambazo zinasubiriwa ni suala la ajira, mazingira ya kibiashara, changamoto za rushwa, vibali vya uhamisho kwa wanandoa, mnyukano wa wabunge na wateule wa Rais majimboni na upungufu wa maabara na vyoo katika shule zilizojengwa hivi karibuni.
Mchengerwa atakuwa wa kwanza kukabiliana na hoja hizo kwani kibarua kinachomngoja ni tayari anakijua kutokana na hotuba yake aliyoiwalisha Aprili 16, 2025 na wabunge kuanza kuchangia.
Katika michango ya wabunge kwa bajeti ya Tamisemi yaliibuka masuala ya upungufu mkubwa wa watumishi, aibu kwa shule mpya kupungukiwa vyoo na maabara lakini hoja ya ubadhirifu ambayo iliibuliwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo kuhusu wizi wa fedha za miradi na ubadhirifu kwenye ujenzi wa jengo la utawala.
Waziri Mchengerwa, pia atatakiwa kujibu hoja za wabunge akiwamo Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma ambaye alitaka wateule wa Rais wanaoyanyatia majimbo wakapimwe kwanza ufahamu na kuchunguzwa kwani wanaweza kuwa na fedha chafu.
Kilio cha Msukuma kilionekana kuwagusa wabunge wengi ambao wanatambua kuna watu wananyatia majimbo yao akiwamo Nicodemus Maganga (Mbogwe) na Dk Charles Kimei (Vunjo) ambao walionyesha wazi kuhusu kuyalinda majimbo yao dhidi ya waliowaita ni wavamizi kutoka nafasi za uteuzi.
Mbunge wa Viti Maalum, Nusrat Hanje aliungwa mkono na wabunge baada ya kuibua hoja ya shule nyingi ambazo hazina maabara na upungufu mkubwa wa vyoo akisema ni aibu kwa karne ya sasa kukimbilia kujenga majengo mazuri lakini hawana vyoo.
Kibarua ya Simbachawene
Mambo mengine yanayotarajiwa kujitokeza katika mjadala wa bajeti za Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ni suala la ajira, kupandishwa kwa madaraja watumishi, malipo ya wastaafu, vibali vya uhamisho na rushwa.
Akifungua kikao kazi kati yake na Wakuu wa Taasisi za Umma, Machi 3, 2025, Waziri Simbachawene alisema kuna watumishi wamekaa zaidi ya miaka 20 hawajawahi kukaa na waume zao kwa zaidi ya mwezi mmoja.
“Wewe ni Mkurugenzi wa Halmashauri unamzuia huyu kutekeleza ombi la uhamisho wakati unajua amekaa zaidi ya miaka 20 pale, hata anapokaribia kustaafu busara zikuongoze uwe na huruma ili huyu mtumishi akajenge familia yake,” alisema Simbachawene.
Ni Simbachawene atakayetakiwa kulitolea ufafanuzi suala la ajira ambalo limekuwa likilalamikiwa hasa aina ya usaili ambao husababishwa waombaji kurundikwa kwa wingi huku wanaotakiwa ni wachache kama ilivyotokea katika ajira za walimu, Zimamoto na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mwishoni mwa wiki Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde (Kibajaji) aliibua sakata hilo kwenye mchango wake akitaka Serikali itoa majibu kuhusu namna ya kusaili waombaji wa ajira mpya kwa madai kuwa mfumo uliopo sasa unatoa mianya rushwa na usumbufu.
Kwa Wizara ya Mipango na Uwekezaji iliyochini ya Profesa Kitila Mkumbo, sakata la wafanyabiashara wa kigeni ambao inasemekana wamejazana katika Soko la Kariakoo litaibuliwa na wabunge.
Katika mjadala wa Hotuba ya Waziri Mkuu kwa makadirio ya fedha kwa mwaka 2025/26. Jambo hilo lilijitokeza ambao inadaiwa raia wa kigeni wanauza vitu vya Sh500 kama ilivyo kwa Watanzania wajasiriamali licha ya kuwa sera haitaki hivyo.
Profesa Mkumbo
Waziri Mkumbo anatarajia kufafanua zaidi kuhusu mashirika ya umma ambayo yameonekana mengi yana hali mbaya kulingana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Masauni huenda asiwe na kibarua kigumu kama wengine ingawa suala la mifuko ya plastiki ambayo inaonekana kuzalishwa huenda likamweka katika wakati mgumu.
Baadhi ya watu wanasema Masauni na wizara yake ni kama wameachia goli kwa kushindwa kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Serikali na sasa wanazidiwa kwa uwepo wa mifuko hiyo karibu kila mahali.
Kingine ni kero za Muungano zinazotajwa kuwa bado nne ambazo ni mgawo wa hisa kutoka sarafu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, mgawo wa faida kutoka Benki Kuu (BoT), uletaji wa sukari kutoka Kiwanda cha Mahonda katika soko la Tanzania Bara na matumizi ya magari kutoka Zanzibar katika ardhi ya Tanzania Bara.
Akizungumza kuhusu Hotuba hizo, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara Othman Dunga, amesema hakuna kitu kinachoweza kujadiliwa na kuleta matokeo chanya kwa wabunge kwani wengi wanaishi kwa kusifia.
Dunga ambaye aliwahi kuwa Katibu wa CCM katika Wilaya za Dodoma na Hanang’ amesema hotuba ya Utumishi na Utawala Bora ilipaswa kushambuliwa zaidi kwa kuwa imeleta picha ya nini kinatakiwa kwa wakati huu lakini akabashiri kuwa haitakuwa hivyo.
Aidha, amesema inachosha mbunge anaposimama anatumia dakika tano zote akiendelea kupongeza na kusifia halafu anakuja kutumia dakika mbili za kuomba miradi au ujenzi wa miundombinu jimboni kwake jambo linaloondoa ufanisi.
Katibu mstaafu wa CCM aliyehudumu katika baadhi ya mikoa nchi ambaye ameombwa jina lake lisitajwe, amesema hakuna jambo jipya ambalo Watanzania walitarajie zaidi ya kelele za kuonewa majimboni.
Mkongwe huyo katika siasa za Tanzania amesema mwaka wa uchaguzi huwa na utulivu kwa mawaziri kwani akili za watunga sheria huwa ziko majimboni kwao na kujipendekeza kwa baadhi ya mawaziri dakika za mwisho wakawasaidie kwenye miradi.