Askofu Sangu alivyomzungumzia Papa Francis

Shinyanga. Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Msinyori Liberatus Sangu ameeleza kwa masikitiko namna anavyomuenzi na kumkumbuka Papa Francis.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 21, 2025 katika Kanisa Kuu Parokia ya Mama mwenye huruma Ngokolo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga amesema kuwa, “Papa Francis ndiye alinifanya kuwa Msinyori (kufanya kazi iliyotukuka) baada ya kufanya naye kazi Roma ya kuhudumu katika kitengo cha uinjilishaji, alipendezwa na kazi yangu. Nimepokea msiba huu kwa masikitiko yenye furaha na ya kujaa matumaini.”

Pia, ametoa wito kwa waumini wote katika kipindi chote cha maombolezo akisema, “nawaomba waumini wote kuwa watulivu na kumuombea Papa wetu kwani amerudi katika nyumba ya baba katika kipindi cha ufufuko wa Yesu Kristo.”

Bendera ya Vatican ikiwa inapepea nusu mlingoti. Picha na Hellen Mdinda.

Baadhi ya waumini wa kanisa hilo Shinyanga wameeleza namna walivyopokea msiba huo na jinsi wa wanavyomkumbuka ikiwa ni pamoja na uteuzi wa Askofu Sangu kuja jimbo Shinyanga kuendeleza utume.

“Tunamkumbuka kwa kumteua Askofu Liberatus Sangu kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga mwaka 2015 kwa sasa ametimiza miaka 10 ya utume jimboni hapa,” amesema Anikazi Kumbemba.

Consolatha Kamuhabwa amesema kuwa, “nimepokea kwa masikitiko makubwa na msiba wa Papa na kwa upande mwingine namuona kama mtakatifu kweli kwa sababu ametuacha katika kipindi ambacho bado tunasherehekea ufufuko wa Yesu Kristo aliyekufa msalabani.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *