
Unguja. Kijana ambaye jina lake halijajulikana amefariki dunia na mwingine kupata majeraha makubwa baada ya kudaiwa kupigwa na shoti ya umeme, walipokuwa wakijaribu kuiba nyaya za umeme kwa kuzikata na msumeno.
Tukio hilo limetokea saa 8:32 usiku wa kuamkia leo Aprili 21, 2025 katika kituo kidogo cha umeme Mtoni Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo aliyejeruhiwa ni Awadh Ali mkazi wa Kilimahewa.
Akizungumza na Mwananchi Digital Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Abubakar Khamis Ally amekiri kutokea kwa tukio hilo.
“Ni kweli tukio hilo limetokea lakini kwa sasa bado nasubiri Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mjini Magharibi (RCO) anipe taarifa za kina halafu nitatoa taarifa baadaye,” amesema.
Akielezea tukio hilo Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), Haji Haji amesema limetokea Mtoni katika laini ya Fumba saa 8:32 usiku.
Amesema wakati linatokea tukio hilo mafundi wa Zeco walikuwa karibu na eneo hilo wakiendelea na matengenezo.
“Mafundi walikuwa wakijaribu kurejesha laini hiyo walisikia kishindo kikubwa ambapo walianza kufuatilia na kugundua kuna vijana wawili waliingia katika kituo hicho kwa nia ya kuiba nyaya,” amesema na kuongeza.
“Walikata waya wa umeme wenye msongo Kilovolt 33 kwa msumeno, kwa kuwa ulikuwa umeme mkubwa walipata shoti na kupata majeraha makubwa katika miili yao ambapo mmoja alifariki papo hapo na mwingine akiwa na hali mbaya, ambapo amepelekwa Hospitali ya Mnazimmoja,” amesema.
Amesema tukio hilo limesababisha maeneo mengi yanayohudumiwa na laini hiyo kukosa umeme ikiwa ni pamoja na Daraja Bovu, Amani, Mwanakwerekwe, Mpendae, Kwa Mchina, Mbuyumnene, Mombasa, Kisauni, Maungani, Kisasakasa Fuoni, Dimani, Bweleo Kombeni hadi Fumba.
Amesema maeneo hayo yatakosa umeme kwa takriban saa 10 zijazo wakati Zeco wakiendelea na jitihada za kurekebisha hali hiyo.
Hata hivyo, Haji amesema kazi hiyo inaweza kuchukua muda mrefu zaidi kutokana na hali ya hewa mvua zinazoendelea, hivyo kuomba radhi kwa wananchi kwani jambo hilo halikutegemewa.
Amewataka wananchi hususan vijana kutojiingiza kwenye matendo haya mbali na kuhatarisha maisha yao lakini yanaleta hasara kubwa katika miundombinu ya umeme na kuwafanya watu wengi waathirike bila sababu za msingi.
Kuhusu hasara ambayo imepatikana, Meneja huyo amesema kwa sasa hawawezi kujua lakini watu wengi wataathirika, kwani maeneo yote yatakayokosa nishati hiyo yana harakati nyingi za kiuchumi.