
Dar es Salaam. Wito wa viongozi wa dini kusisitiza maridhiano kwa viongozi wa vyama vya siasa kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, umeibua msukumo wa makundi mbalimbali katika jamii yakisisitiza kauli ya viongozi wa dini ni sauti ya umma.
Baadhi ya makundi hayo yamesisitiza yapo mambo yanapaswa kufanyiwa kazi kwani uwepo wa uchaguzi huru na haki wanaonufaika ni wananchi na sio vyama vya siasa.
Mitazamo hiyo inakuja wakati ambapo viongozi mbalimbali wa dini waliohubiri Aprili 21, 2025 kwenye Ibada ya Pasaka walitoa wito kwa Serikali na wadau kuhakikisha uchaguzi utakaofanyika Oktoba mwaka huu haupaswi kuwa chanzo cha migogoro, bali ni njia ya kupatikana viongozi wa haki, kweli na wazalendo.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Wolfgang Pisa alisema kabla ya Uchaguzi Mkuu Serikali ikae na wadau wote kuruhusu mabadiliko ya lazima.
Akizungumzia amani, Askofu Pisa alihoji nani anayeiharibu kati ya anayetumia nguvu kusisitiza uchaguzi uende anavyotaka na yule anayeshauri kukaa mezani kufanya mabadiliko ya mifumo.
Askofu Pisa ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alisisitiza wote waliokamatwa kwa kudai mageuzi ya mifumo ya uchaguzi waachiwe haraka na bila masharti, huku akisisitiza kukiwa na dhamira ya kweli, mabadiliko yanawezekana kabla ya uchaguzi,
Wakati Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo alisisitiza maridhiano, uchaguzi huru na haki na uamuzi wa wananchi katika uchaguzi kuheshimiwa.
Kufuatia kauli ya viongozi hao wa dini, makundi mbalimbali ya wananchi leo Jumatatu Aprili 21, 2025 wamezungumza na Mwananchi wakisisitiza yaliyoelezwa na viongozi hao wa kiroho yanahitaji kufanyiwa kazi.
Jicho la wachambuzi
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Dk Richard Mbunda amesema kauli ya viongozi wa dini ilitarajiwa na wasingeitoa wangeshangaza wengi.
“Walichosema viongozi hao ndio sauti ya umma, hatutaki kuona viongozi wa dini wakitoa waraka kwamba wananchi wasishiriki uchaguzi kwa sababu hautakuwa halali.”
“Viongozi wa dini ni sehemu ya jamii na wanafuatilia kila kitu kinachoendelea ndani ya nchi na wanajenga maoni inavyopaswa kuendeshwa,”amesema.
Dk Mbunda amesema kama viongozi hao wapo kwenye jamii na vitu vinavyofanyika haviendani na misingi ya utawala bora.
Mtazamo huo ni sawa na alichosema, Dk Paul Loisule kwamba kauli ya viongozi hao zimeonyesha namna jamii isivyokubaliana na kukamatwa kwa viongozi wa kisiasa.
“Viongozi wa dini wana wajibu wa kuisemea jamii wamesaidia kufikisha ujumbe na wasingesema wangekuwa wananyamazia matendo yasiyofaa, hivyo ni lazima kuyakemea kwa lugha inayofaa.
“Kinachoonekana chaguzi nyingi za Afrika bado zina shida zimetawaliwa na migogoro kuna haja ya kuangalia haya kwa jicho la kipekee,” amesema.
Kauli ya asasi za kiraia
“Viongozi wa dini wanawakilisha sauti ya wengi, wengi wetu tunataka amani, suala la kutunishiana misuli huyu anasema uchaguzi haupo mwingine anasema upo, sisi wananchi tunakosa amani,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria za Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga.
Kiongozi huyo, amesema amani haipotei tu kutokana na vita bali hata wasiwasi wanaoupata wananchi kwa yanayoendelea.
Henga amesema vyama vya siasa vinapaswa kuridhiana vinapokwenda kwenye uchaguzi kwani mvutano uliopo unawakosesha wananchi amani.
Kauli hiyo haitofautiani na alichosema Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa akieleza kilichozungumzwa na viongozi wa kiroho ni matumaini kwa Taifa.
“Tulishaonya Taifa linakwenda kwenye changamoto ya watu wote kukaa kimya na kunyamazia mambo ya kitaifa, suala la uchaguzi halipaswi kuwa la vyama vya upinzani hata miaka ya nyuma tulikuwa na uchaguzi pasipo kuwa na vyama.”
“Tunapaswa kuwa pamoja kama Taifa bila kujali itikadi mahali ambapo tunaona hoja za kitaifa zinachukua muda mrefu kufanyiwa kazi,” amesema.
Ole Ngurumwa amesema suala la maboresho ya mifumo ya uchaguzi ni la muda mrefu hivyo ni kosa kuifanya Chadema pekee ndio ionekane wahitaji wakubwa wa mabadiliko, badala yake liwe takwa la wananchi.
Makundi ya wafanyakazi
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tamstoa), Chuki Shabani akitoa maoni yake amesema kauli ya viongozi wa kiroho ni sahihi kwani Taifa linapoelekea linahitaji maridhiano.
“Wanasiasa kukamatana si jambo sahihi wabishane kwa hoja, wanapokosoana na kazi ikafanyika sisi wananchi ndio tunaonufaika, kuwe na usawa kwenye siasa kusiwe na kundi ambalo wao wanaonekana wanakosea tu kundi lingine halikosei,” amesema.
Chuki amesema ni jambo la msingi viongozi kuaminiana na kuwatumikia wananchi bila kutengenezeana uadui, kwani wanachotaka wananchi ni maendeleo, hivyo maridhiano ni muhimu,” amesema.
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi Mashambani na Kilimo Tanzania (TPAWU), John Vahaya amesisitiza Serikali kuangalia mfumo utakaoleta viongozi bora kwa masilahi ya wananchi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Mrida Mshota amesema anaungana na viongozi uchaguzi mkuu uwe huru na haki, lakini suala la waliokamatwa kuachiwa bila masharti hawezi kulizungumzia kwa kuwa sio mwanasiasa.
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu amesema chama hicho kinaunga mkono wito uliotolewa na Pisa kuwa wanasiasa walioshtakiwa kwa kutetea haki ikiwemo Tundu Lissu, kuachiwa huru bila masharti yoyote na kusitokee kukamatwa kwa wanasiasa wengine kwa sababu ya kudai mageuzi nchini.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Husna Mohamed Abdallah amesema kilichosemwa na viongozi wa dini, kinafanana na maoni ya chama hicho, ambayo wamekuwa wakiyatoa mara kwa mara kwamba viongozi waliokamatwa kuachiwa huru kwa sababu ni haki za binadamu.
“Kipindi hiki tunaelekea kwenye uchaguzi tutapata tafsiri mbaya katika jamii, kwa sababu makosa hayohayo yangefanyika wakati mwingine ni tofauti na yakifanyike nyakati hizi. Inawezekana jamii ikaona ni hujuma dhidi ya uchaguzi.”
“Miaka yote CUF tumedai uchaguzi uwe huru na haki,” amesisitiza Husna.
“Kusema watu waliokamatwa kuachiwa huru ni kuingilia uhuru wa Mahakama, haiwezekani mtu achiwe bila masharti wakati yupo katika vyombo vya dola,” amesema Hassan Doyo ambaye ni Katibu Mkuu wa NLD.
Maelezo ya Doyo yalishaibiana na Juma Ali Khatib ambaye ni Mwenyekiti wa Ada Tadea aliyesema jambo lolote likifika mahakamani, hakuna mtu mwenye uwezo wa kuingilia bali mhimili huo, hivyo uachwe ufanye kazi zake.
Wanahabari
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema kwa hali yoyote Tanzania inastahili kufanya uchaguzi huru na haki, lakini sio kurudi michezo iliyofanyika huko nyuma ikiwemo mawakala kukataliwa kuapishwa.
“Lakini wanasiasa wanapaswa kujua madhara ya kauli wanazozitoa, kusimama na kutoa kauli ngumu ambayo sheria inazuia, unakuwa umejiandaa watu watumie sheria halafu ionekane umeonewa. Hii sio kwa upinzani pekee, bali hata chama tawala CCM,” amesema Balile.