
Urusi imerejelea mashambulizi ya anga dhidi ya Ukraine baada ya kumalizika kwa muda wa usitishwaji vita kwa ajili ya Jumapili ya Pasaka wa saa 30, jeshi la Urusi na maafisa wa Ukraine wametangaza Jumatatu, usitishaji mapigano ambao pande zote mbili zimelaumiana kwa kukiuka.
Imechapishwa:
Dakika 3
Matangazo ya kibiashara
Wakati huo huo, Rais wa Marekani Donald Trump amesema anatumai “makubaliano” ndani ya wiki hii kati ya Kyiv na Moscow, ambayo imekuwa ikivamia jirani yake Ukraine kwa miaka mitatu, vita ambavyo vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu.
Huko Kyiv, ambapo tahadhari ya uvamizi wa anga ilidumu saa moja alfajiri siku ya Jumatatu kutokana na “tishio kutoka kwa ndege zisizo na rubani,” raia wa Ukraine waliohojiwa na shitika la habari la AFP wamesema wameshangazwa na kufarijiwa na kipindi hiki kifupi cha usitishwaji vita lakini hawakuamini uwezekano wa kusitishwa kwa mapigano ya kudumu.
“Ilikuwa vyema” “kupumzika, hata ikiwa ni kwa siku moja tu” kwa sababu “watu wamechoka,” Viktor Danyltchouk, mwanajeshi aliye likizoni, ameliambia shirika la habari la AFP.
Hata hivyo, amesema kuwa makubaliano ya haraka na Urusi “haiwezekani” kufikiwa kwa sababu “adui anaendelea kushambulia.”
Mazungumzo ya kidiplomasia yaliyoanzishwa na utawala wa Marekani kumaliza mzozo huo yamekuwa yakiendelea kwa muda wa miezi miwili, bila matokeo madhubuti.
Katika ripoti yake ya kila siku, Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema siku ya Jumatatu kwamba imefanya mashambulizi ya anga, ndege zisizo na rubani, na mizinga kwenye maeneo 74 ya kijeshi nchini Ukraine baada ya “kumalizika kwa kipindi cha usitishaji vita.”
– Kupungua kwa kasi ya mapigano –
Hapo awali, magavana wa mikoa ya Ukraine ya Dnipropetrovsk (kati-mashariki), Mykolaiv (kusini) na Cherkasy (katikati) walitangaza kwamba mashambulizi ya anga ya Urusi yalifanyika katika mikoa yao, bila kuripoti majeraha yoyote.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambaye alikubali makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotangazwa na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin, alihakikisha Jumapili jioni kwamba vikosi vya Urusi vimekiuka usitishaji vita “zaidi ya mara 2,000” wakati wa mchana, huku akisisitiza, hata hivyo, kwamba hawakufanya mashambulizi yoyote ya anga katika kipindi hiki.
Pia amependekeza kuongezwa kwa siku 30 kwa makubaliano ya kusitisha mapigano dhidi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya masafa marefu dhidi ya miundombinu ya kiraia.
Wanajeshi kadhaa wa Ukraine waliotumwa katika maeneo mbalimbali vita wameliambia shirika la habari laAFP kwamba kumekuwa na kupungua kwa kiwango kikubwa cha mashambulizi ya Urusi katika maeneo yao siku ya Jumapili, ingawa hayajakoma kabisa.
Kwa upande wa Urusi, Wizara ya Ulinzi imeripoti majaribio yasiyofanikiwa ya askari wa Ukraine “kushambulia ngome za Urusi” katika maeneo kadhaa ya mkoa wa Ukraine wa Donetsk (mashariki).
Mamlaka ya Urusi pia imetaja hatua za kijeshi za Ukraine dhidi ya mikoa ya mpaka ya Urusi ya Bryansk, Kursk na Belgorod, ambapo “raia waliuawa au kujeruhiwa.”
– Mazungumzo katika mgogoro –
Alipoulizwa kuhusu kauli hizi, Dmitry Peskov alisema Jumatatu kwamba Kremlin inatumai kwamba “kufanya kazi na upande wa Amerika” kutafuta suluhisho la mzozo kungeleta “matokeo,” lakini hakutoa maelezo juu ya mazungumzo yanayowezekana wiki hii.
Siku ya Ijumaa, Bw. Trump badala yake alitishia kujiondoa katika mazungumzo hayo, kwa kukosekana maendeleo ya haraka katika majadiliano tofauti ambayo wajumbe wake wamekuwa wakifanya kwa wiki kadhaa na Kyiv na Moscow.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China Guo Jiakun kwa upande wake amekaribisha siku ya Jumatatu “juhudi zote zitakazopelekea kusitishwa kwa mapigano, hatua muhimu kuelekea kupatikana kwa amani” nchini Ukraine.
Ingawa nguvu ya mapigano imepungua kwa muda mfupi, shutuma za mtambuka zinaonyesha ugumu wa kuweka hata usitishaji vita wa muda mfupi katika mzozo huu mbaya zaidi wa silaha huko Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia.
Jaribio la kusitisha mapigano tayari limefanyika mara mbili, mnamo Aprili 2022 na Januari 2023, lakini yalishindwa kwa sababu ya kukataa kwa Moscow kwa mara ya kwanza na Kyiv kwa mara ya pili kunyamazisha silaha zao.
Hivi majuzi, mnamo mwezi Machi, Washington ilipendekeza usitishaji mapigano wa siku 30 bila masharti, toleo lililokubaliwa na Kyiv lakini lilikataliwa na Moscow.