Moto wa Jonathan Sowah si mchezo Bara

MABAO mawili aliyofunga mshambuliaji wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah katika ushindi wa timu hiyo wa 3-0 dhidi ya Tabora United, yamemfanya kutishia upya ufalme wa washambuliaji wa Yanga, Prince Dube na Clement Mzize kwenye vita ya ufungaji.

Mshambuliaji huyo raia wa Ghana, tangu ajiunge na kikosi hicho dirisha dogo la Januari mwaka huu, amefunga mabao 11 kupitia mechi 11 za Ligi Kuu akilingana sawa na Clement Mzize akizidiwa bao moja na Prince Dube na nyota wa Simba, Jean Charles Ahoua waliofunga 12 kila mmoja.

Akizungumzia kiwango chake baada ya mchezo huo, Sowah alisema ushirikiano anaoupata kutoka kwa wachezaji wenzake ndio silaha kubwa ya hiki anachokionyesha, huku akipongeza benchi la ufundi kwa imani kubwa wanayompa tangu amejiunga nao.

“Unapoletwa katika timu kubwa na yenye malengo makubwa ni lazima uonyeshe kiu ya kupambana, kwangu ni jambo nzuri kuona naendeleza kiwango bora hadi kufikia sasa, pia naamini tutafikia kule tunapohitaji kwa ushirikiano huu,” alisema Sowah, aliyeshindwa kufunga katika mechi mbili tu, ikiwamo ile waliopoteza 2-0 mbele ya KMC na walipoishinda Azam bao 1-0 likifungwa na Elvis Rupia.

Kaimu kocha mkuu wa Singida BS, David Ouma alisema usajili wa nyota huyo umeleta manufaa makubwa katika timu, kwani kila mmoja wao kwa sasa anaonyesha ushindani, jambo ambalo wao kama benchi la ufundi wanalifurahia.

Nyota huyo aliyejiunga na Singida akitokea Al-Nasr Benghazi FC ya Libya aliyoitumikia kwa miezi sita, alionyesha kiwango kizuri pia kwani alihusika na mabao saba ya kikosi hicho, baada ya kufunga matano na kuasisti mawili kwenye mechi tisa.

Sowah alijiunga na Al-Nasr Benghazi Januari 27, 2024, akitokea Medeama ya kwao Ghana ambapo pia alionyesha kiwango bora na kuzivutia klabu mbalimbali ikiwemo Yanga baada ya kuwasumbua katika Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya makundi.

Akiwa na Medeama aliyojiunga nayo Januari 11, 2023, akitokea Danbort FC, alicheza michezo 20 ya Ligi Kuu ya Ghana ambapo alifunga mabao 16, huku katika Ligi ya Mabingwa Afrika, alifunga matatu kwenye mechi saba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *