Julio akwepa Play-Off Kiluvya United

KOCHA wa Kiluvya United, Julio Elieza amesema hataki kuiona timu hiyo ikiwa katika presha ya kumaliza katika nafasi ya kucheza mtoano (play-offs), ingawa malengo aliyopewa ni kuhakikisha kikosi hicho kinabakia Ligi ya Championship kwa msimu ujao.

Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Julio alisema gepu la pointi lililopo na washindani wao waliokuwa chini linaonyesha hawako sehemu salama, hivyo jitihada zinahitajika ili kukinusuru kikosi hicho na janga la kushuka daraja.

“Kuanzia timu iliyopo nafasi ya 16 hadi sisi tuliyopo ya 12 haitupi jeuri ya kuamini tumejihakikishia kubaki msimu ujao, jitihada zaidi zinahitajika kwa sababu hatutaki hata kucheza michezo ya ‘play-off’, ili kuondoa presha,” alisema Julio.

Kocha huyo wa zamani wa Lipuli FC ya Iringa, ni wa tatu kuifundisha timu hiyo msimu huu baada ya awali kuanza na Twaha Beimbaya aliyetimuliwa kutokana na mwenendo mbaya, kisha kufundishwa na Zulkifri Iddi ‘Mahdi’ aliyeondoka pia kikosini.

Kiluvya iliyopanda Ligi ya Championship msimu huu, baada ya mchezo wa jana dhidi ya TMA FC ulioisha kwa sare ya bao 1-1, imecheza michezo 26, ambapo kati ya hiyo imeshinda sita, sare mitatu na kupoteza 18, ikiwa nafasi ya 12 na pointi 21, ikifunga mabao 18 na kuruhusu 39.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *