Waliofariki ajalini Iringa kuagwa kesho

Mafinga. Miili ya watu sita kati ya saba waliofariki dunia katika ajali ya gari la kubebea wagonjwa lililogongana na pikipiki ya magurudumu matatu, maarufu ‘Guta’ inatarajiwa kuagwa kesho Jumatatu Aprili 21, 2025.

Inaagwa miili sita, kwa sababu mmoja tayari umeshatambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zake.

Ajali hiyo ilitokea Aprili 19, 2025, saa 12:30 asubuhi katika eneo la Luganga Barabara ya Mafinga-Mgololo katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.

Mbali na watu saba waliopoteza maisha, wengine 15 walijeruhiwa na kati yao, wanne wakipewa rufaa kwenda Hospitali ya Mkoa wa Iringa kwa matibabu zaidi.

Akizungumza na Mwananchi  leo, Jumapili Aprili 20, 2025 Diwani wa Upendo ilipotokea ajali hiyo, Michael Msite amesema miili ya watu sita itaagwa kesho katika Shule ya Msingi Upendo.

“Miili ya wapendwa wetu tunatarajia kuiaga kesho katika Shule ya Msingi Upendo. Kwa sasa (ilikuwa mchana) tunaendelea na taratibu nyingine kama kufunga matenti pamoja na mambo mengine,” amesema.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Mufindi, Dk victor Msafiri amesema majeruhi wote waliokuwa wanatibiwa hospitalini hapo wanaendelea vizuri.

“Majeruhi waliopo wanaendelea vizuri na hali zao zinaendelea kuimarika,” amesema.

Amewataja waliofariki dunia ni Latifa Joseph Angela (18), Irene Msanga (55), Siamini Lukosi, Jema Mbwilo (50), Rukia Kasavaga(52), Jenipha Msigwa 42 na Anord Mbosso.

Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Meloe Buzema amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari la wagonjwa kwenda mwendokasi bila sababu.

Amelitaja jina moja la dereva huyo ni Moses na kwamba baada ya ajali alikimbia na anaendelea kutafutwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *