Utitiri wa malori janga kwa barabara

Dar es Salaam. Ingawa kuharibika mara kwa mara kwa miundombinu ya barabara kunachochewa na sababu nyingi, kukosekana udhibiti wa malori ya mizigo yanayopita kwenye barabara hizo inatajwa kuwa sababu kuu.

Kwa mujibu wa wadau wa miundombinu hiyo, barabara hujengwa kwa kuzingatia aina na uzito wa vyombo vya usafiri vinavyokusudiwa kupita na kitendo cha kuruhusu lori kunapunguza uhai wa barabara husika.

Wadau hao wamekwenda mbali zaidi na kueleza kuachwa holela kwa malori, mbali na kusababisha uharibifu wa miundombinu hiyo, pia ni chachu ya ajali na hasara kwa Serikali.

Katika siku za karibuni, lilishuhudiwa lori lililogonga kituo kipya cha mabasi ya mwendokasi (BRT) jijini Dar es Salaam.

Serikali imetenga Sh301.72 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa barabara na madaraja iliyoathirika na mvua na mafuriko kati ya Juni 2023 hadi Aprili 2024.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi, Zainab Katimba, bajeti hiyo itagharamia ukarabati wa kilomita 1,742.19 za barabara, makaravati 4,260, madaraja 319 na mifereji yenye urefu wa mita 108,833 iliyoharibiwa na mvua hizo.

Ingawa si uharibifu wote unasababishwa na malori, wataalamu wa usafiri wanasema magari hayo huchangia kuchakaza miundombinu, hasa barabara ambazo hazikujengwa kwa ajili ya kuhimili uzito mkubwa.

Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri Barabarani kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Johansen Kahatano, anasema ongezeko la shughuli za usafirishaji mizigo, hasa jijini Dar es Salaam, limechochewa na uboreshaji wa ufanisi katika bandari.

“Hii imesababisha mizigo kuongezeka na hivyo kuhitajika kwa malori zaidi ya kuisafirisha kuelekea mikoa mingine na nchi jirani,” anasema Kahatano.

Hata hivyo, anaonesha matumaini ya kupungua kwa tatizo hilo baada ya kukamilika kwa bandari kavu ya Kwala akisema: “Mara bandari ya Kwala itakapoanza kazi rasmi, mizigo mingi haitalazimika kupita katikati ya jiji.”

“Hii itapunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya malori kwenye barabara zetu za mijini, na hivyo kupunguza uharibifu wa barabara na msongamano wa magari,” anasema.

Anaongeza hata kwa sasa, katika maeneo yenye msongamano mkubwa kama bandarini, kuna mfumo wa foleni unaosaidia kupangilia malori kwa wakati ili yasilete msongamano usio wa lazima.

“Tunaendelea kuimarisha mifumo hii ya upangiliaji ili kuhakikisha usalama na ufanisi wa barabara za jiji,” anasema.

Walichokisema Tanroads, Tatoa

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mohamed Besta anasema sheria iko wazi kuhusu uwajibikaji pale miundombinu inapoharibiwa.

“Mtu yeyote anayesababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara, na ikathibitika, sheria itachukua mkondo wake. Tuna taratibu za kufuatilia na kurejesha gharama, hakuna anayepaswa kuwa juu ya sheria,” anasema.

Anasema Tanroads kwa kushirikiana na polisi na halmashauri za jiji, wanaendelea kufuatilia na kuchukua hatua stahiki, lakini akasisitiza kuzuia ni bora kuliko kutibu.

“Hizi ni barabara zetu sote. Ni wajibu wetu kuzilinda kwa ajili ya ustawi wa uchumi wa taifa letu,” alisema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Rahim Dossa anasema changamoto zinazoikumba sekta ya usafirishaji mizigo jijini Dar es Salaam ni kubwa kutokana na namna jiji lilivyopangwa.

“Dar es Salaam imekuwa na changamoto kubwa za kimuundo. Hii inatufanya kazi yetu kuwa ngumu, lakini tunatarajia maboresho yaendelee kufanyika. Tunasubiri kwa matumaini kuwa siku moja hatutalaumiwa tena kwa hali hii, kwa sababu mazingira yatakuwa bora kwa kazi yetu,” anasema Dossa.

Mhandisi mwandamizi kutoka kampuni ya ushauri wa barabara jijini Dar es Salaam ambaye hakutaka kutajwa jina, anasema kuruhusu malori kuingia katikati ya jiji kunasababisha uchakavu wa mapema wa barabara, hasa kwenye maeneo kama Ilala, Temeke na Kinondoni ambazo zilibuniwa kwa magari mepesi.

“Maisha ya barabara yamekuwa mafupi. Tunashuhudia nyufa, mashimo na kuharibika kwa uso wa barabara ndani ya miaka michache tu baada ya ukarabati, jambo ambalo si la kawaida,” anasema.

Anaongeza kuwa  hata miundombinu mipya haiko salama. “Vituo vya mwendokasi na njia zake maalumu vililenga kuboresha usafiri wa umma, lakini sasa vinaharibiwa na malori, hasa nyakati za usiku.”

Madereva teksi

Madereva wa teksi wanaofanya kazi ndani ya jiji wanasema wao ndio wanaoathirika zaidi. Dereva wa teksi anayetumia njia ya Mwenge hadi Posta, Apolinary Kitea, anasema malori husababisha ucheleweshaji, huziba njia wanapogeuza au kupakia na kushusha mizigo, na mara nyingi huendesha bila kujali magari madogo.

“Mara nyingine tunalazimika kusimama kwa dakika 10 hadi 15 kwa sababu lori limeziba barabara Kariakoo au Samora Avenue. Likiharibika, hakuna anayekuja kuliondoa kwa haraka. Huo ni muda na mafuta vilivyopotea maana yake ni hasara,” anasema Kitea.

Dereva mwingine, Emmanuel Mgimba anayefanya kazi kati ya Buguruni na Tazara, anasimulia jinsi alivyonusurika ajali mara mbili kutokana na lori za mizigo wakati wa mvua.

“Ni kama tunagawana jiji na majengo yanayotembea. Yakianza kuingia kwa wingi, hatuwezi hata kupumua,” anasema.

Lakini madereva wa malori nao wanasema mazingira ya jiji hayawapi uchaguzi. Dereva wa kampuni ya usafirishaji iliyopo Goba, Idd Nchimbi, anasema ratiba zao za utoaji mizigo huamuliwa na saa za bandari na maghala, ambazo haziendani na sheria za jiji.

“Wateja wengi hutaka mizigo yao ifikishwe kwa wakati maalum, na wakati mwingine inatulazimu kuingia jiji wakati wa zuio. Kama miundombinu ingekuwa bora na kuna vituo vya malori nje ya jiji, tungeshika sheria,” anasema.

Dereva mwingine, Joel Masimango, anasema ukosefu wa maeneo rasmi ya kushusha mizigo kunawalazimisha kupita barabara za katikati.

“Hatupiti kwenye hizo barabara kwa sababu tunapenda, bali kwa sababu hakuna mfumo mzuri wa kutuongoza. Ukichelewa kufikisha mzigo kwa mteja kwa sababu ulikaa nje ya jiji, unakumbana na adhabu kazini,” anasema.

“Kuna dhana potofu kuwa tuna faida kwa kuvunja sheria, lakini kila mara lori linapoharibu barabara au kuchelewesha mzigo, tunapata hasara,” anaongeza.

Kwa upande mwingine, mtaalamu wa mipango miji kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi, Dkt Gerald Kigoa, anasema Dar es Salaam haijaweza kuendana na kasi ya ongezeko la mizigo linalotokana na ukuaji wa uchumi.

“Unapokuwa na jiji linalokua haraka kuliko mipango, malori yatafuata mizigo mahali popote ilipo. Huwezi kuwa na bandari kubwa ya uingizaji mizigo kama Dar es Salaam na usitarajie msongamano wa malori, lakini tatizo ni kwamba tunatibu dalili badala ya kujenga mfumo,” anasema.

Dk Kigoa anapendekeza kuundwa kwa sera ya jiji kuhusu usafirishaji mizigo, itakayoweka njia maalumu za malori, muda maalumu wa kuwasilisha mizigo na maeneo rasmi ya kushushia mizigo, sambamba na uwekezaji kwenye barabara za mzunguko na vituo vya malori nje ya jiji.

Maoni hayo, yaliungwa mkono na mtaalamu wa usafiri kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Adam Mussa anayesema, “Serikali inatumia mabilioni kurekebisha barabara, lakini malori yanaziharibu kwa kasi kuliko tunavyoweza kuzitengeneza. Ni mtego wa kisera.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *