Constant Mutamba aagiza kesi za kisheria zichukuliwe dhidi ya Joseph Kabila na washirika wake

Waziri wa Sheria wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Constant Mutamba, ameamuru siku ya Jumamosi, Aprili 19, 2025, kufunguliwa kwa kesi za kisheria dhidi ya Joseph Kabila, rais wa zamani wa nchi hiyo, na pia dhidi ya washirika wake, wanaoshukiwa kuunga mkono kundi la waasi la AFC/M23, linaloungwa mkono na jeshi la Rwanda.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa yake rasmi, Waziri huyo amemuagiza Mkaguzi Mkuu wa Majeshi ya DRC (FARDC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzisha kesi dhidi ya kiongozi huyo wa zamani wa nchi ambaye aliongoza DRC kwa miaka 18. Hata hivyo, ameagiza kukamatwa kwa mali zote zinazohamishika na zisizohamishika za Seneta wa Maisha Joseph Kabila.

Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa hatua za kuzuia harakati zimechukuliwa dhidi ya wanachama na maafisa wote wa chama cha PPRD, chama cha Joseph Kabila, wanaohusika katika suala hili, ambalo limeelezwa kuwa ni uhaini mkubwa dhidi ya taifa. Hatua hizi zinalenga kuzuia jaribio lolote la kuvuja au kuficha ushahidi.

Uamuzi huu unakuja huku kukiwa na mzozo unaoendelea wa usalama mashariki mwa nchi hiyo, ambapo waasi kutoka Muungano wa Mto Kongo (AFC) na Vuguvugu la Machi 23 (M23), linaloungwa mkono na Rwanda, wanaendesha mashambulizi ya silaha dhidi ya vikosi vya serikali, na kusababisha maelfu ya vifo na mamilioni ya watu kukimbia makazi yao. Joseph Kabila anatuhumiwa kushiriki moja kwa moja katika uvamizi huu, ambao unajumuisha, kulingana na serikali, ukiukaji mkubwa wa uhuru wa kitaifa.

Kusitishwa kwa shughuli za PPRD

Wakati huohuo, serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imetangaza kusitisha shughuli za Chama cha Wananchi kwa ajili ya Ujenzi na Maendeleo (PPRD) nchini kote, ambacho Joseph Kabila ndiye mwenye mamlaka ya kimaadili na hivyo kuongeza shinikizo la kisiasa kwa rais huyo wa zamani na washirika wake. Wiki chache zilizopita, maafisa kadhaa wakuu wa chama hiki walihojiwa na mahakama.

Katika taarifa nyingine iliyotolewa siku ya Jumamosi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Jacquemain Shabani, amelaani “ukimya kamili” wa PPRD katika kukabiliana na uvamizi wa Rwanda mashariki mwa nchi hiyo na harakati za mamlaka yake ya kimaadili katika vita vinavyoendelea.

Mnamo Aprili 18, Joseph Kabila, rais wa heshima na seneta, aliwasili Goma, katika mkoa wa Kivu Kaskazini, uliochini ya udhibiti wa waasi wa AFC/M23. Akishutumiwa na serikali kuwaunga mkono waasi, alihalalisha kurejea kwake kwa haja ya kuchangia katika kutafuta suluhu la mzozo wa usalama. Katika barua aliyoiandikia Jeune Afrique mnamo Aprili 8, alisema kwamba alitaka kurejea “bila kuchelewa” DRC baada ya miaka sita ya ukimya, mwaka wa uhamishoni, na katika kukabiliana na hali mbaya ya usalama.

Katika kambi ya rais Tshisekedi wanaona kurudi huku kama dhibitisho la ushirikiano wake na waasi, wakati PPRD inalaani shutuma za kisiasa zisizo na msingi zinazolenga kuficha kushindwa kwa serikali ya sasa.

Msemaji wa serikali Patrick Muyaya alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Lubumbashi (Haut-Katanga) Jumamosi asubuhi, Aprili 19, kwamba safari ya rais huyo wa zamani inazua maswali na kwamba ni muhimu kusubiri matokeo ya kurejea kwake ili kutathmini athari zake:

“Tunasubiri kuona, tunasubiri kusikiliza, kwa sababu labda hatupaswi kudhani baadhi ya mambo. Lakini hapa, lazima kwanza tujue kwamba Rais wa Jamhuri alizungumzia suala hili. Alisema kuwa rais, mtangulizi wake, ana uhusiano na AFC kwa miezi kadhaa. Sasa ameamua kurudi, sina uthibitisho bado, tutaona kitakachosemwa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *