Moshi. Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo amesisitiza maridhiano, uchaguzi huru na haki na uamuzi wa wananchi katika uchaguzi kuheshimiwa.
Mbali na hayo, amewataka polisi kuepuka kutumiwa vibaya na watu wasioitakia mema nchi na Watanzania kupenda nchi yao, wakiwa na hofu ya Mungu ili Tanzania iwe mahali salama.
Askofu Shoo amesema hayo leo Aprili 20, 2025 akitoa ujumbe wa Pasaka katika Kanisa Kuu, Usharika wa Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro.
Akizungumzia maridhiano, Dk Shoo amesema yanapaswa kuingia katika matendo na si kubaki kuwa maneno.
“Tunasikia habari za mapigano, migogoro kila mahali kati ya makundi, kati ya nchi na kati ya mtu na mtu, tunasikia habari za ukatili na uonevu kwa wasio na nguvu na mamlaka, mahali pengine inaelekea kushamiri tena hata hapa kwetu,” amesema.

Askofu Fredrick Shoo akizungumza katika ibada ya Pasaka, Kanisa kuu, usharika wa Moshi mjini, mkoani Kilimanjaro
Amesema kunahitajika kupatana, kuridhiana na kupendana.
“Tunaposema juu ya upatanisho tunamaanisha, tunaposema juu ya kuridhiana tunamaanisha, tunaposema juu ya kujenga upya, kuleta mabadiliko yatakayofanya watu wote waweze kuishi kwa amani na haki itendeke na kuletea nchi yetu maendeleo tunamaanisha. Tunapozungumza kuhusu ustahimilivu siyo maneno maneno tu, bali sisi kwa nguvu ya ufufuko wa Yesu Kristo tunakuwa vyombo na wajumbe wa mambo haya,” amesema.
Dk Shoo amesema siyo vyema kwa Mkristo kukaa kimya au kukaa pembeni pale anapoona mambo yanayotishia amani, uzima, furaha na kuondoa haki kwa wale ambao wanastahili, badala yake wanahitajika kujitokeza wazi kushuhudia kwa ujasiri kuwa Mungu ni Mungu wa uhai anayekataa ukatili wa kila namna.
“Tujitokeze kwa sauti moja kutangaza hii nguvu ya ufufuo, tuseme ukweli pale inapopasa kusema ukweli na hata kwa mamlaka zote tuchukue hatua ya pamoja kutetea haki, amani na upatanisho. Kwa pamoja tukatae nguvu, mamlaka zozote zinazosababisha mateso, zinazoleta na kukumbatia vifo,” amesema.
Kuhusu uchaguzi mkuu amesema ni haki na wajibu wa raia kujichagulia viongozi wanaowataka, akionya wananchi wasiingiliwe wala kuzuiwa kuwachagua viongozi wawapendao.
“Huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu, ni wajibu wetu kuchagua viongozi bora. Ni haki yetu kuona tunapata viongozi ambao kweli watatupeleka mbele kama nchi na watajali masilahi ya nchi hii, wananchi na kizazi cha sasa na hata kizazi cha baadaye,” amesema. “Tunaomba uchaguzi huu usifanane na chaguzi zilizopita, ule wa 2019, 2020 na huu uliofanyika mwaka jana. Tumerudia mara nyingi na mahali pengi, hatutaki kuona yale yaliyotokea katika chaguzi hizi nilizotaja yakijirudia.”
Polisi na uchaguzi
Dk Shoo amelitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha hawatumiki vibaya katika uchaguzi kwa masilahi ya watu wachache.
“Polisi tunawapenda na tunawategemea kwa jambo la ulinzi na usalana wa watu na mali zao. Niwaombe katika uchaguzi huu mkuu kila mmoja kwa nafasi yake aangalie na asikubali kutumiwa vibaya kwa masilahi ya watu ambao hawaitakii nchi hii mema. Polisi nawaomba kipekee kabisa, msikubali kutumika vibaya na mfahamu wajibu wenu na Mungu awasaidie,” amesema.
Pia, amewataka Watanzania kuipenda nchi yao na kila mmoja kwa nafasi yake ajitoe kuona Tanzania inakuwa mahali salama ambako kila mtu atakaa kuifurahia na kujivunia kwamba tunayo nchi nzuri.
Akizungumza katika ibada hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava amesema uongozi ni utumishi na utumishi ni kwa ajili ya watu, akiwataka Watanzania wote katika eneo lolote walilopo kujitoa kwa ajili ya wengine.
“Kuteswa kwa Bwana wetu Yesu Kristo na kufa kwake ni kwamba maisha yetu wakati mwingine yanapaswa yawe kwa faida ya wengine na kutanguliza wengine bila kutazama nafsi zetu sisi wenyewe na mambo yetu sisi wenyewe.
“Ikiwa ni katika eneo lolote lile, kwenye utumishi wa umma, utumishi kwenye sekta binafsi, kwenye familia, popote pale ulipo, wakati mwingine ni bora kuwasaidia wengine bila kujitanguliza wewe na ndivyo bwana wetu Yesu Kristo alifanya kwa gharama ya kutoa hata nafsi yake na uhai wake kwa ajili ya kutukomboa sisi sote. Hivyo tunapoendelea kutafakari ukuu wa Yesu Kristo nasi pia tuende kwa mtazamo huo,” amesema.