Dar es Salaam. Askofu wa Jimbo Katoliki teule la Bagamoyo, Stephano Musomba amesema kila muamini anapaswa kuwa mmishionari katika kutangaza mema na ukuu wa Mungu.
Sambamba na hilo, amesisitiza kutoacha aina ya maisha Wakristo Wakatoliki waliyaishi katika kipindi chote cha mfungo wa Kwaresma.
Amesema hayo wakati akihubiri katika ibada ya mkesha wa Sikukuu ya Pasaka iliyofanyika usiku wa kuamkia leo Jumapili Aprili 20, 2025, kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph lililopo Posta Dar es Salaam.

“Kama tulivyosafiri na sala, kufunga, kutoa sadaka na matendo ya huruma katika kipindi cha Kwaresima vivyo hivyo tuenende hata sasa,” amesisitiza.
Amesema neno la Mungu linamkumbusha mwanadamu ni nani ili asiweze kujisahau katika maisha yake. Bali aishi katika upendo, wema na kujaliana.
“Pamoja na udhaifu wetu bado Mungu anatupenda. Hivyo nasi tunapaswa kuenenda katika njia zile zinazompendeza,” amesema.
Aidha, amesema adhimisho la Pasaka linapaswa kuona na hata kusikia yale yote yaliyo ya Mungu.
Katika kusisitiza na kuwatia moyo waamini amesema kila kukicha ni kurasa mpya ya maisha hivyo mmoja anapaswa kutokata tamaa.

Aidha, kila mmoja anapaswa kijitafakari upya matendo na mwenendo wake. Amesema jambo kubwa la kufanya katika kipindi hiki ni kuwa wapya kama Yesu alivyofufuka na kuwa mpya.
Amewataka kuishi katika imani, kama neno la Mungu linavyoelekeza: “Mmekuwa viumbe wapya katika Kristo ishini vyema nyote ndivyo Mungu anavyotaka tuishi.”