Rais TEC: Serikali ikae na wadau wa uchaguzi, waliokamatwa waachiwe

Dar es Salaam. Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Wolfgang Pisa, amesema ni muhimu Serikali kukaa na wadau wa uchaguzi, kuruhusu mabadiliko ya lazima kabla ya uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.

Askofu Pisa, ambaye pia ni rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), amesisitiza umuhimu wa amani kuelekea uchaguzi huo, akitaka wote waliokamatwa kwa kudai mageuzi ya mifumo ya uchaguzi waachiwe haraka na bila masharti.

Wito wa Askofu Pisa kuhusu  kuachiwa kwa viongozi waliokamatwa unashabihiana na wa wadau wa haki, wanaoshinikiza kuachiwa huru kwa Mwenyekiti wa Chadema (Taifa), Tundu Lissu aliyekamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini.

Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025 alipokuwa ziarani kuhamasisha ajenda ya No reforms, no election wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma. Alihamishiwa kituo kikuu cha Polisi Dar es Salaam, baadaye akafikishwa mahakamani.

Askofu Pisa ametoa wito huo usiku wa kuamkia leo Jumapili Aprili 20, 2025 katika mahubiri ya misa ya mkesha wa Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Andrea Kaggwa, mkoani Lindi.

Moja kati ya mapendekezo yake manne kuelekea uchaguzi, Askofu Pisa amesema wahusika wakae na wadau wote kuruhusu mabadiliko ya lazima kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Amesema sauti na vilio vya wengi vinapaswa kusikika akisisitiza: “Kasoro zilizojitokeza zinapaswa kurekebishwa haraka. Kukiwa na nia ya dhati kutoka kwa wahusika muda unatosha kabisa kufanya hayo marekebisho kabla ya uchanguzi mkuu.”

Akizungumzia amani, amehoji nani anayeiharibu kati ya anayetumia nguvu kusisitiza uchaguzi uende anavyotaka na yule anayeshauri kukaa mezani kufanya mabadiliko ya mifumo.

“Katika hali ya kawaida nani anaharibu amani, anayetumia nguvu na kusisitiza uchaguzi uende anavyotaka yeye au yule anayesema jamani turudi mezani ili tuangalie mifumo yetu ya uchaguzi, kwani kwa mfumo wa sasa hauwezi kutupatia viongozi wa haki na wa kweli?” amehoji.

Ametaka wote waliokamatwa kwa kudai haki wakiwamo viongozi wa vyama vya upinzani waachiwe haraka na bila ya masharti.

Askofu Pisa amesema kusitokee wengine watakaokamatwa au kusumbuliwa kwa namna hiyo.

“Tuiombee nchi yetu, iwe ya amani na kuwa na viongozi wa haki na wazalendo,” amesema.

Katika hatua nyingine, Askofu Pisa amesema kwa misingi ya demokrasia, mamlaka ya Serikali yanatokana na iliyochaguliwa kihalali, akieleza katika demokrasia ya kweli viongozi watawajibika kwa wapigakura.

“Kura ni wakala wenye nguvu, wananchi wasiporwe nguvu yao ya kupiga kura na kuchagua,” amesema.

Amesema hoja zinazoibuliwa na wadau hazionyeshi kupatikana kwa uchaguzi wa haki na kweli, hivyo ni muhimu zizingatiwe ili kupata suluhisho.

Askofu Pisa amesema kukiwa na uchaguzi wa haki, viongozi watakaochanguliwa watakuwa tunda la haki na ukweli.

Kuhusu umuhimu wa mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi, amesema unatokana na malalamiko ya uchaguzi wa mwaka 2019, 2020 na 2024, yanayodai haukuwa wa halali wala wa haki.

“Unamhakikishiaje mwananchi huyo kwamba uchaguzi mkuu utakuwa wa halali? Tangu uchaguzi wa serikali za mitaa ufanyike, bado hata miezi sita haijapita,” amesema.

Amesema kwa bahati mbaya bado kasoro zilizobainishwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa Novemba, 2024 hazijarekebishwa wala kujibiwa.

Amesema tayari mapendekezo kuhusu muundo wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) yalishatolewa, hivyo ni muhimu yatekelezwe.

Ametaka mihimili isiingiliwe, iachwe itende kazi zake kwa haki. Amesema watu wasipochagua kwa uhuru, demokrasia itakufa.

“Madikteta wengi duniani na hata hapa Afrika hawataruhusu uchaguzi ufanyike kwani wanaogopa uchaguzi ukifanyika hawatachaguliwa. Kama wataruhusu uchaguzi wataharibu mifumo ili wabaki madarakani. Tanzania hatujafika huku,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *