Wakazi Kibirizi wataka kukarabatiwa daraja lililofunikwa maji

Kigoma. Wakazi wa Kibirizi mkoani hapa wameitaka Serikali ifanye ukarabati wa daraja lililofunikwa na maji yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha, kwa kuwa wanashindwa kumudu gharama za kupita njia mbadala kufika katika shughuli zao.

Daraja hilo lililokuwa likitumiwa na watembea kwa miguu, pikipiki, bajaji na magari kwa sasa limefunikwa na maji baada ya mvua zilizonyesha mwanzoni mwa mwezi huu.

Wakizungumza na Mwananchi jana Jumamosi, Aprili 19, 2025 baadhi ya watumiaji wa daraja hilo, wamesema wanashindwa kumudu gharama za usafiri, kupita eneo mbadala na lilipo daraja hilo.

Shaabani Ngodoki ni mmoja wa wananchi hao, amesema awali kwenda Kigoma Mjini ilikuwa tunatumia Sh500, lakini sasa wanalazimika kulipa Sh1,500 hadi Sh2,000 kuzungukia barabara ya Kasulu.

“Jambo hili siyo kila mtu anaweza kulimudu kikubwa Serikali ishughulikie changamoto ya barabara hii itengenezwe,” amesema.

Mkazi mwingine wa Kibirizi, Odetha Baraka amesema gharama hizo zinapunguza sehemu ya faida yake kwenye biashara ya samaki.

Ingawa imekuwa chungu kwa baadhi, lakini wapo wanaofaidika nayo, hasa vijana walioamua kujiajiri kuwavusha watu kwa mitumbwi.

Adumba Issa ni miongoni mwa vijana hao, amesema kwa sasa anaendesha maisha yake kwa shughuli hiyo, kiasi kwamba ameachana na uvuvi kwa muda.

“Awali nilikuwa najishughulisha na uvuvi lakini baada ya kutokea kwa changamoto hii, kazi yangu imekuwa kuvusha watu na nauli yetu ni Sh200 kwa mtu mmoja,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dk Rashidi Chuachua amesema kwa hatua ya sasa ni vema wananchi waendelee kutumia Barabara ya Kasulu kutokea Masanga stendi ili kuingia mjini Kigoma.

Hata hivyo, amesema ingawa Serikali imetoa maelekezo ya njia mbadala zinazopaswa kutumika, bado wapo wananchi wanaovuka maeneo yaliyokatazwa, jambo linaloweka rehani usalama wao.

Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na vijijini (Tarura) Wilaya ya Kigoma, Elias Mtapima amesema anaifahamu changamoto hiyo na imesababishwa na ongezeko la maji ya Ziwa Tanganyika tangu msimu wa mvua wa mwaka 2023/2024.

Amesema tayari daraja hilo limeshawekwa kwenye bajeti kwa ajili ya hatua za matengenezo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *