Kigogo CUF atimkia CCM, adai ‘matunda ya msimu’ yamemchosha

Handeni. Chama cha Wananchi (CUF) wilayani Handeni mkoani Tanga, kimepata pigo baada ya Mwenyekiti wake kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kitwanga ametambulishwa rasmi leo Jumamosi Aprili 19, 2025, katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Handeni kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa FDC. Utambulisho huo umefanywa na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo na Kitwanga amekiri mbele ya wajumbe kuwa sasa si Mwenyekiti wa CUF na amekuwa mwanachama halali wa CCM, akiomba ushirikiano kutoka kwa wanachama wa chama hicho.

Akieleza sababu za uamuzi wake, Kitwanga amesema baadhi ya vyama vya siasa nchini hufanya siasa za msimu, tofauti na CCM ambayo kwa maelezo yake huendesha shughuli zake muda wote.

“Kwa sasa mimi si mwenyekiti tena wa CUF wilaya, nimeamua kujiunga rasmi na CCM. Vyama vingi vinafanya siasa kama matunda ya msimu. Kuna msimu wa maembe wa mananasi na kama msimu wa matunda hakuna, inabidi usubiri tu maua yaanze. Nimeona kukaa kwangu CUF, muda mwingi unapotea bila kuwa na mchango wa maana kwa wananchi, hivyo nimeamua kuhamia mahali ambako shughuli zinaendelea muda wote,” amesema Kitwanga.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Handeni, Amiri Changogo amesema chama chao kinampokea Kitwanga kwa mikono miwili.

“Namfahamu huyu bwana kwa muda mrefu, aliwahi kuwa mwanachama wa CCM kabla ya kujiunga na CUF,” amesema Changogo.

Amesema Kitwanga ni mwanasiasa mzoefu na anaamini atakuwa msaada mkubwa kwa CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu kutokana na uzoefu wake katika siasa.

Mwananchi imezungumza na Mjumbe wa Baraza la Uongozi Taifa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CUF wilayani Handeni, Masoud Mhina amesema wamesikia taarifa za kuhama kwake mapema leo.

Amesema tayari walikuwa wameanza kuwa na wasiwasi kuhusu mienendo yake kwa kipindi cha takribani miezi miwili iliyopita, lakini hawakuwa na sababu ya kumzuia.

Amesema kuhama chama ni haki ya kila mtu kikatiba na kidemokrasia. “Kweli alikuwa mwenyekiti wetu wa wilaya. Hatujamfukuza, kaamua kuhama mwenyewe, tunamtakia kila la kheri,” amesema Masoud.

Ameongeza kuwa CUF wilayani Handeni inaendelea na maandalizi ya kumpata mwenyekiti mpya haraka iwezekanavyo ili kuendelea na ratiba za kichama, hasa ikizingatiwa kuwa uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unakaribia.

Hilary Kitwanga ni mwanasiasa mkongwe mwenye uzoefu mkubwa, ambaye tayari amewahi kugombea udiwani mara mbili katika kata ya Vibaoni wilayani Handeni, na mara zote alishika nafasi ya pili nyuma ya wagombea wa CCM.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *