Sowah awatisha Ahoua, Dube akitupia mbili

Dar es Salaam. Nyota wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah amebakiza bao moja kuwafikia Prince Dube wa Yanga na Jean Charles Ahoua wanaoongoza kwa kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya leo kuifungia timu yake mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-0 nyunbani dhidi ya Tabora United kwenye Uwanja wa Liti, Singida.

Mabao hayo mawili ya Sowah yamemfanya afikishe mabao 11 na kuwa nyuma ya Dube na Ahoua kwa bao moja kwa vile nyota hao kila mmoja ana mabao 12.

Mabao ya Sowah katika mchezo wa leo ameyafunga katika dakika ya 52 na lingine alipachika katika dakika ya 86.

Bao la kwanza la Sowah alifunga kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na refa Ramadhan Kayoko baada ya Banele Junior wa Tabora United kumuangusha Iddi Habibu ‘Gego’ katika eneo la hatari.

Katika dakika ya 86, Sowah alifunga bao lake la pili ambalo lilikuwa la tatu kwa Singida Black Stars baada ya kumaliza kwa shuti la wastani, pasi ya Marouf Tchakei.

Bao lingine la Singida Black Stars jana limepachikwa na Victorien Adebayor katika dakika ya 21.

Ushindi huo umeifanya Singida Black Stars kufikisha pointi 53 na kukaa kwa muda katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikingojea matokeo ya mchezo baina ya Kagera Sugar na Azam FC zinazocheza muda huu katika Uwanja wa Kaitaba Kagera.

Azam ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 51 na ikiwa itaibuka na ushindi, itarudi katika nafasi ya tano kwani itafikisha pointi 54.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *