Pasaka kavu kwa wafanyabiashara

Dar es Salaam. Ikiwa zimesalia saa chache kabla ya Wakristo wa Tanzania kuungana na mataifa mengine kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, wafanyabiashara walalalimia kukosa wateja.

Sikukuu hii ya kusherehekea kufufuka kwa Yesu Kristo  hufanyika baada ya kumalizika kipindi cha majuma sita ya Kwaresma.
Kufuatia sikukuu hiyo ya Pasaka watu hufanya maandalizi ya kusherekea siku hiyo kwa kununua mahitaji ya aina mbalimbali ikiwemo nguo na vyakula.

Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara katika soko la Kariakoo wamelalamika kutokuwepo na wateja wengi kama ilivyozoeleka inapofika kipindi cha sikuuu.

Akizungumza na Mwananchi, Abdallah Msami mfanyabiashara wa nguo za watoto katika eneo hilo amesema licha ya bei kuwa himilivu biashara imekuwa tofauti kama inavyokuwa katika kipindi cha sikukuu kutoakana na kupata wateja wachache.

“Kwa siku unaweza ukauza nguo nne au tano wakati awali huwa ni zaidi ya hapo, angalau leo biashara imechangamka,” anasema.
Amina Seif mfanyabiashara wa rejareja viatu anasema licha ya bei za nguo na viatu kuwa za kawaida hakuna wateja.

“Wastani wa bei za nguo ni kati ya Sh15,000 hadi Sh45,000 na viatu ni Sh6000 hadi Sh20,000 hata hivyo wateja ni wachache siyo kama tulivyotarajia,” amesema.

Godbless John moja ya wafanyabiashara wa nguo za watoto amesema kuwa hadi sasa biashara bado ni ngumu wateja ni wa chache siyo kama ilivyozoeleka inavyokuwa katika kipindi cha sikukuu.

Kwa upande wa bidhaa za biashara ya chakula baadhi nimepanda na nyingine zimebaki kuwa katika bei ya kawaida.
Mfanyabiashara wa vyakula Ilala, Suleiman Khamisi amesema hali ya biashara kwa upande wa vyakula ipo kawaida huku akijivunia kupata wateja wengi siku ya leo.

“Nauza mchele, viungo mbalimbali na unga japo soko la unga limetetereka kidogo leo lakini mchele na viungo ipo vizuri,” amesema Khamisi.

Amesema bei ya mchele ni kati ya Sh2000 na Sh3000 kiwango ambacho Mtanzania wa kawaida anaweza kumudu.

Kwa upande wa vitoweo nyama kilo moja ni Sh11,000 hadi 12,000 kwa kilo katika soko la Buguruni, kuku wa kisasa Sh8,500 na kuendelea ambapo mfanyabiashara wa kuku Ilala, James Mwakaleli amesema bei za kuku zinatofautiana kulingana na ukubwa wa kuku.

Kwa upande wa nyanya na vitunguu katika soko la Ilala John Luhanga anasema bei ya nyanya imeshuka kwa kiasi ukilinganisha na ilivyokuwa kipindi cha sikuuu ya Eid.

“Sikukuu ya Eid tenga lilifika hadi Sh100,000 lakini sasa linapatikana 70,000 kwa tenga, vitunguu vimepanda kutoka Sh 1700 hadi 2000,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *