Fadlu aitega Stellenbosch, atoa ombi Simba

Zanzibar. Ikiwa imebaki siku moja kabla ya mechi baina ya Simba na Stellenbosch ya Afrika Kusini utakaochezwa katika Uwanja wa Amaan Complex, Zanzibar, Kocha wa Simba, Fadlu David amesema wamejipanga vizuri katika kuukabili mchezo huo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo, Jumamosi, Aprili 19, 2025, Fadlu amesema timu zote ambazo zimefika nusu fainali zinastahiki kufika hapo hivyo kwa upande wao wamejipanga vyema katika kukabiliana na wapinzani wao na wanategemea matokeo mazuri.

Amesema kwa sasa wanaangalia zaidi katika mchezo wa nusu fainali ambao ndio utakaowapa matokeo ya kufika Fainali hasa wakiwa katika uwanja wa nyumbani.

Amesema, wamejipanga vyema kucheza katika uwanja wa nyumbani ingawaje wao ndio timu ya kwaza kuuzindua uwanja huo tangu kufanyiwa matengenezo.

“Kwa sasa kila mmoja ana upande wa kutetea timu yake hivyo kwa upande wetu tumejipanga vyema kuwatafutia ushindi mashabiki wa Simba,” amesema 

Amesema katika kazi hakuna urafiki badala yake hao ni wapinzani wao ambao wamejipanga vizuri kama wao kwani kuwatoa mabingwa watetezi wa mchezo huo sio jambo dogo.

“Timu hiyo haipaswi kuchukuliwa kwa urahisi kwani kuwatoa mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho sio jambo rahisi kama inavyodhaniwa,” amesema 

Hata hivyo, amesema licha ya kujipanga kwao lakini bado mchezo huo ni mgumu kwani timu hiyo ndio mara ya kwanza kufika nusu Fainali katik mashindano hayo ya CAF.

Kwa upande wake, beki Che Malone amewataka wachezaji wenzake kuwa watulivu katika uchezaji wao kwani kadri ya wanavyoufanya mchezo huo kuwa mgumu ndivyo wanayoifanya timu hiyo kuwa ngumu kwao.

Pia, amesema watazingatia maelezo yote waliyopatiwa na kocha katika kuukabili mchezo huo ili kupata matokeo mazuri

“Tunahitaji hamasa kutoka kwa mashabiki ili kufanikisha mchezo huo uende vizuri,” amesema 

Malone ameahidi kutofanya makosa katika mchezo huo utakaowapatia matokeo ya kufika Fainali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *