
Unguja. Katika jitihada za kuhakikisha Zanzibar inajitegemea kwa chakula, umeandaliwa mradi wa kuendeleza mabonde ya mpunga ambao utatumia Dola za Marekani 5.153 milioni sawa na (Sh13.8 bilioni).
Mradi huo wa msaada wa Maendeleo ya Kimataifa (Oda) unafadhiliwa na Serikali ya Korea kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, ambao utafanya kazi kwa miaka mitatu kuanzia sasa, utasaidia kuendeleza mabonde ya Cheju, Kinyasini, Kilombero, Chaani, Kibokwa ya Unguja na Mlemele kwa upande wa Pemba.
Akizungumza wakati wa kuwapatia mafunzo maalumu jumuiya za wakulima katika bonde la Cheju Mkoa wa Kaskazini Unguja Aprili 19, 2025 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Ali Khamis Juma, amewataka kuzingatia matumizi bora ya zana za kilimo kama wanavyoelekezwa na wataalamu ili kuondokana na kilimo cha mazoea badala yake wajikite katika kilimo biashara.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia wizara ya kilimo itaendelea kuimarisha kilimo cha mpunga ili kuongeza uzalishaji wa chakula kwa kuhimiza matumizi bora ya miundombinu maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba,” amesema.
Amesema wanalenga kuwapatia taaluma wanachama wa jumuiya hao kwa ajili ya matumizi ya zana za kilimo za kisasa ili kuweza kuondokana na mbinu za kizamani kwenye uzalishaji wa zao hilo.
Awali akizungumza kwa niaba ya wanachama wenzake, mkulima Khadija Rajab Ali, amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo na kuwaendeleza kulima katika mabonde yao yaliyowekwa miundombinu mipya pamoja na vifaa vitakavyotolewa na mradi kwa ajili ya kuimarisha maeneo yao ya kilimo ili waweze kujipatia sio tu chakula, pia na kipato.
Amesema wakulima wengi bado hawana uelewa wa matumizi ya mbegu na zana za kisasa na ndio maana kilimo chao kimeendelea kuwa duni lakini kupitia mafunzo hayo huenda yakaleta mabadiliko na kuinua kilimo katika visiwa hivyo.
Ameomba elimu hiyo isambae kwa wakulima wengine zaidi ili wafanikiwe kwa pamoja kuongeza uzalishaji wa zao hilo na mazao mengine ambayo yanalimwa Zanzibar.
“Hii elimu ni muhimu sana kwani bado wakulima wengi hawana uelewa kuhusu zana za kilimo za kisasa, ndio maana hata mazao yanakuwa machache kwa sababu ya kilimo cha mazoea, kwa hiyo tunapongeza lakini tunaomba iendelee na isambae zaidi kwa wakulima wote,” amesema mkulima mwingine Othman Haji Mzee.
Jumuiya 13 za wakulima wa umwagiliaji wa bonde la Cheju wamepatiwa mafunzo hayo ambapo mradi huo unatarajiwa kunufaisha mabonde sita ya kilimo cha mpunga kwa miaka mitatu.