Mafinga. Ajali ya gari la kubebea wagonjwa imekatisha matumaini ya watu saba ya kuiona Sikukuu ya Pasaka inayosherehekewa kesho Jumapili, Aprili 20, 2025, na waumini wa dini ya Kikristo, ikilenga kuadhimisha kufufuka kwa Yesu Kristo.
Hilo ni baada ya watu hao kupoteza maisha na wengine 15 kujeruhiwa, katika ajali iliyohusisha ari hilo lililogongana uso kwa uso na pikipiki yenye magurudumu matatu, maarufu kama Toyo, katika eneo la Luganga, barabara ya Mafinga–Mgololo, mkoani Iringa.
Kati ya waliopoteza maisha katika ajali hiyo, wanawake ni sita waliofariki dunia papo hapo na mwanaume mmoja aliyefariki wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Mkuu wa Wilaya ya Mafinga, Dk Linda Salekwa leo, Jumamosi Aprili 19, 2025, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, huku Hospitali ya Mji wa Mafinga nayo ikithibitisha kuwapokea majeruhi na miili ya waliofariki dunia.

Kwa mujibu wa Dk Salekwa, waliopoteza maisha ni abiria waliokuwepo ndani ya Toyo na inadaiwa walikuwa safarini kwenda shambani wanakofanya shughuli zao za kila siku.
Simulizi za manusura
Unaposikia kifo hakitamfikia asiye na ahadi, basi Farida Abedi ana ushuhuda wa hilo, baada ya kile anachoeleza kuwa alipaswa kuwa miongoni mwa abiria katika Toyo hilo, lakini ilishindikana.
Sababu ya kushindikana, amesema, ni kuchelewa na kukuta Toyo imeshaondoka, hivyo akiwa na mwenzake walilazimika kupanda bodaboda kuifukuzia.
Amesema mbio za bodaboda zikaishia katika eneo ambalo walishuhudia Toyo hiyo ikiwa imeharibiwa vibaya na ajali hiyo .na miili ya watu waliopoteza maisha ikiwa imelazwa kandokando ya barabara.
“Mimi na mwenzangu tumetoka nyumbani kwenda shambani, lakini kwa siku ya leo (Aprili 19), Toyo ilituacha tulivyokuwa tunawasiliana na wenzetu. Tukapanda pikipiki kuifukuzia, lakini tulipofika eneo la Luganga tukakuta wenzetu wamepata ajali,” amesema.
Kwa mujibu wa Farida, Toyo hiyo ni usafiri wao wa kila siku kwenda shambani, na mara nyingi hupanda kati ya abiria 21 hadi 24.

Isala Zugala, dereva wa pikipiki, amesema aliambiwa kuwa kuna ajali, ndipo alipofunga safari hadi eneo la tukio kujionea.
“Nilikuja kuangalia maana unaposikia kuna ajali huwezi kujua, pengine kuna ndugu yako, ndiyo maana nimekuja, lakini tumefika tumekuta kuna baadhi wamepakiwa kwenye gari la wagonjwa na wengine wachache wakiwa wamefariki dunia,” amesema.
Kauli ya Kamanda wa Polisi
Akizungumza kwa simu na Mwananchi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Meloe Buzema, amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari la wagonjwa, mali ya Halmashauri ya Mji wa Mafinga, aliyekuwa akiendesha kwa mwendo kasi.
Amesema dereva huyo anayefahamika kwa jina moja la Mose, amekimbia baada ya ajali hiyo.
“Jeshi la Polisi linaendelea na juhudi mbalimbali ili kuhakikisha anapatikana na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria,” amesema Kamanda Buzema.
Aidha, ametoa wito kwa madereva wa magari ya wagonjwa kuzingatia sheria za barabarani. Amesema wanapaswa kuzifuata kama madereva wengine.
Amesema kuwepo kwa ving’ora kwenye magari hayo hakuwapi ruhusa ya kuvunja sheria kwa kuendesha mwendo kasi na vitendo vingine vinavyovunja sheria ya usalama barabarani. Amesema ving’ora vya magari hayo ni kwa ajili ya kuwasaidia kupata kipaumbele barabarani wanapokuwa na dharura.
“Endapo hakuna mgonjwa ndani ya gari, hakuna sababu ya kuendesha kwa mwendo kasi kupita kiasi, jambo ambalo linaweza kusababisha madhara makubwa kama haya yaliyotokea,” amesema kamanda huyo.
Kauli ya DC
Dk Salekwa amesema taarifa zinaonyesha watu hao walikuwa wanakwenda shambani kufanya kazi, ndipo gari hilo la kubebea wagonjwa likawagonga wakiwa kwenye Toyo.
Amesema hadi sasa majeruhi wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Mji Mafinga, kati yao wanne wana hali mbaya, hivyo wamepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Mkoa wa Iringa.
Hata hivyo, amewataka wananchi kuacha kutumia vyombo visivyo rasmi kusafiria, kwa kuwa ni maalumu kwa ajili ya mizigo.
“Ukijaribu kufikiria kwa hali ya kawaida watu 22 kupanda kwenye Toyo ni wengi sana… hivyo, wananchi, hata kama tunatafuta fedha, basi tuzitafute kwa namna salama. Unaweza kuona kwamba nia yao ilikuwa ni kwenda shamba, lakini wengine wameishia hospitali na kupoteza maisha,” amesema.
Amesema ajali hiyo imetokea saa alfajiri ya kuamkia leo, muda ambao watu huutumia kwenda shambani. Pengine, wangetumia usafiri mwingine wangekuwa salama.
Awali, akizungumzia tukio hilo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Mafinga, Dk Victor Msafiri, amesema walipokea majeruhi 15 na miili ya wanawake sita na mwanaume mmoja aliyefariki wakati akipatiwa matibabu.
Amesema kati ya majeruhi hao, wanawake ni wanane na wanaume saba, na wanaendelea na matibabu kwenye hospitali hiyo, huku wanne wamepewa rufaa.
Ametaja majeruhi hao kuwa ni Jonas Chaula (17), Devotha Mkwele (42), Veronika Mbilinyi (49), Tumaini Mbilinyi (32), Benedict Mlengula (18), Adofu Ndanzi (27), Beatrice Kimbe (35) na Innocent Mgimwa (21).
Wengine ni Shania Ngisha (33), Faraha Kikoti (41), Elia Mbembati (17), Sauda Kimata (30), Jenifa Lyuvale (28), Robati Mgimwa na Stephano Cholela (19), wote ni wakazi wa Mtaa wa Amani, mkoani Iringa.
Amesema kwa sasa .bado wananchi wanaendelea kutambua miili ya marehemu waliopata ajali kwa ajili ya taratibu nyingine.