CAG Kichere afukua ‘uozo’ vyama vya siasa

Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeibua madudu katika vyama vya siasa kwa kueleza kuwa baadhi ya vyama hivyo mali zake zimesajiliwa kwa majina binafsi, huku vingine vikiwa na dosari katika ukusanyaji wa mapato yake.

Pia, ripoti ya ukaguzi wa Serikali Kuu iliyotolewa na CAG, Charles Kichere, imeeleza kuwa baadhi ya vyama havijafanya mikutano yake ya kikatiba, huku vingine vikiwa havina viongozi kulingana na muundo wake.

“Ukaguzi wangu ulibaini kuwa kiwanja namba 37 kilichopo Ilala, chenye jengo kilichonunuliwa mwaka 1998 na chama cha NCCR-Mageuzi chenye thamani ya pamoja na jengo Sh145.06 milioni, kilisajiliwa kwa jina la mtu binafsi badala ya Bodi ya Wadhamini, licha ya mapendekezo yangu ya awali kuhusu usajili sahihi wa mali.

“Zaidi ya hayo, nilibaini kuwa chama cha CUF kina magari 10 yenye thamani ya Sh274.93 milioni, yaliyonunuliwa kati ya mwaka 2012 na 2015, lakini magari haya yalisajiliwa kwa majina mbalimbali ya watu binafsi.”

Changamoto za umiliki wa mali nyingine zilibainika, ambapo mali ya NCCR-Mageuzi yenye thamani ya Sh145.06 milioni na magari 10 ya CUF yenye thamani ya Sh274.93 milioni bado yamesajiliwa kwa majina ya watu binafsi badala ya Bodi za Wadhamini wa vyama hivyo, hali inayosababisha hatari za kisheria na kudhoofisha udhibiti wa kifedha.

Kichere amesema hali hiyo ni kinyume cha Ibara ya 26(7)(a) ya Katiba ya NCCR-Mageuzi ya mwaka 2020, inayotoa majukumu kwa bodi ya wadhamini kusimamia mali zote za chama, zisizohamishika na zinazohamishika.

Ripoti imeeeza kuwa hali hiyo ilisababishwa na changamoto katika mchakato wa usajili, hivyo kuleta hatari ya migongano ya kisheria juu ya umiliki wa mali hizo na kupunguza uwajibikaji. Pia, inadhoofisha mfumo wa utawala bora wa vyama na inaweza kuhatarisha utulivu wa kifedha na kuathiri uendelevu wa shughuli zao.

“Ninapendekeza kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa ahakikishe vyama vya NCCR-Mageuzi na CUF vinahamisha umiliki wa mali kutoka kwa watu binafsi kwenda kwa bodi zao za wadhamini,” amesema.

Pia, ukaguzi wa CAG umebaini upungufu katika usimamizi wa fedha, utawala na mali ndani ya vyama vya siasa. Upungufu wa mapato ulibainika, ambapo vyama 10 vya siasa vilishindwa kukusanya Sh133.26 milioni kutoka kwa michango ya wanachama na ruzuku, hali iliyopunguza uwezo wao wa kifedha.

Aidha, Sh31.7 milioni za michango hazikuwekwa benki, jambo lililokiuka matakwa ya kisheria na kuongeza hatari ya matumizi mabaya ya fedha.

Pia, mapungufu ya utawala yalionekana, ambapo vyama vya Demokrasia Makini (DM) na National Reconstruction Alliance (NRA) havikuandaa mikutano ya kisheria, hali iliyokiuka Kanuni ya 24(1) ya Kanuni za Baraza la Vyama vya Siasa ya mwaka 2019 na kudhoofisha utawala bora.

Mapungufu hayo ya usimamizi wa fedha na utawala yanadhoofisha uwajibikaji, ufanisi wa kiutendaji na uthabiti wa vyama vya siasa.

Kifungu cha 18A(2)(a) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 (iliyorekebishwa mwaka 2019), kinataka vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa kuwasilisha taarifa zao za fedha kwa ajili ya ukaguzi ifikapo Septemba 30 ya kila mwaka.

Ukaguzi wake ulibaini kuwa vyama viwili vya siasa, Chama cha Kidemokrasia cha Muungano (UDP) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) — vilichelewa kuwasilisha taarifa za fedha kwa makadirio ya kati ya siku 29 hadi 34.

Uongozi wa vyama vya siasa ulieleza kuwa uchelewaji huo ulitokana na kuchelewa kwa mchakato wa uandaaji wa taarifa za fedha.

“Ninapendekeza Msajili wa Vyama vya Siasa achukue hatua stahiki kuhakikisha kuwa vyama vya UDP na Chadema vinawasilisha taarifa zao za fedha kufikia tarehe 30 Septemba ya kila mwaka,” amependekeza CAG.

Vilevile, CAG katika ripoti hiyo ameeleza kuwa Kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 (iliyorekebishwa mwaka 2019), kinataka kila chama cha siasa kilichosajiliwa kisheria kufungua akaunti ya benki ya chama ambayo mapato yote yanayopatikana kutokana na ada za uanachama, michango ya hiari, misaada, ruzuku au mapato ya uwekezaji yanapaswa kuwasilishwa benki.

“Licha ya pendekezo langu katika miaka iliyopita, nilibaini kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24, vyama vinne vya siasa vilikusanya jumla ya Sh31.7 milioni bila kuwasilisha katika akaunti za benki za vyama husika,” amesema CAG.

Amesema hali hiyo ilitokana na mazoea ya muda mrefu ya kutumia fedha zinazokusanywa na kuepuka gharama za uendeshaji wa akaunti za benki, hivyo kusababisha akaunti za benki kutotumika.

Amesisitiza kuwa kushindwa kuwasilisha fedha za makusanyo ya michango ya wanachama katika akaunti za benki kunaweza kusababisha matumizi mabaya ya fedha. Pia, kunaweza kusababisha hali ya kutofautiana kwa kumbukumbu za kihasibu, na zaidi kunaondoa uwazi katika utendaji.

“Ninapendekeza kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa ahakikishe makusanyo ya fedha yanawasilishwa kwa wakati katika akaunti za benki za vyama vya siasa,” amesema.

Kadhalika, CAG katika ukaguzi wake amebaini kuwa kati ya Februari 15, 2020 na Julai 18, 2020, NCCR-Mageuzi iliingia mikataba na wakopeshaji watano yenye jumla ya Sh135 milioni kwa ajili ya kusaidia gharama za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Kifungu cha 5 cha makubaliano ya mikopo kati ya NCCR-Mageuzi na wakopeshaji mbalimbali kilitaka chama hicho kurejesha fedha bila riba ndani ya miezi 28.

Hata hivyo, mikopo hiyo haijarejeshwa kwa zaidi ya miaka mitano (miezi 60), na hilo lilisababishwa na uhaba wa kifedha unaokikabili chama hicho.

Hata hivyo, kushindwa kulipa mikopo ya muda mrefu kunakiuka masharti ya makubaliano, hivyo kuharibu sifa ya kukopeshwa na kupunguza uwezo wa kupata mikopo mingine baadaye.

“Ninapendekeza kuwa chama cha NCCR-Mageuzi kitafute fedha na kuandaa mpango wa ulipaji wa deni la Sh135 milioni. Pia, kifanye majadiliano na wakopeshaji kuhusu kurekebisha masharti ya malipo,” amesema.

Katika hatua nyingine, CAG amebaini kuwa vyama vya Demokrasia Makini (DM) na National Reconstruction Alliance (NRA) vilishindwa kufanya mikutano ya Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya Taifa. Hii ilisababishwa na uhaba wa fedha za kuendeshea mikutano.

Kushindwa kufanya mikutano ya kisheria kunachelewesha mchakato wa kutoa maamuzi muhimu ya vyama, hivyo kuathiri mfumo wa utawala, mipango ya kimkakati na ufanisi wa shughuli za vyama.

Amesema kutokufanyika kwa mikutano ya kisheria ya vyama vya siasa kunakiuka Kanuni ya 24(1) ya Kanuni za Baraza la Vyama vya Siasa ya mwaka 2019, inayovipa mamlaka vyama vya siasa kufanya mikutano miwili ya Halmashauri Kuu na miwili ya Kamati Kuu ya Taifa ili kuhakikisha utawala bora na maamuzi ya kimkakati.

“Ninapendekeza kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa ahakikishe kuwa vyama vya Demokrasia Makini (DM) na National Reconstruction Alliance (NRA) vinatenga fedha za kutosha kuwezesha kufanyika kwa mikutano ya kisheria kwa wakati,” amependekeza CAG.

Ukaguzi wake pia umebaini kuwa chama cha NCCR-Mageuzi kilikuwa na nafasi wazi za Makamu Mwenyekiti kutoka Zanzibar na Katibu Mkuu Msaidizi kutoka Bara tangu Agosti 2023.

Hali hiyo imeisababishwa na viongozi waliokuwepo kuteuliwa na kupangiwa majukumu mengine, hivyo kuacha nafasi zao katika chama zikiwa wazi.

Amesema Ibara ya 27 ya Katiba ya NCCR-Mageuzi ya mwaka 2020 inawatambua Makamu Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kitaifa kutoka Zanzibar na Katibu Mkuu Msaidizi kutoka Bara kama viongozi wa juu wa chama, ambao husimamia shughuli za chama na kusaidia majukumu ya Katibu Mkuu.

“Uchelewaji wa muda mrefu wa kuitisha vikao vya kamati kuu kwa ajili ya kuteua viongozi umesababisha ukosefu wa uongozi madhubuti na kuchelewesha maamuzi muhimu na muelekeo ndani ya chama. Kukosekana kwa viongozi wa juu wa chama kunahatarisha uchelewaji wa kufanya maamuzi, kunapunguza ari ya kazi na kunaathiri ufanisi wa shughuli, jambo linalopunguza uwezo wa chama kufikia malengo yake,” amesema.

CAG amependekeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ihakikishe kuwa NCCR-Mageuzi inateua Katibu Mkuu Msaidizi kutoka Tanzania Bara na Makamu Mwenyekiti kutoka Zanzibar bila kuchelewa zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *