Dar es Salaam. Carolina Hawa a.k.a Carina. Hatunaye! Ndiyo, katangulia mbele ya haki. Kwa maradhi ya tumbo. Ni tatizo la muda mrefu, lililomsumbua hadi kupelekwa India kwa matibabu zaidi. ‘Soo sadi’!
Sanaa ya filamu imempoteza msanii. Mtaa umepoteza mrembo, Magomeni imepoteza balozi. Familia imepoteza mtoto, dada, anti na jembe. Pole kwa wote, pole zaidi kwa Mama Carina. Hii dunia tumekodisha tu.
Kwa waliokuwa wanafuatilia taarifa za kuumwa kwake na kupelekewa India mpaka umauti wake, bila shaka kuna hisia kali zaidi juu ya kifo hiki. Tofauti na wale waliosikia kifo tu. Kateseka sana dada yetu. Tumbo!

Tumbo lile lile lenye kutubeba waja na kutuleta duniani. Ndilo lililomtesa dada Carina na kumuondoa duniani. Mungu ampe pumziko la milele. Tunafahamu huko aliko hatoumwa tena. Hatolia na kuugulia tena. Ameni!
Miaka na miaka Carina amekuwa na tatizo hilo. Vyombo vya habari mara kadhaa viliripoti taarifa zake. Mbali na kuripoti tatizo husika, pia vilitumika kuomba msaada wa matibabu yake. Pole kwa mama yake.
Kwa wasichana wa mjini, waigizaji wa kike, na binti zetu kwa ujumla wake kuna somo kupitia msiba wa Carina. Utu, urafiki, kusitiriana na ushirikiano. Msiba huu liwe funzo kwetu tulio hai na bado tunavuta pumzi. Yes!
Funzo kwa mtoto wa kike unayefanya upuuzi mitandaoni, ukirekodi faragha zako. Ukisambaza kwenye mitandao. Ukitaka ‘utrendi’, jina lako litajwe kwa upuuzi. Tambua maisha haya tunapita tu. Ni mafupi sana na hayarudi tena.
Ambaye hukui kiakili. Hutaki kuukubali utu uzima. Unauchukia uzee. Hutulii na hutaki kuukubali ukweli kwamba umepitwa na muda. Hutaki kuamini kama wako umri umeenda. Hii dunia ni njia tunapita tu. Muda wako waja.
Kuwapa moyo watu sampuli hii ni kuwapoteza zaidi. Bora tuwe wakweli. tunahitaji siyo tu kubadili tabia bali mitazamo ya jamii. Kwa sababu jamii yetu inajenga bintiz wajinga. Hawajui kama afya zetu tumeazima. Leo nadili na bintiz tu.

Wanaua ‘brandi’ za familia. Wanaua biashara, wanaua na ndugu zao. Yes! Wanaoteseka ni ndugu ambao wapo nao siku zote hadi kifo chao. Dunia hii imelaza wengi ardhini kuliko walio hai. Lakini hatujifunzi kila siku.
Unaweza kutengwa na ‘boyfrendi’ au shostiako. Lakini ndugu utakuwa nao mpaka unaoza. Unapofanya madudu ndugu zako huumia zaidi kuliko rafiki zako. Poteza muda tafakari hili kwa kina. Utanielewa. Na utaacha upuuzi.
Unaweza kuwa umezoea ‘skendo’ na maneno ya watu, lakini wanaoteseka ni nduguzo na watakaoteseka zaidi ni kizazi chako. Mabinti wa leo kama mmerogwa au kukata tamaa! Dunia ni daraja la uhai na kifo.
Tukio moja linagharimu maisha miaka nenda rudi. Na binti zetu hawakomi. Kutaka kujenga majina kimitandao, hulazimika kufanya mengi ya kijinga. Lakini ufupi wa ‘laifu’ uwatishe basi. Kwamba tuna muda mfupi wa kuishi.
Kama tuna muda mfupi namna hii. Basi tutumie huu muda mfupi vizuri ili tukumbukwe kesho. Tukiwa hatupo tena mbele ya uso wa dunia. Lakini tunapofanya mambo kama tutaishi milele tunakosea.
Hutaki kuishi katika hofu. Hofu ya maisha ya leo na maisha yajayo. Mitandaoni kama Insta, unakutana na pisi kali mpaka unaogopa. Picha mpya deile, nywele mpya deile, nguo mpya deile. Kumbe na danga jipya deile.
Na zaidi maeneo anayopigia picha ni tofauti tofauti. Hayafanani na maisha ya ‘mtizii’ wa kawaida. Walah unaweza kutamani kushika bunduki. Ukidhani umechelewa kupata maisha mazuri. Unasahau kama dunia ni njia tu.
Kadiri unavyomfuatilia katika ukurasa wake. Ndivyo na wewe unaanza kuishi kwa mawazo ya kuchelewa ‘laifu’ na kuhisi kutengwa na dunia ukidhani ni wewe tu unayekula ugali bamia nchi hii. Kumbuka tutaacha kila kitu hapa hapa.
Ukiishi kwa tamaa na wivu wa kijinga, na maisha yako yatakuwa ya kijinga. Kila ufanyalo kumbuka na ufupi wa maisha. Kwamba leo kesho haupo, unawaachia nini walio nyuma yako? Kifo hakina hodi wa ‘alamu’.
Vyovyote iwavyo ukiwa staa hasa wa kike, kujidhalilisha mitandaoni siyo kitu poa. Mungu kaweka tofauti ya wanyama na wanadamu kwa utashi wa kifikra. Usiishi kama mbuzi kwa kukosa utashi? Tunapita hapa.
Wakati tukijiandaa kuupokea mwili wa kipenzi chetu Carina. Ni wakati sahihi wa kuwaza kesho yetu, kesho ya wale watakaobaki tukiwa hatupo. Tufikiri namna maisha yalivyo mafupi. Siyo kosa kuwaza haya bali ni hekima.
Carina ni mmoja kati wapendwa wetu wengi waliotangulia mbele za haki. Kama kabla hukuwaza hili basi tumia msiba huu kuwaza hili. Kwamba tupo duniani ili tuishi na kuondoka. Dunia hii ni njia tu, kuna sehemu tunaenda.
Tunapomlilia Carina. Tuliobaki na sisi tuombe mwisho mwema. Mungu wa Yakobo, Mungu wa Isaka. Atupe afya njema na mwisho usio na mateso. Apangalo yeye halina makosa, ila waja ndo wenye makosa. Naam!
Wasanii tuwe sehemu ya ujenzi wa dunia njema. Dunia tulivu. Dunia yenye amani. Tustawishe utu, tulinde maadili na kuchunga nyendo. Tusiwe sehemu ya uharibifu bali sehemu ya ujenzi na kuimarisha kizazi hiki kibaki salama.
Maisha ni mafupi sana. Binamu tuna muda mfupi sana duniani. Tuutumie vizuri ili nyuma yetu iwe salama. Mungu amlaze mahala pema Carina.