Moshi. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ameonyesha masikitiko yake kutokana na kutoanza kwa mradi wa Chuma Liganga, licha ya fidia kubwa kulipwa kwa watu walioathirika na mradi huo.
Wakati ripoti hiyo ya CAG ya mwaka wa fedha 2023/2024 ikieleza hayo, Februari 18, 2025, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo alinukuliwa akisema Serikali iko hatua za mwisho za kimkataba katika utekelezaji wa mradi huo.
Mradi huo unakadiriwa kuzalisha mapato ya zaidi ya Dola bilioni 1.2 za Marekani kila mwaka ambazo ni karibu Sh3 trilioni za Tanzania kutokana na uzalishaji wa madini ya Chuma, Titani, Vanadium, na Sulfati ya Alumini
Mradi wa Chuma Liganga ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayolenga kuimarisha uchumi wa viwanda wa Tanzania kwa kuanzisha sekta za msingi zitakazosaidia sekta nyingine katika mnyororo wa thamani.
CAG, Charles Kichere amebainisha kuwa mradi huo ulianzishwa mwaka 2011 chini ya mkataba wa ubia kati ya Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na Kampuni Mshirika.

Katika taarifa yake, amesema ingawa hatua ya awali ya kutambua rasilimali ilikamilika ndani ya miezi 36 hadi mwaka 2014, hatua zilizofuata za uendelezaji wa mgodi na ujenzi wa kiwanda cha kuyeyusha madini ya chuma bado hazijakamilika kutokana na kuchelewa kwa majadiliano na changamoto za kisheria.
“Licha ya mapendekezo yangu ya awali katika mwaka wa fedha 2020/21 kuhusu kuhakikisha utekelezaji wa mradi huu, hakuna maendeleo yaliyofanyika”amesema CAG katika taarifa hiyo iliyokabidhiwa bungeni Aprili 16, 2025.
“Ingawa fidia kubwa imelipwa kwa watu waliothirika na mradi, bado kuna majadiliano kuhusu motisha za kampuni mshirika kama vile msamaha wa ushuru wa bidhaa, ushuru wa forodha, na kodi ya ongezeko la thamani kwa vifaa vya ujenzi wa mradi, jambo linalochelewesha utekelezaji wa mradi”
CAG amefafanua kuwa Sheria ya Uwekezaji, Sura ya 38 ya mwaka 2002, inataka motisha hizi zichapishwe kwenye Gazeti la Serikali, jambo ambalo bado halijafanyika.
Zaidi ya hayo, CAG amebainisha kuwa kati ya motisha 29 zilizopendekezwa, 19 zinakabiliwa na changamoto za utekelezaji kutokana na kukinzana kwa sheria za kitaifa, ikiwemo Sheria ya Fedha ya 2015 na Sheria ya Madini ya 2017, ambazo ziliwekwa ili kulinda rasilimali za taifa.
“Ingawa tathmini ya athari za mazingira imefanyika na watu waliothirika wamelipwa fidia, kutokuwepo kwa makubaliano kati ya Serikali na mwekezaji kumeufanya mradi kusimama,” ameeleza CAG na kuongeza;-
“Matokeo yake, faida kubwa za kiuchumi, kama vile ajira na ukuaji wa viwanda, hazijapatikana,” amesisitiza CAG katika taarifa yake hiyo.

“Ucheleweshaji huu wa muda mrefu katika utekelezaji wa mradi umesababisha kupoteza fursa za ajira na kuzuia maendeleo ya viwanda nchini Tanzania”
CAG ameeleza kuwa mradi huo ulitarajiwa kuchochea ukuaji wa sekta zinazotegemea chuma, hivyo ucheleweshaji wake unaweza kuongeza gharama za utekelezaji na kupoteza fursa za kiuchumi.
Amependekeza Shirika la Maendeleo ya Taifa, kupitia Wizara ya Viwanda, liharakishe majadiliano na mwekezaji ili kufikia makubaliano ya mwisho.
Lihakikishe pia utekelezaji wa mradi unafuata mifumo sahihi ya kisheria, na lifuatilie kwa karibu na kutatua changamoto za kisheria kwa wakati, ili kuzuia ucheleweshaji zaidi na kufungua fursa za kiuchumi za mradi wa Chuma Liganga.
Kauli ya Waziri Jafo
Februari 18,2025 Waziri Jafo alipofika katika mradi huo pamoja na mlima mdogo wa Maganga Matitu wilayani Ludewa, alitoa hakikisho kuwa Serikali iko hatua za mwisho za kimkataba, ili mradi huo uanze kazi mapema mwaka 2025.
“Imani yetu ni kwamba ndani ya mwaka huu 2025, Mungu akijaalia mradi huu ambao ni mkombozi kwa uchumi wetu kwa kuokoa fedha nyingi inayotumika kuagiza chuma nje ya nchi uanze,”alisema Waziri Jaffo na kuongeza:-
“Kwa sababu malighafi ya chuma ni muhimu katika ujenzi wa madaraja, barabara, majengo pamoja na matumizi mbalimbali”
Jaffo alinukuliwa akiwahakikishia wananchi wa kijiji cha Mudindi kuwa Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuweka miundombinu wezeshi kama barabara, umeme wa viwandani na maji ili kuwezesha mradi huo kutekelezeka kwa ufanisi.
Kaimu Mkurugenzi wa NDC linalosimamia miradi hiyo, Esther Mwaigomole, alisema kuanza kwa mradi huo ambalo Liganga utadumu kwa miaka 50 na Maganga miaka 25, Tanzania itakuwa nchi ya nne Afrika kwa uzalishaji chuma.